Dec 29, 2018 23:48 UTC
  • Leo Katika Historia

Leo ni Jumapili tarehe 22 Mfunguo Saba, Rabiu Thani 1440 Hijria sawa na tarehe 30 Disemba mwaka 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1144 iliyopita, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Musa al-Mubarraqa mtoto wa Imam Muhammad Taqi al-Jawad na ndugu wa Imam Hadi as aliaga dunia katika mji mtakatifu wa Qum Iran. Alizaliwa mjini Madina mwaka 214 Hijria na mpaka anafikisha umri wa miaka 6 ambapo baba yake aliuawa shahidi, alikuwa chini ya malezi na usimamizi wa baba yake huyo. Baadaye alijifunza elimu kutoka kwa kaka yake yaani Imam Hadi (as). Musa al-Mubarraqa kipindi fulani aliishi mjini Kufa katika Iraq ya leo na alipokuwa na umri wa miaka 42 alisafiri na kuelekea katika mji wa Qum Iran. Aliishi mjini Qum akijishughulisha na uenezaji Uislamu hadi alipofariki dunia katika siku kama ya leo. Musa al-Mubarraqa ana daraja ya juu ya kielimu na alikuwa mpokezi wa hadithi. Aidha alisifika mno kwa taqwa na uchaji Mungu.

Katika siku kama ya leo miaka 178 iliyopita, alizaliwa mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Sheikh Muhammad Taqi Razi katika mji wa Isfahan nchini Iran. Sheikh Taqi Razi maarufu kwa jila la Agha Najafi, alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kwa ajili ya elimu ya juu ya kidini baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri kama Mirza Muhammad Hassan Shirazi na Sheikh Mahdi Kashiful Ghitaa. Baada ya kurejea Isfahan, Sheikh Agha Najafi alikuwa marejeo ya Waislamu katika masuala ya kidini na kisheria. Alikuwa mstari wa mbele kupambana na wakoloni kupitia harakati iliyopewa jina la Harakati ya Tumbaku. Vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni pamoja na "Anwarul Arifin", "Asrarul Ayat" na "Al-Ijtihad Wattaqlid".

Sheikh Muhammad Taqi Razi (Agha Najafi)

Miaka 71 iliyopita katika siku kama ya leo, magaidi wa mashirika mawili ya kijasusi ya Israel walishambulia kitongoji cha Balad al-Sheikh huko Palestina na kuchoma moto nyumba za kitongoji hicho. Moto huo uliwateketeza na kuwaua shahidi Wapalestina 60. Siku hiyo hiyo kundi jingine la kigaidi la Israel lililojulikana kwa jina la Irgun lilidondosha mabomu katikati ya kundi la Wapalestina na kuwaua shahidi 17 kati yao. Mashambulio hayo yaliyoshadidi mwishoni mwa mwaka 1947 na mwanzoni mwa 1948, yalikuwa na lengo la kuandaa mazingira ya kuwafukuza kwa nguvu Wapalestina katika ardhi zao ili kuasisisiwa utawala pandikizi na ghasibu wa Israel katika ardhi hizo.

Jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, uongozi wa kifalme wa Romania uling'olewa madarakani kufuatia kujiuzulu mfalme wa nchi hiyo na badala yake kukaundwa mfumo wa jamhuri nchini humo.  Hadi kufikia mwaka 1862, Romania ilijiamualia utawala wa ndani chini ya utawala wa Othmania na kujipatia uhuru wake taratibu hadi kufikia mwaka 1877. Romania ni moja ya nchi masikini za Ulaya ya Mashariki huku siasa za Kikomonisti zinazotawala, zikishindwa kumaliza matatizo ya nchi hiyo. 

