Jumatatu tarehe, 7 Januari, 2019
Leo ni Jumatatu tarehe 30 Rabiuthani 1440 Hijria sawa na Januari 7 mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita na kwa amri ya mfalme wa wakati huo wa Iran, Reza Khan Pahlavi, wanawake wa Iran walipigwa marufuku kuvaa vazi la Hijabu. Amri ya mfalme huyo ilitolewa baada ya kutekelezwa pendekezo la mabadiliko ya nguo za wanaume ambapo lengo lilikuwa ni kufuta athari za Kiislamu na kufuata kibubusa Umagharibi. Baada ya kusafiri nchini Uturuki na kumfuata Mustafa Kemal Atatürk, rais wa wakati huo wa taifa hilo na ambaye alikuwa ameathiriwa sana na Umagharibi huku akiwa naye alishapiga marufuku mavazi ya Kiislamu, Reza Khan Pahlavi naye alitaka kutekelezwa hatua kama hiyo nchini Iran. Tangu wakati huo maafisa usalama wa mfalme huyo walikuwa wakiwadhalilisha wanawake waliokuwa wamejisitiri kwa vazi la hijabu. Mpango huo wa kikoloni ulipingwa vikali na maulama wa Kiislamu kwa kushirikiana na raia wa taifa hili.
Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, alifariki dunia Nikola Tesla mwanafizikia mzaliwa wa Yugoslavia. Nikola alizaliwa mwaka 1857 na alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza masomo ya fizikia wakati akiwa shuleni. Msomi huyo wa Kiyugoslavia alifanya tafiti na uvumbuzi wake mwingi katika uwanja wa nishati ya umeme na kupata mafanikio makubwa. Umeme mbadala au altenative electricity unahesabiwa kuwa miongoni mwa uvumbuzi wa Nikola Tesla. Mwanafikizia huyo alikipa jina lake la Tesla, kifaa kinachotumika kupimia kiwango na mtiririko wa sumaku yaani (magnetic flux).
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita dikteta wa Cambodia Pol Pot alikimbia nchi kufuatia mashambulizi ya jeshi la Vietnam dhidi ya nchi hiyo. Kiongozi huyo wa kundi la Khmer Rouge alikuwa muungaji mkono mkubwa wa fikra za Kimao na serikali ya China. Sifa kuu ya serikali ya Pol Pot ilikuwa kutumia mabavu dhidi ya raia, kuwahamishia kwa nguvu vijijini na kufuta kabisa athari zote za utamaduni na ustaarabu. Pol Pot na kundi lake la Khmer Rouge waliua watu wanaokadiriwa kuwa milioni moja na nusu hususan raia wenye asili ya Vietnam katika kipindi cha chini ya miaka mitatu ya utawala wake huko Cambodia. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana jeshi la Vietnam likachukua hatua za kuiondoa madarakani serikali ya Pol Pot.
Siku kama hii ya leo miaka 33 iliyopita Suleiman Khatir aliyekuwa miongoni mwa polisi wa mpakani wa Misri katika jangwa la Sinai alikufa shahidi akiwa jela. Suleiman Khatir mwezi Oktoba mwaka 1985 aliwaangamiza Wazayuni wengi katika kulalamikia hatua ya serikali ya Misri ya kusaini hati ya mapatano ya Camp David kati yake na utawala wa Kizayuni. Serikali ya Misri ilimtia mbaroni polisi huyo na kuamuru ahukumiwe kifungo cha maisha jela.
Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa masuala ya Kiislamu na mtarjumi wa Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Kijapani, Toshihiko Izutsu. Alizaliwa tarehe 4 Mei 1914 katika mji wa Tokyo na mwaka 1960 alipata shahada ya uzamivu katika taaluma ya lugha na kuanza kufunza lugha na falsafa. Toshihiko Izutsu alitunukiwa nishani ya juu kabisa ya elimu kutoka kwa mfalme wa Japan na ameandika vitabu vingi. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni "Historia ya Fikra za Kiislamu", tarjumu ya kitabu cha "al Mashair" cha Mulla Sadra na vilevile tarjumu ya kitabu cha "Fihi Maa Fiih" cha Maulawi kwa lugha ya Kijapan.