Jan 21, 2019 23:20 UTC
  • Jumanne tarehe 22 Januari 2019

Leo ni Jumanne tarehe 15 Jamadil Awwal 1440 Hijria sawa na tarehe 22 Januari 2019.

Siku kama ya leo miaka 1402 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, alizaliwa Imam Ali bin Hussein (AS) maarufu kwa laqabu ya Zainul Abidin katika mji mtakatifu wa Madina. Mtukufu huyo ni mwana wa Imam Hussein bin Ali Bin Abi Twalib, mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (SAW). Alikuwa kinara wa elimu, uchamungu, wema ukarimu na upendo. Miongoni mwa sifa kuu za Imam Zainul Abidin ni kufanya ibada na kusali Swala za usiku. Alikuwa mwingi wa ibada na alipewa laqabu ya Sajjad kwa maana ya mwenye kusujudu sana na Zainul Abidin kwa maana ya 'Pambo la Wafanya Ibada' kutokana na sijda zake ndefu katika Swala. Imam Zainul Abidin alichukua jukumu la kuendeleza ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein ya kupambana na ufisadi na dhulma ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuuawa baba yake katika medani ya Karbala. Aliishi miaka 35 baada ya tukio hilo chungu na aliuawa shahidi na mtawala wa Bani Ummayah Hisham bin Abdul Malik. Athari maarufu zaidi ya mtukufu huyo ni kitabu cha dua na miongozo ya Kiislamu cha al Sahifa as Sajjadiyya.

Tarehe 15 Jamadil Awwal mwaka 38 Hijria miaka 1402 iliyopita aliuawa shahidi Muhammad bin Abu Bakr ambaye alikuwa miongoni mwa maswahaba waaminifu wa Imama Ali bin Abi Twalib (as) na kamanda maarufu wa jeshi la Uislamu katika vita dhidi ya jeshi la Muawiya lililokuwa likiongozwa na Amr bin al As. Mtawala wa kizazi cha Banii Umayyah, Muawiya alituma jeshi la wapiganaji elfu sita nchini Misri kwa ajili ya kupigana na jeshi la Muhammad bin Abu Bakr lililokuwa na wapiganaji elfu mbili. Jeshi la Muhammad bin Abu Bakr lilishindwa katika vita hivyo na kiongozi huyo akauawa shahidi kwa kuchomwa moto baada ya kukamatwa mateka.

Miaka 210 iliyopita na katika siku kama ya leo, Mirza Muhammad Hassan Shirazi, mmoja wa wanazuoni na mamar'ja' mashuhuri wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kuendeleza masomo yake ya kidini na kupata elimu kwa wanazuoni mashuhuri wa mji huo kama Sheikh Murtadha Ansari. Bidii yake kwenye masomo ilimuwezesha kukwea haraka daraja za elimu na kuwa mhadhiri na mwanazuoni wa ngazi za juu mjini hapo na katika ulimwengu mzima wa Kiislamu. Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatua yake ya kuharamisha tumbaku katika kipindi cha utawala wa Nassir Deen Shah kutoka ukoo wa Qajaar. Fatuwa yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Fatuwa hiyo ilichukuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran. Kwa hakika iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni nchini.

Mirza Muhammad Hassan Shirazi

Siku kama ya leo miaka 139 iliyopita toleo la kwanza la gazeti la al Uruwatul Wuthqaa lilichapishwa chini ya uongozi wa Sayyid Jamaluddin Asadabadi maarufu kwa jina la Jamaluddin Afghani na Sheikh Muhammad Abduh mjini Paris, Ufaransa. Sayyid Jamaluddin aliasisi Jumuiya ya al Uruwatul Wuthqaa kwa shabaha ya kutimiza lengo lake la kujenga umoja na mshikamano kati ya mataifa ya Kiislamu na akaanza kuchapisha gazeti kwa kutumia jina hilo hilo.

Sayyid Jamaluddin Afghani

Miaka 40 iliyopita katika siku kama hii ya leo, kufuatia kuendelea upinzani wa wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala wa mfalme Shah, kulitokea mapigano baina ya raia na wanajeshi na kupelekea wananchi wengi kuuawa na wengine kujeruhiwa. Wakati huo huo, wananchi Waislamu wa Iran walikuwa wakisubiri kwa hamu na shauku kubwa kurejea nchini Imam Khomeini kutoka uhamishoni na walikuwa wamefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya mapokezi makubwa ya kihistoria ya kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kamati maalumu iliyokuwa ikijumuisha viongozi wa kidini na wawakilishi wa matabaka mbalimbali ya wananchi iliundwa mjini Tehran, ili kutekeleza shughuli ya mapokezi ya Imam Khomeini  kwa hamasa kubwa kadiri inavyowezekana. Wakati huo huo, wananchi kutoka mikoa mbalimbali hpa Iran walikuwa wakimimika mjini Tehran kwa ajili ya kushiriki katika mapokezi ya Imam Khomeini. Aidha baada ya maandamano makubwa ya wananchi, askari 4,000 wa Jeshi la Anga wakiwaunga mkono wananchi wanamapambano wa Iran, walifanya mgomo wa chakula wakitaka kutimuliwa nchini Iran washauri wa Kimarekani.