Romania

Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, baada ya serikali ya kijeshi chini ya uongozi wa Jenerali Azhari hapa nchini Iran kushindwa kukandamiza vuguvugu la mapinduzi la wananchi Waislamu, Muhammad Reza Shah mfalme wa mwisho wa Iran, alimteuwa Shapour Bakhtiar kuwa Waziri Mkuu. Reza Shah na Marekani walikuwa na matumaini kwamba, Bakhtiar kwa kutumia nara na kaulimbiu zenye mielekeo ya utaifa na siasa ambazo kidhahiri zilikuwa zikionekana kama za kutaka mabadiliko, angeweza kuzuia harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Iran. Hata hivyo, wananchi wanamapinduzi wa Iran walitambua hila na hadaa hiyo, hivyo walimpinga vikali Bakhtiar na kumuita kuwa kibaraka wa mabeberu. Imam Khomeini (MA) alitoa taarifa na kutangaza kuwa, serikali ya Bakhtiar haikuwa halali na kuwataka wananchi wapambane na serikali hiyo. 

Shapour Bakhtiar

Miaka 12 iliyo[pita katika siku kama ya leo, Saddam Hussein mtawala katili na dikteta wa zamani wa Iraqalinyongwa baada ya kutolewa hukumu ya kifo dhidi yake. Saddam alizaliwa mwaka 1937 karibu na mji wa Tikrit uliopo umbali wa kilomita 140 kaskazini mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad na kujiunga na chama cha Baath akiwa na umri wa miaka 20. Dikteta huyo alifanikiwa kuwa naibu wa Ahmad Hassan al Bakr kufuatia mapinduzi yaliyojiri ndani ya chama hicho cha Baath mnamo mwaka 1968. Mwaka 1979 Saddam alikuwa Rais wa Iraq na muda mfupi baada ya kushika madaraka alianzisha vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akisaidiwa na madola ya Magharibi na kufanya mauaji na maafa mengi. Kwa msaada wa madola hayo, Saddam alipata silaha za kemikali na kuzitumia dhidi ya mataifa ya Iran na Iraq. Saddam aliendelea kufanya mauaji ya kila aina dhidi ya wananchi wa nchi hiyo na nchi jirani, chini ya himaya na uungaji mkono wa madola ya Magaharibi ikiwemo Marekani.

Kutiwa mbaroni Saddam Hussein

Tarehe 9 Dei mwaka 1388 Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe 30 Desemba, yaani miaka 9 iliyopita, mamilioni ya wananchi wa Tehran na miji mingine hapa nchini walifanya maandamano kulalamikia machafuko ya barabarani na himaya ya madola ya Magharibi kwa machafuko hayo. Baada ya uchaguzi wa Rais wa Juni 30, wagombea wawili walioshindwa walilalamikia matokeo ya uchaguzi, lakini hawakuwa tayari kufuatilia malalamiko yao kupitia njia za kisheria. Uungaji mkono wa madola ya Magharibi kwa wagombea hao ulipelekea kutokea machafuko mjini Tehran. Licha ya kuwa machafuko na vurugu za mitaani hazikuwa kubwa lakini ziliathiri amani na utulivu wa wananchi na kuibua tamaa ya Wamagharibi ya kubadilisha Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu hapa nchini. Maandamano ya mamilioni ya wananchi wa Iran dhidi ya wafanya vujo waliokuwa wakilalamikia matokeo ya uchaguzi wa Rais yalithibitisha kwamba, kinyume na propaganda za maadui, akthari ya wananchi walikuwa wakiyatambua na kuyakubali matokeo ya uchaguzi huo. Kwa hakika siku ya tarehe 9 Dei (30 Disemba 2009) ilikuwa siku ya kudhihirika uadui na uhasama wa wazi na wa nyuma ya pazia wa maadui wa ndani na nje ya nchi, mkabala wa utawala wa Kiislamu hapa nchini, ambapo maadui wa ndani na nje walilenga shabaha Uislamu, itikadi za kidini, maadili, uongozi wa Iran na mengine mengi ya thamani. Siku hii ya tarehe 9 Dei imepewa jina la "Siku ya Ung'amuzi na Muono wa Mbali".