Jumamosi, 12 Januari, 2019
Leo ni Jumamosi tarehe 5 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1440 Hijria mwafaka na tarehe 12 Januria 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1435 iliyopita, yaani tarehe 5 Mfunguo Nane Jamadil Awwal mwaka wa 5 Hijria, alizaliwa Bibi Zainab (as) binti mtukufu wa Imam Ali bin Abi Twalib na Bibi Fatimatu Zahraa (as). Bibi Zainab alikuwa mashuhuri miongoni mwa watu kutokana na maarifa na elimu kubwa aliyokuwa nayo. Katika tukio la Karbala, Bibi Zainab (s.a) alisimama kidete na kukabiliana na dhulma za watawala dhalimu na ujahili watu wa zama hizo ili kutimiza malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein (a.s). Bibi Zainab alipelekwa Sham pamoja na mateka wengine wa Nyumba Tukufu ya Mtume (saw) baada ya mapambano ya Imam Hussein (a.s) huko Karbala. Hotuba za Bibi Zainab mbele ya majlisi ya Ibn Ziyad mtawala wa Kufa na katika ikulu ya Yazid bin Muawiya huko Sham zilikuwa na taathira kubwa katika kufichua dhulma na ukandamizaji wa Bani Umayya na kuonesha jinsi familia ya Mtume ilivyodhulumiwa. Nchini Iran siku ya kuzaliwa Bibi Zainab (a.s) husherehekewa kama 'Siku ya Wauguzi'. ***

Katika siku kkama ya leo miaka 1432 iliyopita, kulijiri vita vya Mu'utah, baina ya jeshi la Waislamu na jeshi la Roma na waitifaki wake. Vita hivyo vilitokea baada ya mjumbe aliyekuwa ametumwa na Mtume (saw) huko Sham kwa ajili ya kulingania dini ya Kiislamu, kuuawa shahidi na askari wa kulinda mpaka wa eneo hilo. Baadhi ya wanahistoria wanasema kuwa, miongoni mwa sababu zilizomfanya Mtume (saw) kutuma jeshi la wapiganaji 3,000 kukabiliana na utawala wa Roma katika eneo hilo ni kuuawa shahidi walimu 14 wa Qur'an Tukufu waliokuwa wametumwa na Mtukufu Mtume katika maeneo ya mpakani ya Sham. Katika vita hivyo Mtume alimteua Jaafar bin Abi Twalib, mtoto wa ami yake, kwa ajili ya kuongoza jeshi la Kiislamu, na akawateua Zaid bin Haritha na Abdullah bin Rawaaha kwa ajili ya kukaimu nafasi hiyo. Jeshi la Kiislamu ambalo lilikuwa limechoka kutokana na kwamba ilikuwa mara ya kwanza kwenda safari ndefu kama hiyo, lilipambana na jeshi la Roma na wapiganaji wa kikabila katika eneo la Mu'utah, magharibi mwa Jordan ya leo ambapo liliwapoteza viongozi wote watatu wa jeshi hilo la Kiislamu. Hatimaye Waislamu walimpa jukumu la kuongoza jeshi hilo Khalid Bin Walid ambaye ndiye kwanza alikuwa amesilimu, ambapo naye alitoa amri ya kuwataka Waislamu kurudi nyuma. Hata kama jeshi la Kiislamu halikushinda vita hivyo, lakini liliweza kusoma mbinu za jeshi la adui hatua ambayo ilikuwa utangulizi wa ushindi dhidi ya jeshi hilo la adui katika vita vya baadaye. ***
Miaka 458 iliyopita katika siku kama ya leo, kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia, Muhammad Mustafa Imadi, maarufu kwa jina la 'Abus-Suud', faqihi na mfasiri wa Qur'an Tukufu. Abus-Suud alizaliwa karibu na mji wa Istanbul, magharibi mwa Uturuki na kuanza kujifunza masomo ya dini ya Kiislamu ambapo alipanda daraja na kuanza kufundisha. Mbali na msomi huyo wa Kiislamu kufahamu lugha ya Kituruki, alikuwa hodari pia katika lugha ya Kifarsi na Kiarabu ambapo aliweza hata kusoma mashairi kwa lugha hizo. Miongoni mwa athari za Abus-Suud ni pamoja na 'Tafsir Abis-Suud' 'Dua Nameh' 'Qanun Nameh' na 'Mafruudhaat.' ***
Siku kama ya leo miaka 354 iliyopita, aliaga dunia Pierre de Fermat mwanahisabati wa Kifaransa na mwasisi wa nadharia ya leo ya namba yaani Modern Theory of Numbers na ile ya uwelekeo inayojulikana kama Theory of Probability. Pierre de Fermat alizaliwa mwaka 1601 Miladia na alianza kujifunza hesabu tangu akiwa mtoto. Mwanahisabati huyo wa Kifaransa aligundua pia kanuni msingi ya jiometri changanuzi, yaani Analytic Geometry. ***
Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo, Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran aliagiza kuundwa Baraza la Mapinduzi katika kipindi hicho muhimu cha harakati za Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Imam aliagiza baraza hilo liundwe wakati Marekani ilipokuwa ikifanya njama za kuulinda utawala wa kifalme wa Pahlavi. Jukumu kubwa la baraza hilo lilikuwa ni kuratibu mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah, kupeleka mbele malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na pia kuandaa uwanja mzuri wa kuundwa serikali ya muda nchini Iran. ***

Katika siku kama ya leo miaka 9 iliyopita, mhadhiri wa nyuklia wa Chuo Kikuu cha Tehran, Dokta Massoud Ali-Mohammadi aliuawa kigaidi. Massoud Ali-Mohammadi aliyekuwa na umri wa miaka 50 aliuawa kwa mlipuko wa bomu la kuongozwa kutoka mbali wakati alipokuwa akitoka nyumbani kwake Alipata shahada ya uzamivu ya taaluma ya fizikia katika Chuo Kikuu cha Sharif mjini Tehran mwaka 1371 na alikuwa miongoni mwa wanachuo wa kwanza wa Iran kupata shahada ya uzamivu ya somo la fizikia ndani ya Iran. Alitunukiwa tuzo ya Tamasha ya Kimataifa ya Kharazmi mwaka 1386 na kushika nafasi ya pili katika utafiti wa masuala ya kimsingi. Wapinzani wa miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran baada ya kushindwa kusimamisha miradi hiyo kwa hatua za kisiasa na vikwazo vya kiuchumi walikhitari kutumia njia za kigaidi na kuwaua wasomi wa nyuklia wa Iran. Magaidi waliomuua msomi huyo wa Iran walitiwa nguvuni na kukiri kwamba walikuwa wakishirikiana na utawala haramu wa Israel. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 8 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi wenye ukubwa wa 7 kwa kipimo cha Rishta ilitokea huko Haiti katika bahari ya Caribbean. Zilzala hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuwahi kutokea duniani katika miongo kadhaa iliyopita na iliua watu karibu laki tatu na kujeruhi wengine wengi. Mtetemeko huo wa ardhi ulioikumba Haiti uliharibu kabisa miundo mbinu na nyumba nyingi za nchi hiyo. Aidha ulipelekea mamia ya maelfu ya raia kuwa wakimbizi. ***