Jumapili, Januari 27, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 20 Jamadul Awwal 1440 Hijiria, sawa na tarehe 27 Januari 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 758 iliyopita, alizaliwa Muhammad Bin Hassan Hilli, aliyepewa lakabu ya 'Fakhrul-Muhaqiqina' faqihi na mtafiti mkubwa wa Kiislamu katika mji wa Hillah nchini Iraq. Alilelewa na baba yake Allamah Hilli ambapo akiwa kijana alifikia daraja ya ijtihadi. Fakhrul-Muhaqiqina kama ambavyo alikuwa maarufu kutokana na mustawa wake wa juu wa kielimu, alitabahari pia katika elimu ya fasihi na ucha-Mungu. Aidha msomi huyo aliandika vitabu vingi vya rafsiri ya Qur'an, fiqihi, usulu fiqihi pamoja na theolojia. miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Sharhu Mabaadiul-Usuul', 'Tahswilun-Najaat' na 'Al-Kaafiyah.' Allamah Fakhrul-Muhaqiqina alifariki dunia mwaka 771 Hijiria.
Siku kama ya leo miaka 703 iliyopita alifariki dunia Abu Abdillah Muhammad Bin Muhammad Abdari Fasi mashuhuri kwa jina la Ibn Hajj, faqihi mkubwa wa Kiislamu. Al Fasi awali alipata elimu kwa maulamaa wa mji wa Fas huko Morocco ya leo. Baadaye alielekea Cairo na kuishi huko hadi alipoaga dunia. Faqihi Abu Abdullah al Fasi ameandika vitabu vingi vya thamani kikiwemo kile cha al Madkhal. Katika kitabu hicho, Ibn Hajj amechunguza masuala mbalimbali yakiwemo ya kiakhlaqi, kifiqi, kijamii na kiuchumi.
Siku kama ya leo miaka 128 iliyopita, alizaliwa Ilya Ehrenburg mwandishi wa Umoja wa Kisovieti yaani Urusi ya zamani. Ilya alifanya kazi ya uandishi habari kwa miaka kadhaa huko Uhispania na kuanza kujishughulisha na utunzi wa mashairi pia. Ehrenburg alifahamika vyema nchini humo kama mwandishi wa hadithi na mwanahabari, khususan pale alipokuwa akiripoti matukio katika Vita vya Kwanza vya Dunia, vya Pili na vile vya ndani vya Uhispania. Mwandishi huyo wa Kirusi aliandika vitabu visivyopungua 100 ambapo miongoni mwake ni hivi alivyovipa majina ya "Tufani" na "Tuanguka Paris". Ilya alifariki dunia mwaka 1967.
Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita aliaga dunia Johann Gottlieb Fichte, mwanafalsafa wa Ujerumani. Fichte alizaliwa tarehe 19 Mei 1762 Miladia katika familia masiki nchini Ujerumani. Hata hivyo kutokana na kuwa na kipaji na kumbukumbu ya ajabu alipewa uzingatiaji na mmoja wa viongozi ambaye aliamua kumsimamia masomo yake na kujiunga na fani ya theolojia katika Chuo Kikuu cha Jena nchini humo. Akiwa chuoni hapo alisoma athari na fikra za Immanuel Kant, mwanafalsafa mashuhuri wa nchi hiyo ambapo aliathiriwa sana na mitazamo yake. Muda punde baadaye alikuwa kiongozi wa harakati mpya ya idiolojia nchini Ujerumani ambapo wafuasi wake walikuwa wakiamini kwamba akthari ya miili imeumbwa. Fikra za Fichte zilimfanya kukosolewa na vyuo vikuu vingine hasa kwa kuzingatia kuwa, misimamo yake ilikuwa inakinzana na mafundisho ya dini.
Na siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, makubaliano ya kusitisha vita kati ya Marekani na Vietnam Kaskazini yalitiwa saini mjini Paris Ufaransa, baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa kipindi cha miaka minne. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya Paris, Marekani ilikubali kuondoa majeshi yake huko Vietnam Kusini. Japokuwa baada ya kutiwa saini makubaliano hayo vita kati ya Marekani na Vietnam Kaskazini havikusitishwa, lakini serikali ya Washington ililazimika kuondoa majeshi yake huko Vietnam Kusini baada ya kupata hasara kubwa za hali na mali. Makubaliano ya Paris yalikuwa pigo kubwa kwa siasa za uingiliaji na za kibeberu za Marekani nchini Vietnam ambazo zilianza kutekelezwa mwaka 1964.