Jumamosi, Februari 2, 2019
Leo ni Jumamosi tarehe 26 Mfunguo Nane Jamad al-Awwal 1440 Hijria mwafaka na tarehe Pili Februari 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 227 iliyopita, mkataba wa kihistoria wa Berlin, ulitiwa saini baina ya Leopold II mfalme wa wakati huo wa Austria na Frederick William aliyekuwa mfalme wa Prussia. Mkataba huo ulikuwa natija ya maafikiano baina ya viongozi hao wawili yaliyofikiwa tarehe Pili Agosti mwaka 1791 huko Pillnitz kwa ajili ya kukabiliana na mapinduzi ya Ufaransa. Hii ilitokana na kuwa, watawala wa Ulaya walikuwa wameingiwa na woga mkubwa kutokana na baadhi ya nadharia za wapigania uhuru wa Ufaransa. Licha ya kuweko mkataba huo na hata mashambulio ya pamoja ya Austria, Prussia na Uingereza dhidi ya Ufaransa na himaya yao kwa wapigania mfumo wa utawala wa Kifalme wa nchi hiyo, harakati hizo hazikuwa na natija kwani hatimaye wanamapinduzi wa Ufaransa waliibuka na ushindi. ***
Miaka 123 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 13 Bahman, aliaga dunia Ayatullah Mirza Javad Mujtahid Tabrizi, alimu, msomi, mwanamapambano na aliyekuwa mchaji-Mungu. Alizaliwa mjini Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran katika familia iliyosifika kwa kushikama na dini. Mirza Javad Tabriz alisoma masomo ya awali kwa baba yake na kisha akaelekea katika mji wa Najaf Iraq ambapo akiwa huko alihudhuuria darsa za maulama waliokuwa mahiri katika zama hizo kama Sheikh Muurtadha Ansari na Sayyid Hussein Kuh Kamari na kufanikiwa kufikia marhala ya Ijtihadi. Baada ya kurejea katika mji aliozaliwa wa Tabriz, Ayatullah Mirza Javad Tabriz alijishughulisha na tablighi na kazi ya kufundisha. Akiwa Imam wa Swala ya Ijumaa mjini Tabiriz, msomi huuyo alikuwa na ushawishi mkubwa miongoni mwa wananchi. Ayatullah Mirza Javad Tabrizi alikuwa akipinga vikali uingiliaji wa Russia na Uingereza katika masuala ya ndani ya Iran. ***
Katika siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, Dmitri Ivanovich Mendeleev msomi na mwanakemia wa Kirusi alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 73 huko Saint Petersburg uliokuwa mji mkuu wa Russia wakati huo. Dmitri alizaliwa mwaka 1834 na kusoma taaluma ya kemia. Msomi huyo alifanya utafiti na uhakiki mwingi muhimu katika taaluma ya kemia ambapo baadaye ulikuja kujulikana kwa jina la jedwali la Mendeleev. ***
Miaka 99 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Ustadh Shahidi Murtadha Mutahhari. Ustadh Mutahhari alizaliwa katika mji wa Fariman Iran na baada ya kumaliza masomo ya awali alisafiri na kuelekea katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha mjini Quum na kuhudhuria darsa za wanazuoni wakubwa wa zama hizo kama Ayatullah al-Udhma Buroujerdi, Allama Tabatabai na Imam Khomeini MA. Wakati wa kuanzisha harakati ya Kiislamu nchini Iran, Shahidi Murtadha Mutahhari naye alijunga na harakati hiyo. Murtadha Mutahhari alitiwa mbaroni mara kadhaa na vyombo vya usalama vya utawala wa Shah. Mbali na harakati za kisiasa, Ayatullah Mutahhari alikuwa na nafasi muhimu pia katika harakati za kijamii na uandishi wa vitabu ambapo amevirithisha vizazi vilivyokuja baada yake vitabu vingi na vyenye thamani kubwa. ***
Na miaka 85 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Ayatullah Allamah Mirza Muhammad Hussein Naini, marjaa na faqihi mkubwa na mmoja wa wahakiki wa elimu ya usulu fiq’h. Allamah Naini alizaliwa mwaka 1276 Hijiria Qamaria mkoani Nain, ambao ni moja ya mikoa ya katikati mwa Iran katika familia ya kidini. Allamah Naini alisoma na kuhitimu masomo yake ya awali nyumbani kwao na kuendelea na masomo ya juu huko mjini Najaf, Iraq. Akiwa mjini hapo, alipata kusoma kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama vile Allamah Mirza Shirazi na kufikia daraja ya juu ya elimu za hesabu, falsafa ya sayansi, falsafa, irfan na fiq’hi. Miongoni mwa athari za Allamah Naini ni pamoja na vitabu vya “Wasiilatun-Najjat” na “Tanbiihul-Ummah wa Tanziihul-Millah” kitabu ambacho kilitoa mchango mkubwa katika kuathiri mapambano dhidi ya viongozi dhalimu wa zama hizo. ***