Feb 20, 2019 23:30 UTC
  • Alkhamisi tarehe 21 Februari 2019

Leo ni Alkhamisi tarehe 15 Jumadithani 1440 Hijria sawa na 21 Februari 2019.

Siku kama ya leo miaka 1403 iliyopita yaani tarehe 15 Jumadi Thani mwaka 36 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, vilianza vita vya Jamal, baina ya jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kundi la waasi waliozusha vurugu na fitina. Katika vita hivyo, jeshi la Kiislamu lililishinda kundi hilo ambalo lilianzisha uasi baada ya kushindwa kustahamili uadilifu wa Imam Ali, na hivyo kuamua kuvunja baia na kiapo chao cha utiifu. Viongozi wa kundi hilo ambalo lilijulikana kwa jina la Nakithina yaani wavunja ahadi, walikuwa Twalha na Zubair, ambapo waliamua kukusanya jeshi kubwa na kulichochea kwa matarajio ya kufikia malengo batili ya kutaka kutwaa utawala kwa nguvu. Imam Ali (as) alijiepusha sana kuanza vita dhidi ya kundi hilo la waasi na kuanzisha mazungumzo na viongozi wake. Hata hivyo vinara wa kundi hilo waliokuwa wamempa Imam Ali bin Abi Twalib mkono wa utiifu huko Madina na baadaye kukengeuka, walianza vita dhidi ya jeshi la Uislamu na hatimaye kundi hilo la waasi lilishindwa vibaya na vinara wake wengi wakauliwa.

Vita vya Ngamia

Tarehe 15 Jumadi Thani mwaka 771 katika siku kama ya leo miaka 668 iliyopita, alifariki dunia Muhammad bin Hassan Hilli, maarufu kwa jina la 'Fakhrul Muhaqqiqiin', faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu. Mwanachuoni huyo alizaliwa mwaka 682 Hijria na kupata elimu ya kidini kwa mzazi wake, Allamah Hilli na wanachuoni wengine wa zama zake. Fakhrul Muhaqqiqiin ameacha vitabu vingi na miongoni mwavyo ni Manbau'l Asrar na Tahswilul Najah.

Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita, alizaliwa Reinhart Dozy, mtaalamu wa masuala ya mashariki mwa dunia aliyekuwa raia wa Uholanzi. Dozy alizamili katika fani za historia na lugha huku akifikia daraja ya PHD katika fani ya fasihi akiwa na umri wa miaka 24. Reinhart Dozy alipendelea sana kusomea tamaduni za Kiislamu ambapo mbali na kuwa mahiri katika lugha ya Kiingereza, Kifaransa na Kijerumani, alikuwa pia mtaalamu katika lugha ya Kiarabu. Msomi huyo wa Uholanzi alifanya utafiti mwingi wa tamaduni za Kiarabu na historia ya Kiislamu, hususan Waislamu wa Andalusia, kusini mwa Uhispania. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu cha 'Historia ya kisiasa na tamaduni za Kiarabu katika Andalusia' 'Historia ya Uislamu kuanzia mwanzo wake hadi katikati ya karne ya 19' na 'Tamaduni za mavazi ya Kiislamu.' Reinhart Dozy alifariki dunia mwaka 1883.

Reinhart Dozy

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, inayosadifiana na 21 Februari 1916 vilianza vita vikubwa vya umwagikaji damu vilivyojulikana kwa jina la 'Verdun' kati ya Ujerumani na Ufaransa. Vita hivyo vilivyoendelea kwa muda wa miezi kumi vilimalizika kwa kushindwa vikosi vya jeshi la Ujerumani na wanajeshi karibu milioni moja wa nchi hizo mbili kuuawa. Tukio hilo ni miongoni mwa sababu za kushindwa Ujerumani kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia.

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, wananchi wa Misri na Syria walishiriki kwenye kura ya maoni ya kuunganisha nchi mbili hizo chini ya Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu. Wananchi wa nchi hizo mbili walimchagua Jamal Abdul-Nasser kiongozi wa wakati huo wa Misri, kuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu. Baada ya kupita miezi kadhaa, Yemen nayo ilijiunga kwenye muungano huo. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa zaidi ya miaka mitatu, kwani Syria ilitangaza kujitoa kwenye muungano huo kutokana na kutoridhishwa na uongozi wa Jamal Abdul-Nasser.

Na siku kama ya leo 53 iliyopita, Malcolm X, Mmarekani mweusi aliuawa baada ya kushambuliwa na magaidi nchini humo. Malcolm X alizaliwa mwaka 1925, na wakati alipokuwa kwenye rika la ujana alifahamiana na makundi ya vijana wa Kiislamu na hatimaye kusilimu. Itikadi za mwanaharakati huyo wa Kiislamu ziliwachukiza watawala wa Marekani na makundi ya ubaguzi wa rangi nchini humo. Malcolm X aliuawa akihutubia mkutano. Alikuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa, Wamarekani weusi ambao wanakandamizwa na kubaguliwa na serikali ya Marekani wanaweza kujipatia uhuru na uadilifu chini ya mwavuli wa utawala wa Kiislamu.

Malcolm X