Feb 23, 2019 00:13 UTC
  • Jumamosi, 23 Februari, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 17 Mfunguo Tisa Jamadi Thani 1440 Hijria sawa na tarehe 23 Februari 2019.

Siku kama ya leo miaka 916 iliyopita, yaani tarehe 17 Jamadithani mwaka 524 Hijiria, alifariki dunia Bari'i Baghdadi, mwanafasihi na malenga mashuhuri wa Kiarabu. Baghdadi alizaliwa mwaka 443 Hijiria na kuanza kusomea elimu ya nahau na lugha kutoka kwa maulama wakubwa wa kipindi chake. Moja ya athari mashuhuri za Bari'i Baghdadi ni kitabu cha mashairi kilichopewa jina lake. Malenga na mshairi huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 81 hali akiwa ni kipofu. ***

Bari'i Baghdadi

Miaka 853 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitiwa saini makubaliano ya kisiasa ya Acre katika kipindi cha Vita vya Msalaba baina ya Waislamu na wapiganaji wa Kikristo. Makubaliano hayo yalitiwa saini kwa ajili ya kukabidhiwa mji wa Acre kwa Wakristo na mkabala wake kuachiliwa huru mateka wa Kiislamu wapatao 3,000. Hata hivyo na bila ya kuheshimu makubaliano hayo, Wakristo waliwaua mateka hao wa Kiislamu suala lililosababisha kuanza tena kwa Vita vya Msalaba ambavyo vilimalizika kwa kushindwa vibaya Wakristo. Mji wa Acre ulikombolewa na Waislamu katika karne ya 15 Hijiria na ukachukuliwa tena na Wamagharibi mwaka 587. ***

Salahudeen Ayubi

Siku kama ya leo miaka 220 iliyopita, Napoleon Bonaparte mfalme wa Ufaransa, alianza kuishambulia Sham, ambayo wakati huo ilikuwa ikiundwa na nchi za Syria, Jordan, Lebanon na Palestina. Mashambulio ya Bonaparte dhidi ya Misri yalifanyika kwa lengo la kutoa pigo kwa Uingereza iliyokuwa mkoloni wa Misri. Sababu ya mashambulio ya Napoleon Bonaparte dhidi ya Sham iliyokuwa sehemu ya ardhi ya utawala wa Othmania, ilikuwa ni hatua ya mfalme wa utawala wa Othmania ya kutangaza vita dhidi ya Ufaransa. Katika mashambulio hayo, na licha ya kwamba awali Bonaparte alipata ushindi, lakini baadaye alilazimika kuacha vita na kurejea kwao kutokana na uungaji mkono wa Uingereza na Urusi kwa utawala wa Othmania na kuharibika hali ya mambo ndani ya Ufaransa. ***

Napoleon Bonaparte

Katika siku kama ya leo miaka 120 iliyopita, alifariki dunia msomi wa Kiislamu Hajj Mirza Hussain Nuri. Msomi huyu mkubwa alifikia daraja ya juu katika ibada, ucha-Mungu na ukamilifu wa nafsi. Hajj Mirza Hussein alikuwa hodari katika elimu za fiqhi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani tukufu na mashairi na mwandishi aliyebobea wa vitabu. Vitabu vyake vingi vilihusu elimu za hadithi, tafsiri na ufafanuzi kuhusiana na maisha ya wasomi wa Kiislamu. Mirza Hussain Nuri alilipa umuhimu mkubwa suala la kueneza athari za Ahlul-Beiti wa Mtume (saw). Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi na miongoni mwa athari zake mashuhuri ni pamoja na kitabu cha "Mustadrakul Wasaail", "Maalimus Sabr", "Jannatul Maawa" na "Nafasur Rahman". Mirza Hussein Nuri amezikwa katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq. ***

Hajj Mirza Hussain Nuri

Siku kama ya leo miaka 39, Ayatullah Dakta Muhammad Husseini Beheshti aliteuliwa kuwa mkuu wa kwanza wa Mahakama Kuu ya Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Hatua hiyo ilichukuliwa na Imam Ruhullah Khomeini MA baada ya kupasishwa Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu na kuundwa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge. Dakta Beheshti alikuwa miongoni mwa wanafikra wakubwa na shakhsia mashuhuri wa Mapinduzi ya Kiislamu. Msomi huyo aliuawa kigaidi katika shambulizi la bomu lililotekelezwa na kundi la kigaidi la MKO mwaka 1360 Hijria Shamsia. ***

Dakta Muhammad Husseini Beheshti

Na miaka 9 iliyopita katika siku kama ya leo, Abdul-Malik Rigi kiongozi wa kundi la kigaidi la Jundullah lenye makao yake huko Pakistan, alitiwa mbaroni katika oparesheni tata ya kiintelijinsia iliyofanywa na maajenti wa Wizara ya Usalama wa Ndani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baada ya kufanya mashambulizi mengi ya kigaidi, gaidi huyo katili alikuwa safarini kuelekea nchini Kyrgyzstan akitokea Dubai, Imarati, kwenda kukutana na kufanya mazungumzo na kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani. Hata hivyo maafisa usalama wa Iran waliokuwa wakifuatilia kwa karibu nyendo zake waliweza kuitambua ndege iliyokuwa imembeba gaidi huyo na kuisubiri iingie katika anga ya Iran na hivyo kuilazimisha kutua katika uwanja wa ndege wa Bandar Abbas wa kusini mwa Iran na baadae wakamtia mbaroni kiongozi huyo wa kundi la kigaidi la Jundullah. Rubani wa ndege hiyo alifanya jitihada kubwa za kutoroka na kutoka nje ya anga ya Iran, lakini alizidiwa nguvu na maafisa usalama wa Iran, na kulazimishwa kuishusha chini ndege hiyo kabla haijaingia kwenye anga ya Imarati. Abdulmalik Rigi alifanya jinai nyingi ikiwa ni pamoja na kutega na kuripua mabomu katika maeneo ya umma nchini Iran, kuwauwa kwa umati raia pamoja na kuwateka nyara. Rigi hakuwa na huruma hata kwa watu wake wa karibu. Abdulmalik Rigi alikiri kwamba alikuwa anapata misaada ya kila namna ikiwemo ya kifedha na kisilaha kutoka kwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kama njia ya kuliwezesha kundi lake lifanye mauaji ya watu ndani ya Iran hususan katika maeneo ya kusini mashariki mwa Iran na kusababisha mizozo ya kimadhehebu katika maeneo hayo. Gaidi huyo alinyongwa tarehe 30 Khordad mwaka 1389 Hijria Shamsia sawa na tarehe 20 Juni, 2010 Milaadia yaani miezi minne baada ya kutiwa mbaroni. Kukiri huko kwa Rigi kunaonyesha wazi madai ya uwongo ya serikali ya Marekani ya eti inapambana na ugaidi.***

Abdul-Malik Rigi