Jan 01, 2019 02:27 UTC
  • Jumanne tarehe Mosi Januari 2019

Leo ni Jumanne tarehe 24 Rabiuthani mwaka 1440 Hijria sawa na tarehe Mosi Januari 2019.

Leo ni tarehe Mosi Januari inayosadifiana na kuanza mwaka mpya wa 2019 Miladia. Mpangilio wa miezi ya mwaka wa Kirumi unaoanza Januari hadi Disemba ulianza kutumiwa katika kipindi cha Mfalme Numa Pompilius yapata miaka 700 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa Masih (as). Kwa msingi huo tarehe 31 Disemba huwa siku ya mwisho ya mwaka wa Miladia na usiku wa kuamkia tarehe Mosi Januari huanza sherehe za kupokea mwaka mpya katika jamii za Wakristo na nchi nyingi za Afrika, America, Ulaya, Australia na hata Asia. Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran inakutakieni mwaka mpya wenye mafanikio. 

Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, sawa na tarehe Mosi Januari 1956, nchi ya Sudan ilipata uhuru kutoka kwa Misri na Uingereza. Mwaka 1899 Uingereza na Misri zilitiliana saini mkataba wa kuitawala kwa pamoja Sudan. Katikati mwa karne ya 20 lilianza vuguvugu la kutaka kujipatia uhuru nchini Sudan na mwaka 1956 Misri na Uingereza zikalazimika kuutambua uhuru wa nchi hiyo.

Bendera ya Sudan

Tarehe Mosi Januari mwaka 1959 mapinduzi ya Cuba yalipata ushindi na dikteta Fulgencio Batista akaikimbia nchi hiyo. Ushindi wa mapinduzi hayo yaliyoongozwa na Fidel Castro uliiweka Marekani katika mazingira magumu baada ya kushindwa vibaraka wake nchini Cuba.

Bendera ya Cuba

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, inayosadifiana na tarehe Mosi Januari 1993, yalianza kutekelezwa makubaliano ya Maastricht, eneo lililoko kusini mwa Uholanzi yaliyokuwa na lengo la kuondoa mipaka ya kiuchumi kati ya nchi 12 za Ulaya. Mkataba wa muungano wa Ulaya ulitiwa saini tarehe 10 Disemba mwaka 1991 na viongozi wa nchi 12 wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya katika mji mashuhuri wa Maastricht. Baadaye Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya ilibadilishwa na kuwa Umoja wa Ulaya. Utekelezwaji wa makubaliano ya Maastricht ulikuwa hatua kubwa katika mchakato wa kuungana zaidi wanachama wa Umoja wa Ulaya japo kuwa umoja huo ulikabiliwa na matatizo mengi katika miaka iliyofuatia.

Katika siku kama ya leo miaka 125 iliyopita, Heinrich Rudolf Hertz mwanafizikia  na mwanahisabati wa Ujerumani aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 37. Alizaliwa mjini Hamburg Ujerumani mwaka 1857. Alikuwa na mapenzi makubwa na fizikia na umakenika tangu akiwa kijana mdogo. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana akajiendeleza kimasomo katika uwanja huo.

Heinrich Rudolf Hertz