Jumanne, tarehe 15, Januari 2019
Leo ni Jumanne tarehe 8 Jamadi Awwal 1440 Hijria sawa na 15 Januari 2019.
Tarehe 15 Januari miaka 18 iliyopita ensaiklopidia ya Wikipedia ilianza kazi katika ntandao wa intaneti. Lengo la kuanzishwa ensaiklopidia hiyo limetajwa kuwa ni kupanua maarifa na uelewa wa watu kupitia njia ya kushirikishwa watu wote katika mradi huo. Insaiklopidia hiyo kubwa ya intaneti ina taarifa na makala kuhusu mamilioni ya vitu kwa lugha mbalimbali na ndiyo inayotembelewa zaidi na watu katika mtandao huo. Hata hivyo uwezekano wa kila mtu kuingia na kuandika atakavyo katika ensaiklopidia hiyo umeshusha chini hadhi na nafasi yake ya kielimu. Zaidi ni kwamba licha ya kuwa wasimamizi wa Wikipedia wanadai hawapendelei upande wowote lakini kwa kawaida makala zinazohusiana kwa njia moja au nyingine na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel huwa za upendeleo.
Kituo kikuu cha Wikipedia kiko katika jimbo la Florida nchini Marekani na ensaiklopidia hiyo inafanya kazi kwa mujibu wa sheria za Marekani.

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita inayosadifiana na tarehe 25 Dey 1357 Hijria Shamsia, kulitokea mapigano makali baina ya jeshi la utawala wa Shah na wananchi wa Iran kufuatia maandamano ya mara kwa mara ya wananchi dhidi utawala huo wa kidikteta. Katika mapigano hayo baadhi ya wanajeshi waliotambua sababu za mapambano ya wananchi, waliamua kuzikimbia kambi zao za kijeshi na kujiunga katika safu za wananchi. Kujiunga wanajeshi na safu za wananchi ilikuwa bishara njema ya mabadiliko makubwa katika moyo na muundo wa jeshi la utawala wa Shah. Wakati huo huo Imam Khomeini ambaye alikuwa uhamishoni nchini Ufaransa, alikuwa akituma taarifa mara kwa mara akiwahimiza wanajeshi kujiunga na mapambano ya wananchi, kuuhami na kuutetea Uislamu na sheria zake na kuwafukuza wageni waliokuwa wakidhibiti kila kitu nchini Iran.

Siku kama ya leo miaka 117 iliyopita aliaga dunia Sheikh Muhammad Abduh ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika mji wa Alexandria nchini Misri. Alipata elimu katika Chuo Kikuu cha al Azhar na kisha akahudhuria darsa za Jamaluddin Asadabadi, mwanazuoni aliyepigania uhuru wa nchi za Kiislamu. Baada ya kupelekwa uhamishoni Sayyid Jamaluddin, Sheikh Muhammad Abduh alichukua nafasi yake ya kufundisha na kutoa elimu kwa wanazuoni na wanafikra za Kiislamu. Hata hivyo Sheikh Abduh alibaidishiwa nchini Syria baada ya satuwa ya wakoloni wa Kiingereza kuenea nchini Misri. Baada ya kufunza kwa kipindi cha miaka sita nchini Syria alihamia Paris na kusaidiana na Sayyid Jamaluddin Asadabadi katika kuchapisha gazeti la al Uruwatul Wuthqaa.

Miaka 127 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mwanazuoni wa Kiislamu, Muhammad Baqir Zainul Abidin Khansari katika mji wa Isfahan nchini Iran. Alikuwa hodari katika elimu za fiqhi na hadithi na alipewa ijaza ya kunukuu Hadithi na wanazuoni wakubwa katika taaluma hiyo. Baada ya muda msomi huyo mkubwa ambaye alikuwa gwiji wa wasifu na shajara za maulamaa na wataalamu wa fiqhi ya Kiislamu, alishika hatamu za kuongoza chuo kikuu cha kidini cha Isfahan. Mirza Muhammad Baqir Khansari ameandika vitabu vingi na miongoni mwa vitabu vyake ni Raudhaatul Jannat na Hashiyatu Sharhil Lum'ah.

Siku kama ya leo miaka 180 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 15 Januari 1839 Miladia, nchi ya El Salvador ilijitangazia rasmi uhuru wake baada ya kusambaratika Muungano wa Amerika ya Kati, amma nchi hiyo haikupata amani na utulivu hata baada ya kupita karne moja. El Salvador ambayo ilikuwa ikikoloniwa na Uhispania kwa miaka kadhaa, ilijipatia uhuru wake mwaka 1821, na ulipofika mwaka 1824 ilijiunga na Muungano wa Amerika ya Kati, na hatimaye uliposambaratika muungano huo, nchi hiyo ilijitegemea kikamilifu. El Salvador ilikabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi mwaka 1931, baada ya kuporomoka bei ya kahawa katika soko la dunia, zao lililokuwa likitegemewa nchini humo. Hali mbaya ya kiuchumi iliwakasirisha wananchi wa nchi hiyo, na kupelekea kuanza kuibuka uasi wa wananchi na wanachuo dhidi ya dikteta Jenerali Maximiliano Hernandez Martinez wa El Salvador.
