Feb 27, 2019 03:27 UTC
  • Jumatano tarehe 27 Februari 2019

Leo ni Jumatano tarehe 21 Jumadithani 1440 Hijria sawa na Februari 27 mwaka 2019.

 Miaka 1056 iliyopita katika siku kama hii ya leo aliaga dunia Muhsin bin Ali Tanukhi mwandishi na mwanahistoria mashuhuri wa Kiislamu akiwa na miaka 55. Muhsin Tanukhi alikuwa na kipawa cha hali ya juu katika nyanja za mashairi na lugha ambapo aliweza kutunga mashairi mengi. Muhsin bin Ali Tanukhi katika kipindi kifupi alijifunza masomo ya dini na mengineyo ya zama hizo na baadaye akaanza kujishughulisha na kazi ya uwakili. Kitabu cha msomi huyo wa Kiislamu alichokipa jina la al-Faraj Ba'da al-Shidda ni mkusanyiko wa matukio ya kihistoria na kijamii yaliyojiri katika zama hizo ambayo aliyaandika kwa umakini mkubwa.

Tarehe 27 Februari miaka 117 iliyopita alizaliwa mwandishi wa riwaya wa Kimarekani, John Steinbeck katika jimbo la California. Alijiunga na chuo kikuu akiwa na umri wa miaka 17 na kuacha masomo kabla ya kupata shahada yake. Katika kipindi cha ujana wake alijishughulisha na kazi mbalimbali kabla ya kuchagua kazi ya uandishi. Kitabu cha kwanza cha riwaya cha mwandishi huo ni Cup of Gold akichokiandika akiwa na umri wa miaka 27. Mashaka ya kimaisha yalimtayarishia John Steinbeck mazingira mazuri ya kueleza kwa ufasaha maisha ya watu dhaifu na maskini katika jamii ya Marekani. Alikuwa hodari mno katika kueleza mandhari tofauti, matukio na hali mbalimbali. Steinbech ameandika vitabu vingi kama Of Mice and Men, Bombs Away, Travels with Charley, East of Eden, A Russian Jornal na Burning Bright.

John Steinbeck

Miaka 83 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Ivan Petrovich Pavlov, tabibu na mtaalamu mkubwa wa elimu ya biolojia wa Russia akiwa na umri wa miaka 87. Alizaliwa mwaka 1849 katika familia ya kidini na mwaka 1879 alihitimu elimu ya udaktari. Tabibu huyo alikuwa na shauku kubwa ya kufanya utafiti kuhusu miili ya wanyama inavyofanya kazi. Aidha alifanya utafiti mkubwa kuhusu mzunguko wa damu. Mwaka 1904 Pavlov alitunukiwa tuzo ya Nobel.

Na siku kama ya leo miaka 8 iliyopita, alifariki dunia Waziri Mkuu wa zamani wa Uturuki Najmuddin Erbakan akiwa na umri wa miaka 84. Baada ya kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Istanbul, Erbakan alijiunga na Chuo Kikuu cha Aachen nchini Ujerumani ambako alipata shahada ya uzamivu. Mwaka 1969 Najmuddin Erbakan aliingia katika uwanja wa siasa na kuchaguliwa kuwa mbunge. Mwaka 1987 aliongoza chama chenye mielekeo ya Kiislamu cha Refah ambacho kilipata viti vingi vya bunge na kumteuwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 1996. Tukio hilo liliwakasirisha mno wanasiasa wa kilaiki wa Uturuki, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. Serikali ya Erbakan ilipigwa vita na jeshi la Uturuki na miezi 10 baadaye chama cha Refah kilivunjwa na wanajeshi, na mwanasiasa huyo akapigwa marufuku kujishughulisha na masuala ya kisiasa kwa kipindi cha miaka 5. Profesa Najmuddin Erbakan anatambuliwa kuwa baba wa harakati ya Kiislamu ya Uturuki. 

Najmuddin Erbakan