Jan 02, 2019 23:39 UTC
  • Alkhamisi tarehe 3 Januari 2019

Leo ni Alkhamisi tarehe 26 Rabiuthani 1440 Hijria sawa na Januari 3, mwaka 2019.

Katika siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, inayosadifiana na Januari 3, 1993 kulitiwa saini makubaliano ya Start-2 kati ya Marais wa zamani wa Russia na Marekani, Boris Yeltsin na Bill Clinton. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi hizo mbili zinapaswa kupunguza theluthi mbili za silaha zao za nyuklia. Makubaliano ya Start-1 yenye lengo hilohilo yalitiwa saini mwaka 1987 kati ya Marais Mikhael Gorbachev wa Russia na Ronald Reagan wa Marekani. Hata hivyo badala ya kuanza kuharibu silaha zake za nyuklia, Marekani ilijilimbikizia sialaha zaidi za aina hiyo suala ambalo liliilazimisha pia Russia kusitisha mpango wa kuanza kuharibu silaha zake za atomiki.

Makombora ya nyuklia

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 13 Dei 1367 Hijria Shamsia, ujumbe wa Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliwasilishwa kwa Mikhail Gorbachev kiongozi wa mwisho wa Umoja wa Kisovieti akimlingania dini ya Kiislamu na kumtaka aachane na fikra za Kimaksi. Katika sehemu moja ya ujumbe huo Imam Khomeini alisema: "Tatizo kuu la nchi yako si suala la umiliki, uchumi wala uhuru, bali ni kutokuwa na imani ya kweli juu ya Mwenyezi Mungu; na tatizo hilo ndilo lililoitumbukiza au litakaloitumbukiza Magharibi katika mporomoko wa kimaadili na kuifanya igonge ukuta. Tatizo lenu kubwa ni kupigana vita visivyokuwa na faida dhidi ya Mwenyezi Mungu." Mwishoni mwa ujumbe huo Imam Khomeini alisema: "Tokea sasa Ukomonisti unapaswa kutafutwa kwenye majumba ya makumbusho ya kisiasa duniani; kwani hauwezi kukidhi mahitaji halisi ya mwanadamu." Imam Khomeini alimuusia Gorbachev akisema: "Nakutaka ufanye uchunguzi wa kina kuhusu Uislamu, sio kwa sababu Uislamu na Waislamu wanakuhitajia wewe, hapana, bali kutokana na thamani za hali ya juu na za ulimwengu mzima za dini hiyo ambayo inaweza kuwa wenzo wa ufanisi na uokovu wa mataifa mbalimbali na kukidhi matatizo makubwa ya mwanadamu."

Mikhail Gorbachev

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita inayosadifiana na 13 Dey 1358 Hijria Shamsia, kulifanyika kongamano la kwanza la harakati za kupigania uhuru duniani mjini Tehran na kuhudhuriwa na wawakilishi wa harakati hizo. Lengo kuu la kuitishwa kongamano hilo, lilikuwa kuitambulisha harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu kwa walimwengu, sambamba na kuandaa mazingira ya kujenga umoja na mshikamano wa harakati hizo katika kukabiliana na dhuluma na mabeberu duniani.

Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo kulifanyika mkutano wa Guadeloupe kati ya viongozi wa serikali za Marekani, Uingereza, Ujerumani ya Magharibi na Ufaransa kwa ajili ya kuchunguza masuala kadhaa muhimu ya kimataifa hususan Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Mkutano huo ulifanyika katika kisiwa cha Guadeloupe kilichoko magharibi mwa Bahari ya Atlantic ambacho ni koloni la Ufaransa. Katika mkutano huo uliofanyika siku 40 kabla ya ushindi kamili wa harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Iran washiriki wote walikiri kwamba, Mfalme wa wakati huo wa Iran Shah Pahlavi ataondolewa madarakani isipokuwa Jimmy Carter rais wa wakati huo wa Marekani ndiye pekee aliyekuwa na matumaini ya kubakia madarakani utawala wa Shah kwa msaada wa jeshi. Hata hivyo mkutano huo wa Guadeloupe haukuwa na mbinu ya kukabiliana na Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi wa Iran na uliishia kukiri nguvu kubwa ya mapinduzi hayo na mustakbali wake mwema.

Mkutano wa Guadeloupe

Siku kama ya leo miaka 975 iliyopita, alizaliwa mjini Marv, moja ya miji ya Khurasan ya zamani ya Turkmenistan ya sasa, Ainuz-Zaman Qatwan Marvazi, mtaalamu wa hesabati, tabibu na mwanafalsafa wa Kiislamu. Qatwan Marvazi alikuwa na umahiri mkubwa katika elimu za hesabati, falsafa, fasihi na elimu ya dini ya Kiislamu. Hata hivyo binafsi alipendelea sana elimu ya tiba. Marvazi ambaye alikuwa akijishughulisha na kutoa huduma ya tiba katika mji wa Marv aliandika vitabu kadhaa na moja ya vitabu hivyo ni 'Kiihaan Shenokht' ambacho kinahusu elimu ya hesabati. Ainuz-Zaman Qatwan Marvazi alifariki dunia mwaka 548 Hijiria.

Siku kama ya leo miaka 922 iliyopita alifariki dunia Hassan al-Sabbah mwasisi wa utawala wa Ismailiyah nchini Iran. Sabbah alizaliwa mwaka 445 Hijiria mjini Qum na akiwa mtoto pamoja na familia yake alielekea mjini Ray, kusini mwa mji wa Tehran. Akiwa mjini hapo alijifunza masomo ya dini ya Kiislamu na Ushia. Hata hivyo akiwa kijana alijiunga na madhehebu ya Ismailiyah. Wafuasi wa kundi hilo kinyume na Mashia wengine baada ya Imam Swadiq (as) walikataa kumtambua mtoto wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) yaani al-Imam al-Kadhim (as) kuwa Imam na badala yake wakamtambua mtoto mwingine wa Imam Swadiq, yaani Ismail kuwa ndiye Imam. Baada ya Hassan al-Sabbah kujiunga na kundi hilo alielekea nchini Misri kwa lengo la kujifunza mafundisho zaidi ya Ismailiyah. Wakati huo viongozi wa Ismailiyah walikuwa makhalifa wa utawala wa Fatimiyah nchini Misri. Mwaka 473 Hassan al-Sabbah alirejea Iran na kuanza kueneza mafundisho ya kundi hilo katika maeneo tofauti ya Iran. Mwaka 483 alidhibiti ngome imara ya Alamūt karibu na mji wa Qazvin na ukawa mwanzo wa harakati ya mapambano dhidi ya utawala wa Seljuk uliokuwa ukitawala Iran. Utawala wa Ismailiya chini ya uongozi wa Hassan al-Sabbah ulidhibiti pia ngome tofauti za kaskazini mashariki, kusini na hata katikati ya Iran sambamba na kuua viongozi wengi wa utawala wa Seljuk. 

Hassan al-Sabbah