Ijumaa, Februari 15, 2019
Leo ni Ijumaa tarehe 9 Mfunguo Tisa Jamadithani mwaka 1440 Hijria inayosadifiana na Februari 15 mwaka 2019 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, Jeshi Jekundu la Shirikisho la Urusi ya zamani lililazimika kuondoka nchini Afghanistan baada ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa kipindi cha miaka kumi. Majeshi hayo yaliondoka baada ya kushindwa kukabiliana na mapambano ya mujahidina wa Kiislamu. Lengo la Umoja wa Sovieti la kuivamia na kuikalia kwa mabavu Afghanistan mwaka 1979, lilikuwa kuizatiti na kuipa nguvu serikali kibaraka ya Kabul iliyokuwa ikiungwa mkono na Moscow na kueneza satua yake upande wa maeneo ya kusini mwa Asia. Hatua hiyo iliyoyatumbukiza hatarini maslahi ya Marekani, ilikabiliwa na radiamali kali ya Washington ambapo Ikulu ya Marekani (White House) ilianzisha operesheni za kuyatoa majeshi ya Umoja wa Sovieti huko Afghanistan. Hatimaye baada ya miaka 10 wananchi wa Afghanistan wakisaidiwa na Mujahidina walifanikiwa kuhitimisha uvamizi huo na kuyafukuza majeshi ya Urusi katika ardhi yao.
Miaka 237 iliyopita vilianza vita vya majini kati ya Ufaransa na Uingereza katika pwani ya India. Vita hivyo vilivyoendelea kwa muda wa miezi saba, vilikuwa mlolongo wa vita kati ya nchi mbili hizo vilivyokuwa na lengo la kuikoloni India na kupora utajiri wake. Ijapokuwa Ufaransa ilishinda vita hivyo, lakini nchi hiyo haikuweza kurejea India na kuikoloni nchi hiyo na badala yake Uingereza ilibaki na kuendelea kuwa mkoloni mkuu huko Bara Hindi.
Siku kama ya leo miaka 455 iliyopita alizaliwa msomi mashuhuri, mnajimu na mtaalamu wa fizikia wa Italia, Galileo Galilei katika mji wa Pisa. Alisoma fasihi hadi alipokuwa na umri wa miaka 19 na baadaye akajishughulisha na fizikia na hisabati. Galileo alitumia lenzi iliyovumbuliwa na msomi na mnajimu mashuhuri wa Kiislamu, Ibn Haitham kutengeneza darubini ya elimu ya nujumu kwa ajili ya kutazamia nyota na sayari. Galileo alitumia chombo hicho kuthibitisha kwamba, sayari ikiwemo ya ardhi, zinazunguka jua. Utafiti huo wa Galileo Galilei ulithibitisha nadharia ya msomi Muislamu wa Iran ambaye karne kadhaa kabla yake alithibitisha kwamba, ardhi inazunguka jua. Baada ya kusambaa nadharia hiyo ya Galileo kuhusu mzunguko wa ardhi na sayari nyingine kando ya jua, kanisa la Roma lilimtuhumu kuwa kafiri na akahukumiwa kifungo cha maisha cha nyumbani. Baadaye msomi huyo alilazimika kukanusha nadharia hiyo kwa ajili ya kuokoa maisha yake.
Na katika siku kama ya leo miaka 741 iliyopita yaani tarehe 9 Mfunguo Tisa Jamadithani mwaka 699 Hijria, Ibn Farah Eshbily malenga, mshairi na mtaalamu wa elimu ya hadithi katika karne ya saba Hijria alifariki dunia. Alizaliwa katika Andalusia ya zamani ambayo leo hii ni eneo la kusini mwa Uhispania. Alitiwa mbaroni baada ya majeshi ya Uhispania kuushambulia mji huo. Hata hivyo baada ya kushikiliwa kwa muda, alitoroka na kukimbilia nchini Misri. Akiwa nchini Misri, Ibn Farah Eshbily alifanikiwa kuchota elimu na maarifa kwa maulama mashuhuri wa zama hizo mjini Cairo. Baada ya muda alielekea Damascus huko Syria na kujiendeleza zaidi kielimu. Alimu na msomi huyu wa Kiislamu ameacha athari nyingi za kielimu hususan katika uga wa mashairi.
