Jan 04, 2019 23:09 UTC
  • Jumamosi, Januari 5, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 28 Mfunguo Saba, Rabiu Thani 1440 Hijria mwafaka na tarehe 5 Januari 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 328 iliyopita,  inayosadifiana na tarehe 5 Januari 1691, ilichapishwa na kusambazwa noti ya kwanza huko Ulaya. Noti hiyo ilichapishwa na Benki ya Stockholm na kutumiwa kama fedha. Kabla ya kuchapishwa noti hiyo nchini Sweden, miamala ya kibiashara ilikuwa ikifanyika kwa kutumia sarafu za dhahabu zenye pembe nne. Moja kati ya noti za awali kabisa kuchapishwa nchini Sweden, inahifadhiwa kwenye jumba la makumbusho la Benki ya Stockholm.***

Noti ya kwanza iliyochapishwa Ulaya

Miaka 210 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitiwa saini mkataba wa Dardanelles (Treaty of the Dardanelles) baina ya utawala wa Othmania na Uingereza. Kwa mujibu wa mkataba huo, Uingereza iliahidi kuondoka katika ardhi zote zilizokuwa chini ya utawala wa Othmania ikiwemo Misri na kuhitimisha ukaliaji mabavu wa ardhi hizo. Mkabala wake, utawala wa Othmania uliahidi kutambua rasmi haki za kibalozi za Uingereza katika ardhi za utawala wa Othmania. ***

Muonekano wa Lango Bahari la Dardanelles 

Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Iran waligoma kwenda madarasani na kukataa kusoma wakionesha upinzani wao dhidi ya safari ya rais wa wakati huo wa Marekani, Jimmy Carter hapa nchini na uungaji mkono wake kwa utawala wa Shah. Wakati huo Carter alikuwa akidai kuwa ni mtetezi wa haki za binadamu na mpinzani wa suala la kuziuzia silaha tawala za kidikteta. Hata hivyo serikali ya Washington ilichukua uamuzi wa kufunga mikataba ya kuuzia silaha nzito utawala wa kidikteta wa Shah na kupuuza ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliokuwa ukifanywa nchini Iran. Jimmy Cater alifikia kiwango cha kumwita Shah kuwa ni kiongozi anayependwa na wananchi na kwamba, Iran ni kisiwa cha amani. Hata hivyo muda mfupi baadaye wananchi walianza harakati za kudai uhuru na kujitawala na miezi 13 baada ya safari ya Carter mjini Tehran, Shah aliondolewa madarakani na ikaanzishwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. ***

Jimmy Carter akiwa na mfalme Shah

Miaka 34 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 5 Januari 1985, utawala wa Kizayuni wa Israel uliwachukua maelfu ya Mayahudi wa Ethiopia "Mafalasha' kupitia ardhi ya Sudan. Mafalasha hao ambao idadi yao ilikuwa watu 8,000 walipelekwa huko Israel. Nchi za Kiarabu ziliikasirikia Sudan kwa kushirikiana na Israel katika kuwahamisha Mayahudi wa Kiethiopia na kuwapeleka Israel. ***

Na miaka 4 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Eusébio da Silva Ferreira, nyota wa mpira wa miguu nchini Ureno. Alizaliwa Januari 25 mwaka 1942, huko Maputo Msumbiji. Alionyesha hamu na kipaji cha hali ya juu ya kusakata kabumbu akiwa shuleni. Alikuwa nyota katika timu ya taifa ya soka ya Ureno katika zama zake. Alifunga jumla ya magoli 733 katika mechi za kimataifa 745 alizocheza na anahesabiwa kuwa, mmoja wa wafungaji bora duniani katika ulimwengu wa soka. Mwaka 1956 Eusébio da Silva Ferreira alishinda tuzo ya mchezaji bora barani Ulaya. Aidha katika miaka ya 1970 na 1973 alitunukiwa tuzo ya mchezaji bora wa soka nchini Ureno. Baada ya kuugua moyo kwa muda na kulazwa mara kadhaa hospitali hatimaye Eusébio da Silva Ferreira aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 71. ***

Eusébio da Silva Ferreira,