Jumamosi, Februari 09, 2019
Leo ni Jumamosi tarehe 3 Mfunguo Tisa Jamad al-Thani 1440 Hijria sawa na tarehe 9 Februari 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1429 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alikufa shahidi Bibi Fatima al-Zahra, binti mtukufu wa Mtume wetu Muhammad (saw) na mke wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Alizaliwa miaka mitano baada ya kubaathiwa Nabii Muhammad (saw) na mtukufu huyo akampa jina la Fatima. Alipewa malezi na wazazi wake wawili yaani Bibi Khadija na Mtume wa Mwenyezi Mungu na kupata maarifa aali ya dini kutoka kwa baba yake. Bibi Fatima alifikia daraja za juu za ukamilifu wa kiroho na kimaanawi ndani ya nyumba ya Wahyi na ufunuo. Baada ya kuolewa na Imam Ali bin Abi Twalib ambaye alikuwa kielelezo halisi cha takwa na uadilifu, Bibi Fatima alikuwa na nafasi kubwa na alitoa mchango wa aina yake katika jamii ya Kiislamu. Alikuwa dhihirisho la uchamungu, ukarimu, kujitolea, subira, kujipinda katika ibada na kuwasaidia watu wote na alilea watu adhimu kama Imam Hassan na Hussein (as). ***

Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, vibaraka wa gadi ya mfalme Shah wa Iran, walivamia moja ya kambi za kikosi cha Jeshi la Anga mjini Tehran majira ya usiku, baada ya kundi la makamanda wa jeshi hilo kutangaza uungaji mkono wao kwa Mapinduzi ya Kiislamu na utiifu wao kwa Imam Ruhullah Khomeini. Baada ya kutangazwa habari hiyo, wananchi Waislamu wa Iran kutoka pembe zote za mji wa Tehran walielekea katika kambi ya kikosi cha Jeshi la Anga ili kuwasadia wanajeshi hao ambao walikuwa wakipambana na vibaraka hao wa mfalme Shah. Licha ya kutokuwa na silaha za maana wananchi hao walifanikiwa kuzima shambulio la mamluki hao na kwa utaratibu huo, hatua ya mwisho ya kuuangusha utawala wa Shah nchini Iran ikawa imeanza. ***
Miaka 33 iliyopita katika siku kama ya leo, wapiganaji shupavu wa Iran walianzisha operesheni iliyopewa jina la Walfajr 8 kwa kushambulia ngome za jeshi la utawala wa zamani wa Iraq katika eneo la kusini zaidi la mpaka wa nchi mbili hizi. Maelfu ya wapiganaji wa Iran walivuka Mto Arvand na kufanikiwa kuuteka mji wa Faw unaopatikana kusini mashariki mwa Iraq, katika siku ya kwanza ya operesheni hiyo. Operesheni hiyo ilikuwa ya ghafla na tata kwa upande wa kijeshi na iliwashangaza weledi wa masuala ya kijeshi na kisiasa ulimwenguni na utawala wa zamani wa Iraq. Operesheni ya Walfajr-8 ilitekelezwa kwa lengo la kuushinikiza utawala wa Saddam uache kuikalia kwa mabavu ardhi ya Iran na kuilipa fidia Tehran kutokana na hasara na maafa yaliyosababishwa na uvamizi wa Iraq. ***
Na siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, baada ya Chama cha Wokovu wa Kiislamu cha Algeria (FIS) kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge, wanajeshi waliokuwa wakitawala nchini humo, walibatilisha matokeo ya uchaguzi huo na kukipiga marufuku chama hicho, hali iliyopelekea kuzuka machafuko makubwa. Machafuko hayo yalipelekea kuuawa watu wengi nchini Algeria. ***