Jan 05, 2019 23:05 UTC
  • Jumapili, 6 Januari, 2019

Leo ni Jumapili tarehe 29 Mfunguo Saba, Rabiu Thani 1440 Hijria mwafaka na tarehe 6 Januari 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 767 kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa Muhammad bin Ahmad Dhihni mwenye lakabu ya Shamsuddin mtaalamu wa elimu ya hadithi na mwanahistoria mashuhuri. Alikuwa na mapenzi makubwa ya kukusanya hadithi. Shamsuddin akiwa na lengo la kujikamisha zaidi katika elimu hiyo alifanya safari katika maeneo mbalimbali na kupata fursa ya kusikia hadithi kutoka kwa wanazuoni mbalimbali. Muhammad bin Ahmad Dhihni hakuwa nyuma pia katika utunzi wa vitabu. Al-Kashif, Tabaqat al-Quraa, al-Muujam al-Saqhir na al-Muujam al-Kabir ni baadhi tu ya vitabu vyake mashuhuri.***

Muhammad bin Ahmad Dhihni

Miaka 158 iliyopita, yaani sawa na tarehe 6 Januari mwaka 1861 kuliasisiwa nchi ya Romania. Mpango wa kupatikana nchi hii msingi wake ulikuwa kutiwa saini kwa muungano wa miji miwili midogo iliyojulikana kwa jina la Moldavia na Wallachia, makubaliano yaliyofikiwa tarehe 13 Disemba mwaka 1859. Baada ya miaka miwili majimbo na miji mingine ya jirani vikajiunga na muungano huo. Kwa utaratibu huu ikapatikana nchi iliyokuja kutambulika kwa jina la Romania. ***

Romania

Katika siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, aliaga dunia Theodore Roosevelt Rais wa zamani wa Marekani. Theodore Roosevelt Rais wa 26 wa Marekani alizaliwa Oktoba 27 mwaka 1857. Alijiunga na harakati za kisiasa akiwa katika rika la ujana. Alikuwa mwanachama wa chama cha Republican. Alikuwa Makamu wa Rais na baada ya kuuawa William McKinley aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo, Theodore Roosevelt akawa Rais wa muda wa nchi hiyo. Mwaka 1901 alichaguliwa kuwa Rais wa Marekani. Mwanzoni mwa utawala wake, Theodore Roosevelt aliimarisha uwepo wa vikosi vya Marekani nchini Cuba iliyokuwa ikikaliwa kwa mabavu na Washington na akaitangaza rasmi nchi hiyo kuwa chini ya mamlaka na himaya ya Marekani. ***

 Theodore Roosevelt

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, alizaliwa Ali Isfandiyari mashuhuri kwa jina la Nima Yooshij, mwasisi wa mashairi ya kisasa nchini Iran. Isfandiyari alizaliwa katika mojawapo ya vijiji vya mkoa wa Mazandaran kwa jina la Yush huko kaskazini mwa Iran. Malenga huyo baadaye alielekea Tehran na kuanza kujifunza lugha ya Kifaransa. Nima Yooshij alianza kutunga mashairi na kubuni mfumo mpya wa mashairi. Miongoni mwa sifa za mfumo huo wa mashairi mapya ni kueleza masuala ya jamii kwa lugha nyepesi. Kazi muhimu zaidi ya malenga huyo mashuhuri wa Iran ni maarufu kwa jina la "Afsaneh". ***

Ali Isfandiyari mashuhuri kwa jina la Nima Yooshij,

Katika siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, Muhammad bin Abdullah bin Bahlul maarufu kwa jina la Sheibani aliaga dunia. Sheibani alikuwa mashuhuri katika elimu ya hadithi. Alimu huyo alikuwa na asili ya mji wa Kufa katika Iraq ya leo. Alifanya safari katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kwenda kusikiliza hadithi na ameandika vitabu katika nyanja mbalimbali. ***

Muhammad bin Abdullah bin Bahlul 

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, serikali ya kijeshi ya Gholam Reza Azhari ilianguka nchini Iran na nafasi yake ikachukuliwa na serikali ya Shapour Bakhtiar. Baada ya Shapour Bakhtiar kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa utawala wa Kipahlavi, katika siku kama ya leo alitangaza baraza lake na mawaziri na hivyo akawa amechukua rasmi hatamu za uongozi. Baraza la Mawaziri la Shapour Bakhtiar lilianza kazi katika hali ambayo, harakati ya Kiislamu ilikuwa imeshika kasi katika kila kona ya Iran na hakukuwa na nguvu yoyote ya kuweza kukabiliana na harakati hiyo ya wananchi. Shapour Bakhtiar akiwa Waziri Mkuu wa mwisho katika kipindi cha utawala wa Kifalme wa Kipahlavi hapa nchini alijaribu kuwapatia wananchi baadhi ya mambo na upendeleo ili kwa njia hiyo aweze kupunguza malalamiko ya wananchi. Hata hivyo, ujumbe wa Imam Khomeini kuhusiana na serikali ya Bakhtiar ulisambaratisha njama za utawala wa Kifalme zilizokuwa na lengo la kuvuruga harakati ya mapinduzi ya wananchi. Katika ujumbe wake huo, Imam Khomeini MA aliitaja serikali hiyo kwamba, si halali. ***

Gholam Reza Azhari 

Na miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitokea hamasa ya mashahidi wa Huweize iliyoongozwa na Shahidi Alamul Huda katika miezi ya mwanzoni mwa uvamizi wa Iraq dhidi ya ardhi ya Iran. Mwezi Dei mwaka 1359 Hijria Shamsia na baada ya jeshi la Iran ya Kiislamu kuvishinda vikosi zaidi ya viwili vya jeshi la Iraq huko kusini mwa eneo la Susangerd, kundi moja la Jeshi al Sepah la Ahwaz huko kusini mwa Iran lilitumwa katika mji wa Huweize kwenda kuulinda mji huo mbele ya mashambulizi ya Iraq. Hata hivyo kutokana na kuchelewa kufika zana na hujuma kubwa ya Iraq, jeshi la Iran lililazimika kurudi nyuma. Wakati huo zaidi ya wapiganaji mia moja wa Jeshi la Sepah, wapiganaji wa kujitolea na wanafunzi wa vyuo vikuu wafuasi waaminifu wa Imam Khomeini wakiongozwa na Sayyid Muhammad Hussein Alamul Huda walibakia katika mji huo wa Huweize wakipambana na adui na wakauawa shahidi. Baadaye jeshi la Iraq liliubomoa kabisa mji wa Huweize na kuusawazisha na ardhi. Pamoja na hayo ushujaa wa vijana hao shupavu wa Iran waliosabilia roho zao kulinda ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu umebakia hai katika historia ya Iran.***