Jumapili, tarehe 17 Februari, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 11 Mfunguo Tisa Jamadith-Thani 1440 Hijria, mwafaka na tarehe 17 Februari 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1042 iliyopita, yaani tarehe 11 Jamadith-Thani mwaka 398 Hijiria na kwa mujibu wa baadhi ya marejeo ya kihistoria, alifariki dunia Badiuz-Zaman Hamadani, mtaalamu wa fasihi, mwandishi na malenga wa Iran. Badiuz-Zaman alizaliwa mjini Hamadan, magharibi mwa Iran na baadaye akapata umashuhuri wa jina la Fadhil Hamadani. Badiuz-Zaman Hamadani alikuwa na ujuzi maalumu katika elimu ya lugha na mashairi ya Kiarabu ambapo alikuwa na uwezo mkubwa katika uwanja huo. Miongoni mwa athari za malenga na mwandishi huyo wa Iran ni pamoja na diwani ya mashairi inayoitwa ‘Rasaailu Badiz-Zamaan.’
Siku kama ya leo miaka 786 iliyopita, alifariki dunia Ebn-e Shaar, mtaalamu wa fasihi na mwanahistoria wa Kiarabu. Alizaliwa mjini Mosul, moja ya miji ya kaskazini mwa Iraq na baada ya kuhitimu masomo ya msingi alianza kujifunza mashairi. Mtaalamu huyo mkubwa wa fasihi aliandika historia ya wasomi wa fasihi na malenga wa zama zake huku akifanya safari katika maeneo tofauti na juhudi kubwa katika uwanja huo ambapo alifanikiwa kuandika kitabu alichokipa jina la ‘Uquudul-Jamaan.’
Siku kama ya leo miaka 304 iliyopita alifariki dunia Antoine Galland, mtaalamu maarufu wa masuala ya eneo la Mashariki ya Kati. Galland alizaliwa tarehe 4 Aprili 1646 Miladia katika viunga vya miji ya kaskazini mashariki mwa Ufaransa. Antoine Galland alilazimika kukatiza masomo yake baada ya muda mfupi kutokana na umasikini na hivyo akaanza kujishughulisha na kazi. Baadaye alielekea mjini Paris, mji mkuu wa nchi hiyo na baada ya kujifundisha lugha ya Kituruki, alipata ajira ya kuwa sekretari wa balozi wa Ufaransa katika masuala ya utawala wa Othmania na hivyo akaelekea mjini Constantinople. Akiwa huko aliendelea kufanya utafiti kuhusiana na eneo la Mashariki ya Kati sambamba na kujifundisha lugha ya Kigiriki na kufanya uchunguzi kuhusiana na sarafu za Ugiriki. Baada ya Antoine Galland kurejea Ufaransa alitokea kuwa mmoja wa wataalamu wakubwa wa Mashariki ya Kati ambapo pia alibeba sarafu nyingi za Ugiriki na kuziweka katika majengo ya makumbusho ya Ufaransa. Mwaka 1701 Miladia alijiunga na kamisheni ya jumuiya ya vitabu vya historia ambapo alipata nafasi ya kuandika vitabu vyake. Vitabu vya Galland vilipata soko kubwa barani Ulaya.
Siku kama ya leo miaka 210 iliyopita, vilimalizika vita vya umwagaji damu vya Zaragoza vilivyopiganwa kati ya wanajeshi wa Ufaransa na wale wa Uhispania. Vita hivyo vilimalizika kwa Ufaransa kupata ushindi na kuukalia kwa mabavu mji wa Zaragoza ulioko mashariki mwa Uhispania. Vita hivyo vilianza Novemba 15 mwaka 1808, kufuatia uvamizi wa jeshi la Napoleon Bonaparte.
Siku kama ya leo miaka 192 iliyopita, alifariki dunia Johann Heinrich Pestalozzi, msomi wa Uswisi na mmoja wa walimu mashuhuri. Pestalozzi alikuwa mjuzi wa elimu nyingi hasa hisabati na tiba na alikuwa akizungumza lugha kadhaa za kimataifa. Msomi huyo wa Uswisi alikuwa na mtindo wake makhsusi wa kufundisha ambapo aliweza kutoa mafunzo ya masuala mbalimbali kwa watoto kwa wakati mmoja.
Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Mirza Ali Akbar Nuqani, faqihi na mtaalamu wa theolojia wa Iran. Alizaliwa mwaka 1261 Hijiria Shamsia mjini Mash’had, kaskazini mashariki mwa Iran. Baada ya kuhitimu masomo ya msingi alianza kujifunza elimu ya fasihi, fiqihi (sheria za Kiislamu) na usulu fiqhi kwa walimu wakubwa wa zama zake. Akiwa na umri wa miaka 26 alielekea mjini Najaf Iraq, kwa ajili ya kujiendeleza kielimu katika hawza ya elimu ya mji huo ambapo akiwa mjini hapo alipata kusoma kwa maulama wakubwa na kukwea daraja za elimu. Msomi huyo mkubwa aliyekuwa pia malenga hodari aliandika vitabu kadhaa kama vile ‘Taaliiqaati Alaa Sharhi Nahjul-Balaaghah’ ‘Se Maqaaleh Nuuqaan’ na ‘Raddu Aqaaid Maaddiyyun.’
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, mazungumzo ya amani ya pande tatu kati ya Iran, utawala wa Baath wa Iraq na Umoja wa Mataifa yalianza huko New York Marekani. Katika hali ambayo mazungumzo hayo hayakuwa na natija ya maana na hata kulikuwa na uwezekano wa kuvunjuika, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa imethibitisha nia yake njema kwa jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa hususan kwa Katibu Mkuu wake.
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, mkataba wa kuasisiwa Jumuiya ya Magharibi ya Kiarabu ulitiwa saini huko Morocco kwa kuhudhuriwa na Marais wa nchi za kaskazini mwa Afrika. Nchi washiriki wa mkataba huo zilikuwa Libya, Mauritania, Algeria, Tunisia na mwenyeji Morocco. Lengo la kuasisiwa jumuiya hiyo lilikuwa ni kuanzisha taasisi ya kieneo kwa lengo la kupanua ushirikiano baina ya nchi wanachama na kupunguza uteghemezi kwa nchi za Magharibi. Hata hivyo, hitilafu za kimitazamo za baadhi ya wanachama wa Jumuiya ya Magharibi ya Kiarabu kama Algeria na Morocco kuhusiana na suala la Sahara Magharibi na vilevile mizozo ya mipaka na kisiasa zilizuia kufikiwa malengo ya kuasisiwa jumuiya hiyo.
Sikun kama ya leo miaka 8 iliyopita, ilianza harakati ya wananchi wa Libya dhidi ya utawala wa Kanali Mummar Gadafi. Libya ilikuwa nchi ya tatu kukumbwa na wimbi la mwamko wa Kiislamu na kuziangusha tawala kadhaa za kidikteta. Baada ya kuondolewa madarakani serikali ya Zainul Abidin bin Ali nchini Tunisia na dikteta wa zamani wa Misri, Husni Mubarak, wananchi wa Libya pia walianzisha harakati kubwa dhidi ya Kanali Muammar Gaddafi. Awali Gaddafi alidhani kwamba angeweza kuzima harakati hiyo ya wananchi kwa kutumia jeshi na vyombo vya usalama na kwa msingi huo alianza kutumia mkono wa chuma na kuua wananchi wengi waliokuwa wakiandamana. Wanachama wa shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO pia walidandia mawimbi ya harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Libya na kushambulia vituo vya kijeshi na viwanda vya Libya. Hatimaye Kanali Muammar Gaddafi aliyeitawala Libya kwa kipindi cha miongoni minne aliondolewa madarakani na kuuawa kwa kudhalilishwa na kisha akazikwa sehemu isiyojulikana.
Siku kama ya leo miaka 8 iliyopita, utawala kandamizi wa Aal Khalifa nchini Bahrain uliyageuza maandamano ya amani ya wananchi katika medani ya Lulu kuwa dimbwi la damu. Katika nchi hiyo ambayo nayo ilikuwa imetumbukia katika mkondo wa harakati ya mwamko wa Kiislamu katika nchi za Kiarabu, wananchi wakiwa na lengo la kupigania haki zao za kimsingi na za kiraia walikuwa wameanza kufanya maandamano ya amani dhidi ya utawala wa Manama. Katika miaka sita iliyopita licha ya kutiwa mbaroni wanaharakti wengi wapigania uhuru nchini Bahrain, wananchi hao hawajasalimu amri na kuachana na harakati yao na wamekuwa wakiandelea kudai matakwa yao yatekelezwe na utawala wa Aal Khalifa wa Bahrain.

Na siku kama ya leo miaka mitatu iliyopita Mohamed Hassanein Heikal mwandishi na mwanafikra mtajika wa Misri alifariki dunia. Mohamed Heikal alizaliwa Septemba 23 1923 katika jimbo la Qalyubia huko Misri. Alikuwa mhariri mkuu wa gazeti la al-Ahram la Misri kwa muda wa miaka 17. Heikal alikuwa muasisi wa kituo mashuhuri cha utafiti wa kisiasa na kiistratejia cha al-Ahram.