Ijumaa tarehe Mosi Februari 2019
Leo ni Ijuma tarehe 25 Jamadil Awwal 1440 Hijria sawa na tarehe Mosi Februari 2019.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita Imam Khomein (MA) Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, alirejea nchini na kupokelewa kwa shangwe kubwa na wananchi baada ya kuishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 15. Mapokezi hayo makubwa ya wananchi wa Iran kwa Imam Khomeini hayajawahi kushuhudiwa mfano wake katika historia ya sasa ya dunia. Baada ya kutoa hotuba fupi katika uwanja wa ndege wa Mehrabad, Imam Khomein alielekea moja kwa moja kwenye makaburi ya mashahidi waliouawa katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kutoa heshima kwa mashahidi hao ambako pia alitoa hotuba katika umati mkubwa wa wananchi. Kwa mara nyingine Imam aliitaja serikali ya Shapour Bakhtiar kuwa kibaraka wa Shah na kutangaza kwamba ataunda serikali mpya kwa msaada wa wananchi. Siku kumi baada ya kurejea nchini Imam, Mapinduzi ya Kiislamu yalipata ushindi kamili na kipindi hicho cha siku kumi za baina ya kurejea Imam nchini hadi kupata ushindi kamili Mapinduzi ya Kiislamu, kinajulikana hapa nchini kama "Alfajiri Kumi".
Tarehe Mosi Februari miaka 61 iliyopita iliundwa Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu ya Syria na Misri. Baada ya kumalizika vita vya Suez na kurudi nyuma askari wa Uingereza, Ufaransa na utawala ghasibu wa Israel kutoka katika ardhi ya Misri, Gamal Abdul Nasser alitambuliwa kuwa kiongozi dhidi ya ukoloni wa Magharibi na dhidi ya Uzayuni katika ulimwengu wa Kiarabu na kupata umashuhuri mkubwa. Hatua ya kwanza ya kuanzisha muungano wa nchi za Kiarabu dhidi ya utawala haramu wa Israel na waungaji mkono wake wa Magharibi ilichukuliwa tarehe Mosi Februari 1958 baada ya Syria kutia saini makubaliano ya kuungana na Misri na muungano huo ulianza rasmi baada ya kura ya maamuzi ya tarehe 22 Februari 1958 katika nchi hizo mbili.
Siku kama ya leo miaka 205 iliyopita, kulitokea vita vikali na vya umwagaji damu mkubwa maarufu kwa jina la Routier katika eneo lenye jina kama hilo karibu na Mto Ob kati ya jeshi lililokuwa na askari laki moja na 60 elfu la vikosi vya waitifaki wa nchi za Prussia, Austria na Sweden na jeshi lililokuwa na askari elfu 42 la Ufaransa chini ya uongozi wa Napoleon. Katika vita hivyo jeshi la Ufaransa lilishindwa vibaya na waitifaki kutokana na kutokuwa na moyo wa kupigana na uchache wa wapiganaji wake.
Na siku kama ya leo miaka 1376 alifariiki dunia Khalifa wa tatu wa utawala wa Bani Umayyah, Muawiya bin Yazid katika mazingira ya kutatanisha. Alichukua madaraka baada ya kufariki dunia baba yake, yaani Yazid bin Muawiya. Hata hivyo kutokana na kuwa, alikuwa akiamini kwamba Ahlubaiti wa Mtume ndio wenye haki ya kuongoza Umma wa Kiislamu, Muawiya bin Yazid hakuwa na hamu ya kushika hatamu na kuwa kiongozi wa utawala wa Kiislamu. Muawiya bin Yazid ambaye ni maarufu kwa jina la Muawiya wa Pili alitoa hotuba mbele ya watu na kulaani vita vya babu yake yaani Muawiya bin Abi Sufian dhidi ya Imam Ali bin Abi Twalib na vile vya baba yake yaani Yazi bin Muawiya dhidi ya Imam Hussein (as) na kuwataja kwa wema Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw). Alisema: Jambo baya zaidi ni kwamba, tunajua kuwa Yazid (baba yake) alikufa vibaya na kurejea kwa Mola kwa fedheha. Aliua kizazi cha Mtume (saw) na kuwavunjia heshima na akachoma moto al Kaaba. Mimi sitaki madaraka ya utawala wenu na naachia utawala na madaraka…" Baada ya hapo Muawiya bin Yazid alijiuzulu utawala na siku chache baadaye alifariki dunia katika mazingira ya kutatanisha. Utawala wa Bani Umayya baada yake uliongozwa na Marwan bin al Hakam.
