Feb 22, 2019 01:09 UTC
  • Ijumaa,  22 Februari, 2019

Leo ni Ijumaa tarehe 16 Jumadithani 1440 Hijria sawa na Februari 22 mwaka 2019.

Miaka 1019 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kauli za wanahistoria, alifariki dunia Ibn Darraj Qastalli mshairi na mwandishi mwashuhuri wa Andalusia. Ibn Darraj alizaliwa mwaka 347 Hijiria na alikuwa miongoni mwa washairi wakubwa wa Andalusia huko kusini mwa Uhispania ya leo. Pia alikuwa na nafasi muhimu katika kukuza mashairi ya Kiarabu mwishoni mwa karne ya 4 na mwanzoni mwa karne ya 5 Hijiria. Ibn Darraj ndiye aliyeleta mtindo mpya wa mashairi ya Kiarabu huko Andalusia na mashairi yake mbali na kuwa na thamani ya kifasihi na kisanaa pia yanahesabiwa kuwa marejeo ya kuaminika yanayoakisi matukio ya wakati huo ya Uhispania. 

Siku kama ya leo miaka 93 iliyopita inayosadifiana na tarehe 3 Isfand mwaka 1299 Hijria Shamsia, Uingereza ilitekeleza siasa zake za kikoloni kwa kufanya mapinduzi ya kijeshi nchini Iran. Njama hiyo ya mapinduzi ilipangwa na maafsia wa serikali ya Uingereza waliokuwa mjini Tehran wakishirikiana na baadhi ya maafisa usalama wa mji huo. Wafanya mapinduzi waliudhibiti mji mkuu baada ya mapigano ya muda mfupi, na Ahmad Shah Qajar akalazimika kumteua Reza Khan kuwa Kamanda Mkuu wa majeshi. Miaka minne baadaye Reza Khan ambaye alikuwa akiungwa mkono na kusaidiwa sana na Waingereza kutokana na kukanamiza harakati za ukombozi za wananchi alifanywa mfalme wa Iran hadi mwaka 1320 Hijria Shamsia, ambapo aliondolewa madarakati na Waingereza wenyewe na kupelekwa uhamishoni baada ya kuegemea upande wa Ujerumani katika Vita  Vikuu vya Pili vya Dunia.

Reza Khan

Miaka 61 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 22 Februari mwaka 1958, Abul Kalam Ahmad Azad, msomi, khatibu na mwanasiasa wa India alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 70. Abul Kalam Azad alianza harakati za kisiasa akiwa na umri wa miaka 17 na harakati zake zilikuwa  dhidi ya utawala wa kikoloni wa Uingereza kwa shabaha ya kuwazindua Waislamu wa India. Msomi huyo alifungwa gerezani mara kadhaa na wakoloni wa India, kutokana na hatua zake za kuchapisha na kutoa hotuba zenye kufichua ukandamizaji wa Uingereza. Baada ya India kupata huru, alichaguliwa kuwa mbunge na Waziri wa Elimu wa nchi hiyo.

Abul Kalam Ahmad Azad

Katika siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, wapiganaji shupavu wa Iran walianzisha operesheni ya 'Khaybar' dhidi ya majeshi ya Iraq, kwenye vita vya kulazimishwa vilivyoazishwa na utawala wa Baath wa Saddam Hussein. Katika operesheni hiyo iliyofanyika katika eneo la Hoor al Hoveyzah kusini magharibi mwa Iran, wapiganaji shupavu wa Iran walifanikiwa kuvuka maji na kukiteka kisiwa chenye utajiri mkubwa wa mafuta cha Majnoon, kilichoko karibu na mji wa Basra kusini mashariki mwa Iraq.  Mbinu tata za kijeshi zilizotumika katika oparesheni hiyo ya majini na nchi kavu ya Khaibar ziliwashangaza weledi wa masuala ya kijeshi duniani. 

Operesheni ya kijeshi ya Khaibar

Na siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, Haram mbili takatifu za Maimamu al Hadi na Hassan al Askari katika mji wa Samarra nchini Iraq, ziliharibiwa vibaya kwenye mlipuko wa mabomu kadhaa. Maimamu hao ni wajukuu wa Mtume Muhammad SAW. Kitendo cha kuharibiwa sehemu kubwa ya haram hizo, kiliwakasirisha mno Waislamu hasa wafuasi wa Ahlul Bait wa Mtume SAW. Shambulio hilo lilifanyika kwa lengo la kuzusha vita vya ndani vya kimadhehebu kati ya Waislamu wa madhehebu za Shia na Suni. Hata hivyo kuwa macho wananchi wa Iraq na viongozi wa kidini wa nchi hiyo kulisambaratisha njama hizo.

Haram ya wajukuu wa Mtume Samarra, Iraq