Jumanne tarehe 19 Februari 2019
Leo ni Jumanne tarehe 13 Jamadithani 1440 Hijria sawa na Februari 19 mwaka 2019.
Tarehe 13 Jumadithani mwaka 64 Hijria kwa mujibu wa nukuu mashuhuri zaidi ya wanahistoria, alifariki dunia Fatima bint Huzam al Kulabiyya, maarufu kwa laqabu ya Ummul Banin, mke mwema na mcha Mungu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Wanahistoria wamehitilafiana juu ya siku aliyozaliwa na baadhi wanasema alizaliwa mwaka wa 5 baada ya Hijra ya Mtume (saw). Imam Ali bin Abi Twalib alimuoa bibi huyu mwema baada ya kufariki dunia Bibi Fatima Zahra (as). Ummul Banin anatoka katika kizazi cha mashujaa wakubwa wanaopigiwa mfano baina ya Waarabu. Baada ya kuolewa, mtukufu huyo alimuomba Imam Ali ampe laqabu ambayo atakuwa akiitumia kumwitia badala ya jina lake la Fatima ambalo alichelea kwamba, litakuwa likiwakumbusha wajukuu wa Mtume mama yao, yaani Fatimatu Zahraa (as). Aliwapenda sana Ahlul Bait wa Mtume na historia inahadithia jinsi alivyowatuma wanae wote wanne kwenda kulinda familia ya Mtume hususan Imam Hussain katika ardhi ya Karbala. Watoto wote wanne wa Hadhrat Ummul Banin, wakitanguliwa na Abul Fadhl al Abbas, waliuawa shahidi wakiwa pamoja na kaka yao, Hussein katika medani ya Karbala. Ummul Banin alifariki dunia katika siku kama ya leo mjini Madina na kuzikwa katika makaburi ya Baqi'.

Siku kama ya leo miaka 1010 iliyopita alifariki dunia Ibn Haytham, mwanafizikia, mwanahisabati na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu katika mji wa Cairo. Ibn Haytham alizaliwa mwaka 354 Hijria katika mji wa Basra kusini mwa Iraq. Alibobea katika elimu za fizikia, tiba, falsafa na unajimu. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vya hisabati, nujumu na tiba. Moja ya vitabu vyake muhimu ni al-Manadhir ambacho kimetafsiriwa katika lugha ya Kiingereza na kinatumika katika elimu ya nujumi.
Tarehe 19 Februari miaka 546 iliyopita alizaliwa mnajimu na mwanahesabati mashuhuri wa Poland, Nicolaus Copernicus. Awali alijifunza elimu ya nujumu na baadaye tiba, na baada ya kukamilisha masomo alianza kufundisha hesabati huko Roma. Hata hivyo Copernicus aliendelea kudurusu na kufanya utafiti wa elimu ya nujumu na mwaka 1503 alivumbua nadharia ya harakati ya dunia kuzunguka jua na vilevile dunia kujizunguka yenyewe katika kila baada ya masaa 24. Nicolaus Copernicus alifariki dunia tarehe 24 Mei 1543 siku chache tu baada ya kuchapisha kitabu cha On the Revolutions of the Celestial Spheres kinachofafanua nadharia zake.
19 Februari miaka 22 iliyopita alifariki dunia Deng Xiaoping, kiongozi wa zamani wa China na mhandisi wa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa ya nchi hiyo. Katika kipindi cha uongozi wa Xiaoping China ilifanya mageuzi makubwa katika nyanja mbalimbali na alifanya marekebisho makubwa katika uchumi wa kisoshalisti wa wakati huo wa China na kuuelekeza kwenye uchumi wa soko. Wakati huo China ilifanikiwa kuingia katika nyanja mbalimbali za kimataifa na kutatua migogoro iliyokuwepo katika uhusiano wake na nchi kadhaa. Deng Xiaoping alijiuzulu mwaka 1990 kutokana na maradhi na umri wake mkubwa na hadi anafariki dunia alikuwa akihesabiwa kuwa shakhsia mkubwa zaidi wa China.
Na miaka 9 iliopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 30 Bahman 1388 Hijiria Shamsia, manowari ya kwanza ya kivita ya Iran inayojulikana kwa jina la Jamaran ilianza kufanya kazi. Jamaran ni manowari ya kijeshi yenye uwezo wa kubeba aina kadhaa za makombora ya kuhujumu meli na kutungua makombora na ndege za adui. Pia ina rada za kisasa na uwezo wa kushiriki katika vita vya kielektroniki. Meli hiyo inayoenda kwa kasi kubwa pia ina eneo la kutua helikopta. Baadhi ya teknolojia iliyotumia kutengeneza manuwari hiyo inamilikiwa na nchi kadhaa tu dunia na wataalamu wa Jamhuri ya Kiislamu wamefanikia kuvunja mzingiro huo na kuiwezesha Iran kuwa miongoni mwa nchi zenye utaalamu wa kubuni na kuzalisha teknolojia hiyo.