Jan 16, 2019 00:56 UTC
  • Jumatano, tarehe 16, Januari 2019

Leo ni Jumatano tarehe 9 Jamadil Awwal 1440 Hijria sawa na Januari 16 mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita Rais Laurent Desire Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alipigwa risasi na mmoja wa walinzi wake katika ikulu ya Rais na kujeruhiwa vibaya. Baada ya tukio hilo kulienea habari za kutatanisha juu ya hatima ya kiongozi huyo. Tarehe 18 Januari yaani siku mbili baadaye, serikali ya Kinshasa ilithibitisha kufariki dunia Rais Laurent Desire Kabila . Kabila alizaliwa mwaka 1939 huko Katanga na kupata elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania. Aliingia madarakani mwaka 1997 baada ya vikosi vya askari aliokuwa akiwaongoza kuuteka mji wa Kinshasa na kumlazimisha Mobutu Sese Seko, rais wa wakati huo wa Zaire ya zamani kukimbilia nje ya nchi. Tarehe 26 Januari Joseph Kabila mwana wa Rais Kabila alishika haramu za uongozi nchini Congo.

Laurent Desire Kabila

Tarehe 26 Dey 1357 Hijria Shamsia yaani siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, Muhammad Reza Pahlavi, mfalme wa mwisho wa Iran alitoroka nchini kwa kisingizio cha kwenda kupata matibabu nje ya nchi, baada ya kushadidi wimbi la harakati za mapinduzi. Muhammad Reza Pahlavi alichukua kiti cha ufalme mwaka 1320 Hijria Shamsia baada ya serikali ya Uingereza kumpeleka uhamishoni baba yake, Reza Shah, kwa sababu aliiunga mkono Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Siku chache kabla ya tukio hilo, Imam Ruhullah Khomeini ambaye wakati huo alikuwa Ufaransa, alitoa ujumbe mzito akisema kuwa: "Safari ya Shah bila ya kung’atuka madarakani haitabadilisha lolote na utawala wa kifalme nchini Iran unapaswa kuangushwa kikamilifu".

Shah akikimbia nchi

Miaka miaka 62 iliyopita katika siku sawa na ya leo alifariki dunia mtunzi wa nyimbo mwenye asili ya Italia kwa jina la Arturo Toscanini. Toscanini alizaliwa mwaka 1867 na alianza kupenda muziki akiwa kijana. Arturo Toscanini alikuwa kiongozi wa bendi baada ya kufanya mazoezi mengi na kusafiri katika nchi mbalimbali duniani. Aidha alipata umashuhuri kutokana uwezo wake mkubwa wa kuhifadhi na kuwa makini katika utunzi wa nyimbo. Toscanini aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 90 yaani miaka mitatu baada ya kustaafu kazi ya muziki.

Arturo Toscanini

Katika siku kama ya leo miaka 173 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Januari 1846, vilianza vita baina ya Marekani na Mexico baada ya Washington kuishambulia nchi hiyo. Vita hivyo vilivyochukua muda wa miaka miwili, vilitokea baada ya Marekani kudai kwamba wahajiri wa nchi hiyo wanateswa nchini Mexico. Hata hivyo ukweli ni kuwa, Marekani ilianzisha mashambulizi hayo kwa lengo la kuyatwaa baadhi ya maeneo ya Mexico hususan eneo la Texas. Katika vita hivyo, Marekani iliyakalia kwa mabavu majimbo ya Texas, California, Nevada, Utah, Arizona na New Mexico.

Mchoro wa jinsi askari wa Marekani walivyoingia katika vita na Mexico.

Katika siku kama ya leo miaka 460 iliyopita alizaliwa katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran Ṣadruddin Muḥammad bin Ibrahim al-Shirazi maarufu kwa jina la Ṣadrul Muta'allihīn au Mulla Sadra, mwanafalsafa na arif mkubwa wa Kiislamu. Awali alielekea katika mji wa Qazwin uliokuwa katika zama hizo mji mkuu wa utawala wa Safavi na kuhudhuria darsa na masomo ya walimu wakubwa kama Sheikh Bahai. Alisoma Fikihi, Usul, hadithi na hisabati kwa Sheikh Bahai na kusoma mantiki, falsafa na Irfan kwa Mirdamad. Baada ya Isfahan kufanywa mji mkuu, Mulla Sadra naye alihamia katika mji huo na kuanza kufundisha. Hata hivyo kutokana na mitazamo yake kupingana na maulama kadhaa, Mulla Sadra alilazimika kuuhama mji huo na kuanza kuishi katika kijiji cha karibu na mji wa Qum. Baada ya muda alianza tena kujishughulisha na kazi ya kufundisha na kualifu vitabu. al Mabdau Wal-Maad, Zadul Musafir na Mutashaabihaat al-Qur'an ni baadhi tu ya vitabu vya Ṣadrul-Muta'allihīn.

Mulla Sadra

Siku kama ya leo miaka 654 iliyopita sawa na tarehe 9 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 786 Hijria, aliuawa shahidi faqihi na mtaalamu mkubwa wa hadithi Muhammad bin Jamaluddin Makki Amili, mashuhuri kwa jina la "Shahidi wa Kwanza." Alizaliwa mwaka 734 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Jabal Amil nchini Lebanon. Alijifunza elimu mbalimbali kutoka kwa walimu wakubwa wa zama zake kama vile Allama Hilli. Mbali na elimu ya dini, Muhammad bin Jamaluddin pia alikuwa hodari katika taaluma za mashairi na fasihi. Katika miaka 52 ya umri wake uliojaa baraka, Shahidi wa Kwanza aliandika vitabu vingi, ikiwa ni pamoja na "Albaqiyatus-Swalihat" na "al Lumuatu Dimashqiyya." Aliuawa na wapinzani wenye taasubi katika siku kama ya leo. 

Muhammad bin Jamaluddin Makki Amili