Jumamosi, 16 Februari, 2019
Leo ni Jumamosi tarehe 10 Mfunguo Tisa Jamadithani 1440 Hijria sawa na tarehe 16 Februari 2019 Miladia.
Siku kama ya leo ya tarehe 10 Jamadithani mwaka 627 Hijria yaani miaka 813 iliyopita alifariki dunia mwanafasihi mtajika, arif na malenga mashuhuri wa Kiislamu na Kiirani Sheikh Fariduddin Attar Naishaburi. Attar Naishaburi alizaliwa mwaka 513 Hijria na baada ya kufariki dunia baba yake ambaye alikuwa muuza dawa, aliendeleza kazi hiyo ya baba na kupata maarifa mengi kuhusu elimu ya tiba. Katika kipindi hicho alipatwa na mabadiliko makubwa na kuanza safari ya ndani ya nafsi na kutakasa roho. Alifanya safari katika maeneo mengi ya ulimwengu wa Kiislamu na kupata elimu ya irfani kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo. Baadhi ya nukuu za kihistoria zinasema msomi huyo mkubwa wa Kiislamu aliuawa shahidi katika mashambulizi ya Mogul. Attar Naishaburi ameandika tajiriba na uzoefu wake wa kiirfani katika kalibu ya mashairi na nathari. Miongoni mwa vitabu vya arifu huyo mkubwa Muirani ni "Tadhkiratul Auliyaa" na "Mantwiqut Twair." ***

Miaka 101 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Februari 1918, Lithuania ilijitangazia uhuru wake baada ya kudhoofika Russia kutokana na kushiriki kwake katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kutokea mapinduzi nchini humo mwaka 1917. Pamoja na hayo, Moscow iliendeleza mipango yake ya kuiunganisha tena Lithuania na ardhi za Umoja wa Kisovieti, ambapo mwaka 1940 ilifanikiwa kufikia lengo hilo. Ujerumani ya Kinazi iliikalia kwa mabavu Lithuania kwa zaidi ya miaka mitatu katika kipindi cha Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. ***
Katika siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, kwa mara ya kwanza kura ya veto ilitumiwa na mjumbe wa Urusi ya zamani katika Umoja wa Mataifa. Siku hiyo mwakilishi wa Urusi, alipinga moja ya mapendekezo ya Baraza la Usalama na hivyo kutumia kwa mara ya kwanza haki ya veto. Haki ya kura ya veto inayolalamikiwa, inamilikiwa na nchi tano tu wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambazo ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, China na Russia. Mpango wa kutumia veto ulipasishwa na Marekani, Uingereza na Urusi ya zamani katika mkutano wa Yalta wa mwaka 1945. Tangu wakati huo kumekuwepo malalamiko ya kupinga kupewa nchi hizo tu kura hiyo ya veto hasa kwa kuzingatia kuwa, baadhi ya nchi hizo zimekuwa zikiitumia haki hiyo kwa malengo ya kisiasa. ***

Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 27 Bahman, idadi kadhaa ya viongozi wa utawala wa Kipahlavi walinyongwa baada ya kupatikana na hatia ya khiyana na kutenda jinai dhidi ya wananchi wa Iran. Licha ya kuwa kwa mtazamo wa wananchi Waislamu wa Iran jinai za viongozi hao wa utawala dhalimu wa Shah zilikuwa wazi na bayana, lakini kwa amri ya Imam Khomeini MA mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu kuliundwa Mahakama ya Mapinduzi ya Kiislamu na kushughulikia kesi za viongozi hao waliokuwa wametiwa mbaroni na vikosi vya wananchi. ***
Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, Sheikh Raghib Harb, Imam wa Swala ya Ijumaa katika kijiji cha Jibchit cha kusini mwa Lebanon na mmoja wa waasisi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon dhidi ya utawala ghasibu wa Israel aliuawa shahidi na vikosi vya utawala huo vamizi. Sheikh Raghib alikuwa mmoja wa wanazuoni wanamapambano amilifu kusini mwa Lebanon kabla ya kuuawa kwake shahidi aliwahi kutiwa mbaroni na makachero wa Wazayuni wavamizi kutokana na mapambano na wito wake wa kuwataka wananchi wasimame na kupambana na Wazayuni. Wakati wa kuzikwa mwili wa shahidi Sheikh Raghib Harb, kulitokea mapigano makali baina ya vijana wa kitongoji cha Jibchit na wanajeshi wa Israel ambayo yalipelekea kuuawa na kujeruhiwa idadi kadhaa ya Waislamu madhulumu wa Lebanon. ***
Na siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, aliuawa shahidi katika shambulio la ndege za utawala wa Kizayuni wa Israel Sayyid Abbas Musawi, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, huko kusini mwa nchi hiyo. Shambulio hilo lilipelekea kuuawa pia watu kadhaa waliokuwa wameandamana naye akiwemo mke na mwanawe mdogo, pamoja na wasaidizi wake watatu. Shambulio hilo lilitokea wakati Sayyid Abbas Musawi alipokuwa akirejea nyumbani kutoka kwenye kumbukumbu za kuuawa shahidi Sheikh Raghib Harb aliyeuliwa na maafisa wa utawala huo miaka michache iliyopita kabla ya hapo. Sheikh Raghib Harb alikuwa mwasisi wa harakati za mapambano huko kusini mwa Lebanon. Hujuma hiyo iliamsha hasira kubwa za Waislamu kote ulimwenguni dhidi ya Israel. Hata hivyo madola ya Magharibi yanayodai kutetea haki za binadamu, si tu kwamba, hayakulaani jinai hiyo bali pia yalijaribu kuihalalisha. Baada ya kuuawa shahidi Sayyid Abbas Musawi, Sayyid Hassan Nasrullah alichukua jukumu la kuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah, na kutoa pigo kwa Israel mwaka 2000, baada ya kuyafukuza kwa madhila majeshi ya utawala huo katika ardhi za kusini mwa Lebanon.