Dec 19, 2018 11:39 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 792 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 36 ya Ya-Sin. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 20 na ya 21 ambazo zinasema:

وَجَاءَ مِنْ أَقْصَى الْمَدِينَةِ رَجُلٌ يَسْعَىٰ قَالَ يَا قَوْمِ اتَّبِعُوا الْمُرْسَلِينَ

Na akaja mtu mbio kutokea upande wa mbali wa mjini, akasema: Enyi watu wangu! Wafuateni (hawa) walio tumwa. 

اتَّبِعُوا مَن لَّا يَسْأَلُكُمْ أَجْرًا وَهُم مُّهْتَدُونَ

Wafuateni wasiokuombeni ujira, hali ya kuwa wenyewe wameongoka. 

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia juhudi kubwa zilizofanywa na Mitume kadhaa wa Allah kwa ajili ya kuwaelekeza kwenye uongofu watu wa kaumu yao. Aya hizi zinaendeleza maudhui hiyo kwa kusema: baadhi ya waumini huwa tayari kukabiliana na watawala madhalimu hata kwa kuyatoa mhanga maisha yao kwa ajili ya kuwahami na kuwalinda Mitume wa Mwenyezi Mungu. Mtu mmoja aliyekuwa akiitwa Habib Najjar, alisikia kutokea mbali ya mji kwamba watu wamedhamiria kuwafanyia maudhi na hata kuwaua Mitume hao wa Allah. Kwa hivyo alifanya haraka kukimbilia mjini ili kutaka msaada kwa watu wengine. Kwa kuwa Habib Najjar alikuwa muumini wa kweli alijua kwamba inapasa yeye mwenyewe awe na imani ya kweli na vilevile awalinganie watu wengine wito wa kuiamini haki ili maadui wasiweze kuwadhuru na kuwaondoa Mitume wa Allah ambao kusudio lao ni kuwaelekeza watu tu kwenye uongofu na wala hawataraji kupata malipo yoyote yale ya kimaada kutoka kwao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuihami dini na viongozi wa haki ni moja ya wajibu na majukumu waliyonayo waumini. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mtu kuwa peke yake bila ya msaidizi hakumzuii kutekeleza jukumu lake la kuilinda na kuihami dini. Baadhi ya wakati inabidi mtu asimame na kuchukua hatua peke yake. Na wala tusihofu kuwa wachache kiidadi katika njia ya kutetea haki. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba tuwafuate watu walioshikamana na njia ya uongofu na wenye uhakika kuwa njia hiyo wanayofuata ni sahihi na ya haki.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 22 hadi 24 ambazo zinasema:

وَمَا لِيَ لَا أَعْبُدُ الَّذِي فَطَرَنِي وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ

Na kwa nini nisimuabudu Yule aliye niumba na kwake mtarejeshwa?

أَأَتَّخِذُ مِن دُونِهِ آلِهَةً إِن يُرِدْنِ الرَّحْمَـٰنُ بِضُرٍّ لَّا تُغْنِ عَنِّي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا وَلَا يُنقِذُونِ

Je! Niishike miungu mingine badala yake? Arrahmani, Mwingi wa Rehema, akinitakia madhara uombezi wa hao hautanifaa kitu, wala hawataniokoa.

إِنِّي إِذًا لَّفِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ

Basi hakika mimi hapo nitakuwa katika upotovu ulio dhaahiri.

