Jumamosi, Disemba 22, 2018
Leo ni Jumamosi tarehe 14 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1440 Hijria sawa na tarehe 22 Disemba 2018 Miladia
Siku kama ya leo miaka 2164 iliyopita, duru ya tatu na ya mwisho ya vita vya kihistoria na vya umwagaji damu kati ya tawala za kifalme za Carthage na Roma ilimalizika kwa kupata ushindi Waroma na kuanguka utawala wa Wacartharge. Vita vya falme hizo mbili vilijulikana kwa jina mashuhuri la vita vya Punic. Utawala wa kifalme wa Carthage ulikuwa moja kati ya tamaduni kongwe huko kaskazini magharibi mwa Afrika na katika pwani ya bahari ya Mediterrania. ***
Katika skiku kama ya leo miaka 1374 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Mukhtar bin Abi Ubaida al-Thaqafi alianza mapambano ya kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Mwaka 61 Hijria Imam Hussein (as) akiwa pamoja na wafuasi na watu wa familia yake, aliuawa shahidi na jeshi la Yazid akiwa katika harakati za kuilinda dini tukufu ya Uislamu. Mukhtar alianzisha harakati zake za mapambano katika mji wa Kufa. Kabla yake, kulijitokeza kundi la 'Tawwabiin' ambalo lilipigana na utawala wa Bani Umayyah kwa lengo la kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein AS. Mukhtar Thaqafi alitawala Kufa kwa kipindi cha karibu mwaka mmoja na mwishowe alishindwa na jeshi la Mus'ab bin Zubair na kuuawa shahidi.***

Miaka 325 iliyopita katika siku kama ya leo, ulitokea mtetemeko mkubwa wa ardhi katika kisiwa cha Sicily kusini mwa Italia. Kufuatia zilzala hiyo, miji mitatu mikubwa ya kisiwa hicho iliteketezwa na kusababisha hasara kubwa kwa miji mingine yakiwemo makao makuu ya kisiwa hicho yaani Palermo. Mtetemeko huo wa ardhi unahesabiwa kuwa mkubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Italia. Zaidi ya watu 80,000 walipoteza maisha yao katika janga hilo la kimaumbile. ***
Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, Ufaransa na Uingereza zilihitimisha udhibiti wao wa siku 50 dhidi ya bandari ya Port Said nchini Misri na kutoa majeshi yao katika bandari hiyo. Inafaa kuashiria hapa kwamba, baada ya utawala haramu wa Israel kufanya mashambulio katika jangwa la Sinai, mashambulio ya pamoja ya anga ya Uingereza na Ufaransa dhidi ya Misri nayo yalianza. Mashambulio hayo, yalipelekea kutokea hasara kubwa dhidi ya Kanali ya Suez. Sababu ya kufanywa mashambulio hayo ambayo baadaye yalikuja kujulikana kwa jina la Vita vya Kanali ya Suel, ni hatua ya Rais Gamal Abdul-Nassir wa Misri kuitangaza kanali hiyo kuwa mali ya taifa. Umoja wa Mataifa uliiunga mkono Misri wakati wa mashambulio hayo na kwa utaratibu huo tawala tatu hizo, yaani Uingereza, Ufaransa na utawala wa Kizayuni wa Israel zikaondoa majeshi yao katika ardhi ya nchi hiyo. ***