Ruwaza Njema (10)
Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na karibuni kusikiliza kipindi kingine katika mfululizo wa vipindi vya Ruwaza Njema, ambapo huwa tunanufaika na baadhi ya Hadithi katika kufahamu na kufuata mfano mwema wa Mtume Mtukufu (saw) kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na maisha yetu ya kimaanawi na kimaada.
Katika kipindi cha leo, tutazungumzia suala la kukinaika na mali za kimaada na kufanya juhudi za kunufaika na riziki ya Mwenyezi Mungu, karibuni.
************
Imepokelewa katika kitabu cha Hulyatul Abraar cha Allama al-Baharani akinukuliwa Amru bin Said bin Halaal akisema: 'Nilimwambia Aba Abdillah al-Imam Swadiq (as): Ninasihi, Ewe mwana wa Mtume! Imam (as) akasema: Ninakuusia uzingatie takwa ya Mwenyezi Mungu, umwogope na kufanya bidii. Fahamu kwamba bidii isiyofungamana na kumwogopa Mwenyezi Mungu haina faida yoyote. Na tazama walio chini yako – yaani kuhusiana na uwezo wa kimaada – na wala usiwatazame walio juu yako. Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu amemwambia mara nyingi Mtume wake (saw): Basi zisikushangaze mali zao wala watoto wao (9:55). Pia Amesema: Wala usivikodolee macho tulivyowastareheshea baadhi ya watu miongoni mwao, kwa ajili ya mapambo ya duniani (20:131).
Kisha Imam Swadiq (as) akamshauri muumini huyo afuate mfano mwema wa Mtume Mtukufu (saw) kwa kusema: Nafsi yako itakapokushawishi katika hayo – yaani katika anasa za maisha ya dunia na mapambo yake, elewa na kutambua kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ulikuwa akila mkate wa shayiri, halua ya tende na alipopata kuni zilikuwa ni za matawi ya mtende. Na unapopatwa na msiba basi kumbuka misiba aliyoipata Mtume (saw), kwa sababu hakuna mtu aliyewahi kupata na wala hakuna yeyote atakayepata misiba kama aliyoipta Mtume.'
Na imepokelewa, wapenzi wasikilizaji, katika kitabu cha Aamali cha Sheikh Tousi akinukuliwa Zaid as-Shahaam ambaye anasema: 'Tumeambiwa kuwa Mtume (saw) hakula hadi kushiba mkate wa ngano kwa siku tatu mfululizo.' Imam Swadiq (as) akasema: 'Chakula cha Mtume (saw) kilikuwa ni Shayiri kama kingepatikana, halua ya tende na kuni za matawi ya mtende.'
******
Thiqatul Islam as-Sheikh al-Kuleini (MA) ananukuu Hadithi katika kitabu chake cha al-Kafi kutoka kwa Ali bin Abi Hamza akisema: 'Nilimwona Abal Hassan – yaani Imam Musa Kadhim (as) – akijishughulisha shambani kwake huku miguu yake ikiwa imejaa jasho. Nikasema: Niwe fidia kwako; kwani watu (wafanyakazi) wako wapi? Akasema (as): Ewe Ali! Wamefanya kazi hii kwa mikono yao wenyewe, watu ambao ni bora zaidi kuniliko mimi. Nikasema, je, watu hao ni akina nani? Akasema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na Amir al-Mu'mineen Ali (as). Wote hao walifanya kazi hii kwa mikono yao wenywe. Kufanya kazi kwa mikono ilikuwa ni njia ya manabii, mitume, mawasii na waja wema.'
Na imepokelewa katika kitabu cha Tahdhiib al-Ahkam kwamba Imam Jaffar as-Swadiq (as) aliagiza aonywe mmoja wa masahaba zake ambaye alifahamishwa kwamba alikuwa ameacha biashara kwa ajili ya kujishughulisha na ibada tu. Baada ya kubainisha kwamba hiyo ilikuwa ni moja ya hila za shetani aliamuru aambiwe: 'Je, hajui kwamba Mtume (saw) alinunua mzigo kutoka kwa msafara wa biashara uliokuwa unatoka Sham na kisha kuuza kwa faida ambapo alipata kulipa deni lake kutokana na faida hiyo na kugawa iliyosalia kati ya jamaa zake wa karibu?'
Na tunasoma, ndugu wasikilizaji, katika kitabu cha Aamali cha Sheikh Tousi kuhusiana na hamdu na kuridhia Mtume Muhammad (saw) riziki na kadari ya Mwenyezi Mungu, kauli ya Amir al-Mu'mineen (as) inayosema: 'Mtume (saw) alipokuwa akifikwa na jambo lililomfurahisha (zuri) alikuwa akisema: Hamdu zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye kwa neema zake yanatimia mambo mema, na lilipomfika jambo alilolichukia (baya) alikuwa akisema: Hamdu zote ni za Mwenyezi Mungu katika kila hali.'
*********
Tunakushukuruni nyote wapenzi wasikilizaji kwa kuwa pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambacho kama kawaida kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapojaliwa kukutana tena juma lijalo katika kipindi kingine kama hiki, tunakuageni nyote kwa kusema, kwaherini.