Jumatatu tarehe 14 Januari 2019
Leo ni Jumatatu tarehe 7 Jamadil Awwal 1440 Hijria sawa na Januri 14 mwaka 2019.
Tarehe 14 Januari miaka 8 iliopita, Rais Zainul Abidin Bin Ali wa Tunisia na dikteta wa nchi hiyo alikimbilia Saudi Arabia kufuatia vuguvugu la mapinduzi ya wananchi. Kukimbia nchi Zainul Abidin, kulihitimisha utawala wa kiimla uliodumu kwa nusu karne wa Habib Bourquiba pamoja na Zainul Abidin Bin Ali na wananchi wa Tunisia wakaonja ladha ya uhuru. Zainul Abidin aliingia madarakani mwaka 1987 kupitia mapinduzi ya kijeshi bila umwagaji damu na kumwondoa madarakani Habib Bourguiba aliyekuwa amejitangaza kuwa rais wa maisha wa nchi hiyo. Bin Ali aliiongoza Tunisia kwa mkono wa chuma kwa miaka 23 huku akiendeleza siasa za kutegemea Wamagharibi na kupiga vita Uislamu. Kujichoma moto kijana mmoja muuza mboga katika kulalamikia dhulma na ukatili wa maafisa usalama wa utawala wa nchi hiyo, kuliibua harakati ya wananchi wa Tunisia dhidi ya utawala wa kiufisadi wa Bin Ali na hatimaye kupelekea kupinduliwa dikteta huyo.
Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita maafisa wa shirika la ujasusi la Israel Mossad walitekeleza mauaji ya kigaidi dhidi ya Salah Khalaf maarufu kwa jila la Abu Iyad akiwa pamoja na maafisa wengine wawili wa ngazi za juu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) huko Tunisia. Salah Khalaf alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu na kiongozi nambari mbili wa Fat'h baad ya Yaser Arafat. Mauaji ya viongozi hao wa ngazi za juu wa PLO tena yaliyofanyika kwa kukiuka mamlaka ya kujitawala ya nchi nyingine yaani Tunisia, yalionyesha kwamba utawala haramu wa Israel hauheshimu sheria yoyote ile katika suala la kuwafuta wapinzani wake.
Miaka 54 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo Sayyid Qutb msomi na mwanamapambano wa Misri alinyongwa pamoja na wenzake wawili huko Cairo mji mkuu wa nchi hiyo. Msomi huyo alihifadhi Qur'ani tukufu katika ujana wake. Sayyid Qutb alifahamiana na Hassan al Bana na kujiunga na harakati ya Ikhwanul Muslimin ya nchi hiyo wakati alipokuwa akiendesha harakati za kisiasa. Sayyid Qutb alitiwa nguvuni na baadaye kunyongwa baada ya kuzuka hitilafu kati ya Gamal Abdel Nasser Rais wa wakati huo wa Misri na Ikhwanul Muslimin. Msomi huyo alikuwa akiiamini kwamba "kambi za Mashariki na Magharibi zinapigana na Waislamu na kwamba kambi mbili hizo zimeungana ili kupora maliasili za nchi za Kiislamu". Miongoni mwa vitabu vya msomi na mwanamapambano huyo wa Kiislamu ni kile alichokipa jina la" Uislamu na Amani ya Kimataifa".
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita ulianza mkutano wa kihistoria wa kimataifa wa Casablanca nchini Moroco. Mkutano huo ambao ulihudhuriwa na Rais wa wakati huo wa Marekani Franklin Roosevelt na Waziri Mkuu wa Uingereza Winston Churchill, wakiwa viongozi wa nchi muhimu za waitifaki, ulijadili mpango wa mashambulizi dhidi ya Sicily huko Italia, misaada ya nchi waitifaki kwa Russia na masuala mengine ya vita. Mwishoni mwa mkutano huo uliodumu kwa siku kumi, wawakilishi wa nchi zilizoshiriki walitoa taarifa ya pamoja wakiahidi kuendeleza vita hadi wakati wa kusalimu amri bila ya sharti nchi zilizoungana.
Siku kama ya leo miaka 144 iliyopita alizaliwa Albert Schweitzer katika mji wa Alsace-Lorraine huko Ufaransa. Schweitzer ambaye alikuwa daktari na mtaalamu wa muziki, alielekea barani Afrika baada ya kukamilisha elimu katika fani ya udaktari na kuasisi hospitali nchini Gabon. Hadi mwishoni mwa umri wake, Schweitzer alijitolea kuwasaidia na kutibu wananchi maskini wa Kiafrika. Tabibu huyo aliyekuwa na hisia za kibinadamu, ameandika vitabu kadhaa muhimu zaidi kikiwa ni kile alichokipa jina la "Falsafa ya Ustaarabu". Mwaka 1952 Schweitzer alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel kutokana na huduma zake kubwa kwa wagonjwa. Alifariki dunia mwaka 1965.
Siku kama ya leo miaka 1051 iliyopita, alifariki dunia Ibn Ghalabun al-Halabi, msomi wa Qur'ani na mtaalamu mashuhuri wa elimu ya hadithi wa enzi hizo. Ibn Ghalabun alizaliwa mjini Aleppo, Syria mnamo mwaka 309 Hijiria na kuishi nchini Misri. Alipata kusoma elimu ya hadithi na qiraa ya Qur'ani Tukufu kwa wasomi wengi wa zama zake na kutokea kuwa mwalimu katika uwanja huo. Vilevile ametoa maoni na nadharia zake kuhusiana na qiraa ya Qur'ani ambazo zimeandika katika kitabu cha 'Al-Kashf kilichoandikwa na mwanafunzi wake, Makki bin Abi Twalib.' Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni 'Al-Irshad' ambacho kinazungumzia qiraa saba za Qur'ani tukufu.
