Jan 25, 2019 01:11 UTC
  • Ijumaa, tarehe 25 Januari, 2019

Leo ni Ijumaa tarehe 18 Jamadil Awwal 1440 Hijria sawa na 25 Januari 2019.

Siku  kama ya leo miaka 13 iliyopita Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge ikiwa ni mara ya kwanza kwa harakati hiyo kushiriki kwenye zoezi hilo. Katika uchaguzi huo uliosimamiwa na waangalizi wa kigeni, Hamas ilifanikiwa kupata viti 76 kati ya jumla viti 132 vya Bunge la Palestina licha ya propaganda chafu zilizokuwa zikifanywa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi. Kwa utaratibu huo Hamas ilimuarifisha Ismail Hania kama Waziri Mkuu na kutangaza kwamba itaunda serikali ya umoja wa kitaifa. Hata hivyo nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani na muitifaki wake Israel, zilikataa kutambua rasmi serikali hiyo iliyochaguliwa kidemokrasia na wananchi wa Palestina.

جنبش مقاومت اسلامی فلسطین

Tarehe 5 Bahman miaka 40 iliyopita matabaka mbalimbali ya wananchi wa Iran waliendeleza maandamano makubwa katika miji mbalimbali dhidi ya utawala kibaraka wa Shah licha ya mamluki wa mfalme huyo kutumia mbinu zote za ukatili na ukandamizaji. Siku hiyo wananchi Waislamu wa Iran walipuuza marufuku iliyokuwa imetangazwa ya kuzuia mikusanyiko ya zaidi ya watu mawili katika miji mbalimbali ya Iran. Ukandamizaji mkubwa wa maajenti wa utawala wa Shah ulipelekea kuuawa shahidi idadi kubwa ya raia. Siku hiyo hiyo idadi kubwa ya maafisa wa Jeshi la Anga la Iran ilijiunga na harakati ya mapambano ya wananchi katika mitaa ya jiji la Tehran na kufanya maandamano dhidi ya utawala wa Shah. Askari hao walitangaza utiifu wao kwa Imam Ruhullah Khomeini na harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 148 iliyopita vijidudu maradhi vinavyosababisha maradhi ya ukoma viligunduliwa na tabibu na mhakiki wa Ujerumani kwa jina la Gerhard Henrik Armauer Hansen. Ugonjwa huo huambatana na vidonda vikali vinavyovuruga na kuharibu maumbo ya muathirika. Vijidudu maradhi vya ugonjwa huo wa ukoma pia hukusanyika katika mishipa ya neva na kusababisha uharibifu katika sehemu kubwa ya mishipa hiyo. Maradhi hayo hujitokeza zaidi katika maeneo yenye joto. Licha ya maendeleo makubwa ya kisayansi yaliyopatikana katika kudhibiti ugonjwa wa ukoma, lakini njia ya kutibu maradhi hayo sugu bado haijapatikana na idadi kubwa ya waathirika wake wanaendelea kuteseka katika nchi mbalimbali duniani.

Gerhard Henrik Armauer Hansen

Katika siku kama ya leo miaka 563 iliyopita, kazi ya uchapishaji vitabu ilianza na kitabu cha kwanza kabisa kikachapishwa kwa kutumia mashine iliyogunduliwa na Mjerumani, Johannes Gutenberg. Mashine hiyo ya uchapishaji ilikuwa hatua muhimu katika njia ya uchapishaji na uenezaji wa elimu na maarifa kati ya wanadamu. Katika zama zake, Johannes Gutenberg pia alichapisha kitabu cha Biblia maarufu kwa jina la' Gutenberg Bible.' Hii leo kurasa kadhaa zilizobakia za kitabu hicho zinahifadhiwa katika majumba ya makumbusho. 

Kiwanda cha kuchapisha vitabu

Katika siku kama ya leo miaka 990 iliyopita, Abu al-Abbas Ahmad bin Ali maarufu kwa jina la Najjashi aliaga dunia huko Samarra, Iraq akiwa na umri wa miaka 78. Najjashi alikuwa alimu na msomi mkubwa katika karne ya tano Hijria na alibobea na kutabahari katika elimu ya hadithi na wapokezi wa hadithi. Kitabu cha Rijali ni miongoni mwa vitabu muhimu vya msomi huyo wa Kiislamu.

Katika siku kama ya leo miaka 1112 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Ahmad bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Abdu Rabbuh mshairi na mwandishi mahiri wa Kiarabu. Abdu Rabbuh alibobea mno katika mashairi. Athari mashuhuri zaidi ya msomi huyo ni kitabu cha al Iqdul Fariid ambacho kinahusiana na historia, lugha na mashairi.