Jan 27, 2019 23:16 UTC
  • Jumatatu tarehe 28 Januari 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 21 Jamadil Awwal 1440 Hijria sawa na Januari 28 mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 6 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilituma kwa mara ya kwanza kiumbe hai katika anga za mbali kwa kutumia roketi. Kiumbe huyo alikuwa tumbili ambaye alirejea salama ardhini baada ya jaribio hilo lililofanyika kwa mafanikio. Majaribio hayo yalidhihirisha tena maendeleo makubwa ya Iran katika masuala ya anga licha ya vikwazo vikali zaidi vya Marekani na waitifaki wake. 

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, waziri mkuu wa wakati huo wa utawala wa Shah, Shapour Bakhtiar alitanganza azma yake ya kufanya safari mjini Paris, Ufaransa kwa ajili ya kukutana na Imamu Khomein (MA). Hata hivyo mkabala wake Imamu Khomein aliitaja hatua hiyo kuwa ya hadaa kwa kusema: "Kile kilichoelezwa na Shapour Bakhtiar kwamba nimekubali kukutana naye ni uongo, bali ni kwamba asipojiuzulu sitomkubali." Kadhalika siku hiyo wakazi wa mji wa Tehran waliendelea kujitayarisha kwa ajili ya kumpokea Imamu Ruhullah Khomein katika maeneo ya uwanja wa ndege wa Mehrabad mjini Tehran kutoka uhamishoni nchini Ufaransa.

Shapour Bakhtiar

Miaka 40 iliyopita katika siku kama hii ya leo, kundi kubwa la wanazuoni wa Kiislamu lilianzisha mgomo wa kuketi katika msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran baada ya Waziri Mkuu wa serikali ya wakati huo ya Shah, Shapoor Bakhtiyar, kumzuia Imam Khomeini kurejea nchini Iran akitokea uhamishoni. Wanazuoni hao walisema, sharti pekee la kusitisha mgomo huo ni kuruhusiwa Imam Khomeini kurejea nchini. Mgomo huo ulikuwa miongoni mwa matukio muhimu katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Kwani kwa upande mmoja, serikali ya wakati huo ya Shah iliyokuwa ikiungwa mkono na Marekani, ilifanya jitihada kubwa za kumzuia Imam Khomeini asirejee nchini, na kwa upande mwingine ilikuwa ikifanya njama za kuzusha hitilafu na migawanyiko kati ya matabaka mbalimbali ya wananchi kwa kutoa ahadi na kutumia vitisho. Mgomo huo wa wanazuoni wa Kiislamu uliowashirikisha maulamaa mashuhuri kama Shahid Ayatullah Murtadha Mutahhari na Ayatullah Muhammad Beheshti, ulikifanya Chuo Kikuu cha Tehran kuwa kituo kikuu cha harakati za mapambano.

Maulamaa wakiwa katika mgomo katika Chuo Kikuu cha Tehran

Siku hii ya leo, yaani tarehe 28 mwezi Januari, inaadhimishwa duniani kama Siku ya Kimataifa ya Kuwasaidia Wagonjwa Wenye Maradhi ya Ukoma. Siku hii ilipewa jina hilo na Raul Follivero, raia wa Ufaransa yapata nusu karne iliyopita. Wakati huo dunia ilikuwa watu milioni 15 waliokuwa wakisumbuliwa na maradhi hayo. Kufuatia hali hiyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) liliiainisha tarehe 28 ya Januari kuwa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ugonjwa wa Ukoma. Tangu yalipoanza mapambano dhidi ya ukoma  waathirika wa maradhi hayo wamepungua na kufikia watu milioni mbili. Hata hivyo licha ya juhudi hizo, ugonjwa wa ukoma bado haujatokomezwa kikamilifu.

Na miaka 1120 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 21 Mfunguo 8 mwaka 320 Hijiria, alizaliwa Abu Jaafar Ahmad bin Ibrahim Qirawani, aliyekuwa mashuhuri wka jina la Ibn Jazzar. Msomi huyo wa Morocco alikuwa tabibu, mwanafalsafa na mwanajiografia mashuhuri wa Kiislamu. Ibn Jazzar alikuwa tabibu mwenye moyo wa kujitolea na anayewatakia watu kheri na aliandika kitabu alichokipa jina la "Twibul Fuqaraa” au Tiba ya Watu Maskini." Mwanafalsafa huyo ameandika vitabu 20. Miongoni mwa vitabu vyake ni Risalatun Fii Ibdalil Adwiya na Zadul Musafir.