Yule mtu muumini aliyetoka sehemu ya mbali ya mji na kwenda kutaka msaada kwa ajili ya kuwahami Mitume wa Mwenyezi Mungu, aliitetea imani yake ya Tauhidi kwa kuwaambia wapinzani: mimi sioni hoja yoyote ya kunifanya niabudu masanamu na miungu yenu ya kubuni ilhali ninajua kwamba Allah, aliye Mola Mrehemevu ndiye aliyeniumba mimi; kwa hivyo kama mimi ninataka kuabudu, mwenye kupasa kuabudiwa ni Yeye Mola. Kumwabudu Mola Muumba ni jambo lenye hoja ya kiakili na mantiki; na pia linaendana na wito utokao kwenye batini ya mtu wa fitra na maumbile yake; lakini kuabudu kwenu nyinyi hiyo miungu yenu bandia hakuna msingi wala hoja inayokubalika kiakili. Kwa sababu kama mtu yeyote yule atataka kunidhuru, miungu hiyo haiwezi kunilinda na hatari hiyo, na kama kuna mtu atataka kuninufaisha kwa jambo, haitoweza kunizuia kupata manufaa hayo. Ni wazi kwamba kuiweka pembeni nafasi ya akili na maumbile, yaani fitra ya ndani ya nafsi ya mtu humfanya mtu apotoke; na hakuna hoja yoyote ya kutetea na kuhalalisha jambo hilo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kumwabudu Muumba ni jambo linalokubalika; lakini kuiabudu miungu bandia na ya kubuni hakuna hoja yoyote ya kiakili ya kukuhalalisha. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa si asili tu ya mwanadamu ya kuumbwa kwake inatokana na Allah lakini hatima na mwisho wa uhai wake pia uko kwenye mamlaka yake Yeye Mola. Kama ni hivyo, inapasa kumwabudu Yeye; na kuabudu huko kunaafikiana na akili ya mwanadamu na wito wa fitra na maumbile ya ndani ya nafsi yake.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 25 hadi 27 ambazo zinasema:

إِنِّي آمَنتُ بِرَبِّكُمْ فَاسْمَعُونِ

Hakika mimi nimemuamini Mola wenu Mlezi, basi nisikilizeni!

 قِيلَ ادْخُلِ الْجَنَّةَ ۖ قَالَ يَا لَيْتَ قَوْمِي يَعْلَمُونَ

Ikasemwa: Ingia Peponi! Akasema: Laiti kaumu yangu wangeli jua.

بِمَا غَفَرَ لِي رَبِّي وَجَعَلَنِي مِنَ الْمُكْرَمِينَ

Jinsi Mola wangu Mlezi alivyo nighufiria, na akanifanya miongoni mwa walio hishimiwa.

Baada ya kutoa hoja zake, muumini mwanamapambano aliyesimama kuwahami na kuwaunga mkono Mitume, alitangaza kuwa, mimi nimewaamini Mitume hawa na ninakulinganieni nyinyi pia muwakubali. Kwa hivyo yazingatieni na kuyatafakari maneno yangu. Hata hivyo nasaha na mawaidha yake yalikuwa kazi bure. Makafiri wenye inadi, ambao hawakuwa tayari kuyasikiliza maneno ya haki walimuua shahidi Habib Najjar, wakidhani kwamba kwa kufanya hivyo watapumua na kuepukana na nasaha na mawaidha yake. Lakini Allah SW aliamuru muumini huyo aingizwe kwenye Pepo ya barzakhi inayoendelea mpaka Siku ya Kiyama. Waja wema wa Allah waliokufa shahidi huwa wanawekwa kwenye Pepo hiyo hadi siku hiyo ya hesabu na malipo. Kuhusu kuwa hai mashahidi, katika aya ya 169 ya Suratu Aal Imran, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: "Wala kabisa usiwadhanie walio uliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni maiti. Bali hao ni wahai, wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi." Muumini huyo alikuwa mtu mwenye kuwatakia heri watu wa kaumu yake kiasi kwamba aliwasikitikia hata wao waliomuua, akatamani laiti na wao pia wangeongoka na kuifuata njia ya heri na saada. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba inalazimu kusimama imara hata kama ni kwa gharama ya kujitoa mhanga na kuuawa shahidi katika njia ya Allah kwa ajili ya kuihami dini na viongozi wa dini. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, waja halisi wa Allah ni wenye kuwatakia heri watu. Licha ya tabu wanazopata na maudhi wanayofanyiwa na watu wao, huwa wanatamani watu hao wafanikiwe na kupata saada badala ya adhabu. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, wanaokufa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu huwa wanaishi maisha maalumu katika ulimwengu wa barzakhi mpaka Siku ya Kiyama. Mashahidi hao wananeemeshwa kwa neema na riziki maalumu za Mola katika Pepo ya barzakhi. Wasikilizaji wapenzi, darsa ya 792 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azijaze subira nyoyo zetu, azifanye thabiti imani zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags