Ijuumaa tarehe 21 Disemba 2018
Leo ni Ijumaa tarehe 13 Rabiuthani 1440 Hijria sawa na 21 Disemba 2018.
Leo tarehe 30 Azar mwaka wa Hijria Shamsia ni siku ya usiku mrefu zaidi wa mwaka ambao hapa nchini Iran unaitwa Usiku wa Yalda. Usiku huo wa Yalda au Usiku wa Chelleh ndio usiku mrefu zaidi wa mwaka katika nusu ya kaskazini mwa dunia. Usiku huo huwa baina ya kipindi cha kuzama jua tarehe 30 mwezi wa Azar ambayo ni siku ya mwisho ya kipindi cha mapukutiko (Fall) hadi kuchomoza jua katika siku ya kwanza ya mwezi Dei ambayo huwa siku ya kwanza ya kipindi cha baridi kali (Winter). Wairani na mataifa mengine mengi hufanya sherehe maalumu katika usiku huu wa Yalda. Usiku huo katika nusu ya kaskazini mwa dunia husadifiana na mabadiliko ya kimaumbile na tangu wakati huo mchana huanza kuwa mrefu zaidi kuliko usiku.

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, watu 270 walipoteza maisha yao baada ya ndege ya abiria ya Marekani kuripuka katika anga ya Lockerbie huko Scotland. Marekani na Uingereza ziliwatuhumu raia wawili wa Libya kuwa ndio waliotega bomu katika ndege hiyo. Kufuatia mashinikizo ya nchi mbili hizo, mwaka 1992, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliiwekea vikwazo vya mafuta, anga na kijeshi nchi ya Libya, kwa tuhuma za kuwaficha Walibya hao. Hata hivyo kufuatia makubaliano kati ya Washington na serikali ya Tripoli, mwaka 1999 watuhumiwa hao walikabidhiwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai yenye makao yake makuu mjini The Hague, Uholanzi ambapo baada ya kesi hiyo mmoja kati ya watuhumiwa hao aliachiliwa huru baada ya kutopatikana na hatia, na wa pili alihukumiwa kifungo cha maisha jela.
Katika siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) iliasisiwa. PLO iliundwa kutokana na makundi manane ya mapambano, taasisi za kielimu, kijamii, kitiba na kiutamaduni. Mwaka mmoja baadaye tawi la kijeshi la Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) la Fat-h lilianza harakati zake. Mwaka 1974, PLO ilikubaliwa kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Mataifa, na hadi mwaka 1982, harakati hiyo ilikuwa na uhusiano rasmi na nchi zaidi ya 100 duniani.
Katika siku kama ya leo miaka 194 iliyopita alifariki dunia tabibu na mtaalamu wa masuala ya ardhi wa Uingereza, James Parkinson. Alijifunza tiba kwa baba yake na alikuwa wa kwanza kueleza kwamba ugonjwa wa appendix unaweza kusababisha kifo. Parkinson aligundua ugonjwa wa Parkinson na namna unavyotokea. Kwa sababu hiyo ugonjwa huo ulipewa jina la tabibu huyo. Dalili za ugonjwa huo ni kama vile kutetemeka sana na kwa muda mrefu kwa ulimi, kichwa na mikono na kushindwa kuvuta miguu wakati wa kutembea hususan katika kipindi cha uzeeni na pia kukakamaa misuli katika sehemu yoyote ya mwili. Ugonjwa wa Parkinson unasababishwa na baadhi ya matatizo katika ubongo na hadi kufikia sasa hakuna dawa mujarabu iliyopatikana kwa ajili ya kutibu maradhi hayo.
Siku kama ya leo miaka 1221 iliyopita yaani tarehe 13 Rabiuthani mwaka 218 Hijria aliaga dunia Ibn Hisham msomi na mwanazuoni mkubwa wa Kiarabu. Ibn Hisham alizaliwa Basra nchini Iraq na alibobea katika elimu ya fasihi na utungaji mashairi. Alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufanya uchunguzi kuhusu maisha ya Nabii Muhammad (saw). Umashuhuri mkubwa wa Ibn Hisham unatokana na kitabu chake cha al Sira al Nabawiyya ambacho ni miongoni mwa marejeo muhimu kuhusu maisha ya Mtume Muhammad (saw).