Jan 18, 2019 00:23 UTC
  • Ijumaa tarehe 18 Januari mwaka 2019

Leo ni Ijumaa tarehe 11 Jamadil Awwal 1440 Hijria sawa na 18 Januari mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita yaani tarehe 18 Januari 1919, ulifanyika mkutano wa kihistoria wa amani baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, kwa kuwashirikisha wawakilishi wa nchi 27 kutoka mabara matano duniani. Mkuu wa mkutano huo alikuwa Georges Clémenceau, waziri mkuu wa wakati huo wa Ufaransa. Nchi tano zilizokuwa zimeshindwa kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia yaani Ujerumani, Austria, Hungary, Bulgaria na dola la Othmania, hazikushiriki kwenye mkutano huo. Kwa mujibu wa mkataba uliotiwa saini katika mkutano huo, Ujerumani ililazimishwa kulipa fidia kubwa na kutoa sehemu za ardhi zake kwa Austria. Mkutano huo ulikuwa utangulizi wa kuanzishwa Jumuiya ya Kimataifa.

Georges Clémenceau

Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita mkataba maarufu kwa jina la 'Mkataba wa Siri' ulitiwa saini kati ya nchi tatu za Ufaransa, Uingereza na Russia wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Sababu kuu ya mtakaba huo ilikuwa kadhia ya kujiunga utawala wa Kiothmani (Ottoman Empire) na waitifaki wa Vita vya Kwanza vya Dunia, yaani Ujerumani na Austria. Kwani kujiunga utawala huo na waitifaki hao, kungekata uhusiano wa jeshi la majini la Russia na waitifaki wake katika Bahari Nyeusi. Baada ya kutiwa saini mkataba huo, nchi waitifaki zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya lango bahari la Dardanelles linalounganisha Bahari Nyeusi na Bahari ya Mediterranean.

Ramani ya lango bahari la Dardanelles

Siku kama ya leo miaka 330 iliyopita, alizaliwa mwandishi na mwanafikra maarufu wa Ufaransa Charles de Montesquieu. Charles alikuwa miongoni mwa wasomi ambao fikra na itikadi zao zilikuwa na taathira kubwa katika harakati ya mapinduzi ya Ufaransa na alikuwa mtu wa kwanza kutoa nadharia ya udharura wa kutenganishwa nguvu kuu tatu za dola. Kitabu maarufu cha Charles de Montesquieu ni "The Spirit of the Laws" (Roho ya Sheria) ambacho kilichapishwa mwaka 1748 huko Geneva, Uswis. Kitabu kingine cha mwanafalsafa huyo wa Kifaransa ni (Barua za Kiirani) au "Persian Letters".

Charles de Montesquieu

Na miaka 843 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Khaja Nasiruddin Tusi, mwanafalsafa, mwanahisabati, mnajimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiirani katika mji wa Tus kaskazini mashariki mwa Iran. Katika maisha yake aliasisi kituo kikubwa cha kielimu na akademia ya kwanza ya sayansi yaani mahala pa kuangalilia mwendo wa nyota, mwezi na jua huko Maraghe kaskazini magharibi mwa Iran. Aalimu huyo aligundua namna mpya ya kutumia saa ya jua kwa ajili ya kituo hicho. Kituo hicho kilikuwa na suhula muhimu zaidi ambazo hazikuwa na mfano wake hata katika nchi za Magharibi miaka 300 baada yake.  

Nasiruddin Tusi ameandika vitabu zaidi ya 80 kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi. Vitabu muhimu zaidi vya msomi huyo ni pamoja na ‘Asasul-Iqtibaas’, ‘Akhlaaq Naasiri’, ‘Awsaful-Ashraaf’ na ‘Sharhul Ishaarat.

Khaja Nasiruddin Tusi