Jumapili, tarehe 3 Machi, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 25 Jamadith Thani 1440 Hijria, inayosadifiana na tarehe 3 Machi 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 316 iliyopita alifariki dunia Robert Hooke, mwanasayansi wa Uiingereza. Hooke alizaliwa mwaka 1635 kusini mwa nchi hiyo. Alifanya tafiti mbalimbali katika sayansi ya fizikia, na kutoa mchango mkubwa katika mapinduzi ya sayansi kupitia kazi zake za majaribio na nadharia. Hooke kwa mara ya kwanza aliweza kutumia darubini kutazama chembe ndogo kabisa ya kiumbe hai na kuipa jina la seli. Mwanasayansi huyo wa Uingereza pia alivumbua vifaa kadhaa katika taaluma ya hali ya hewa.
Siku kama ya leo miaka 141 iliyopita, utawala wa Othmaniya na Russia zilisaini mkataba katika eneo lilopewa jina la mkataba huo yaani San Stefano. Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya utawala wa Othmaniya kushindwa na Urusi katika vita. Urusi iliuvamia utawala huo kutokana na uchu wake wa kutaka kuzidhibiti ardhi zilizokuwa chini ya himaya ya Othmaniya katika eneo la Balkan.
Siku kama ya leo miaka 131 iliyopita yaani tarehe 25 Jamadith Thani 1309 Hijiria, hukumu ya kuharamisha tumbaku ilifutwa na Ayatullah Mirza Bozorg Shirazi. Baada ya kufariki dunia Sheikh Mortaza Ansari, mmoja wa maulama wakubwa wa Kishia, wanafunzi na wasomi wakubwa wa Kishia walimtangaza Mirza Shirazi kuwa marjaa wa madhehebu hiyo. Moja ya mambo makubwa aliyoyafanya ilikuwa ni kupambana na ukoloni wa Uingereza uliokuwa unajipenyejeza kupitia tumbaku. Kutokana na hali hiyo Sayyid Mirza Bozorg Shirazi alimtumia ujumbe Mfalme Naser al-Din Shah Qajar akimueleza juu ya madhara makubwa ya kuifungulia milango Uingereza kupitia ushawishi wa tumbaku, hata hivyo ujumbe huo haukuwa na taathira kwa mfalme huyo. Ni kwa ajili hiyo na katika kuuokoa Uislamu na Waislamu na kadhalika kuilinda Iran kutokana na shari ya maadui, akatoa fatwa ya kihistoria ambayo iliharamisha matumizi ya tumbaku nchini. Baada ya fatwa hiyo Waislamu walifunga maduka yote ya kuuzia sigara sambamba na kukusanywa makatoni yake na kutupwa. Kufuatia hali hiyo Mfalme Naser al-Din Shah Qajar alilazimika kufuta mkataba wa tumbaku na Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita alifariki dunia Bi. Kaukab Pur Ranjbar, mwalimu mkubwa wa Qur'an Tukufu. Kaukab Pur Ranjbar alizaliwa mwaka 1282 Hijiria Shamsia mjini Shiraz ambapo akiwa na umri wa miaka 16 alianza kukusanya nyaraka za namna ya kufundisha elimu za Kiislamu. Baada ya kuhitimu elimu ya msingi na kujifunza masomo ya Uislamu, alijishughulisha na kazi ya ualimu wa masomo ya dini huku akianza kuhakiki na kusahihisha chapa za Qur'ani za nchini Pakistan, India na nchi nyingine. Kadhalika Bi. Kaukab Pur Ranjbar mbali na kupitia maandishi ya kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu na kuwa na uwezo mkubwa wa ufahamu wa lugha ya Kiarabu, pia alifanya juhudi kubwa za kufundisha Qur'ani kwa hatua nyepesi na ngumu. Alipofikisha umri wa miaka 27 alipatwa na maradhi ya upofu lakini akapona maradhi hayo baada ya kumuona Bibi Fatwimat Zahra (as) ndotoni na hivyo akayatolea wakfu maisha yake yote kwa ajili ya Qur'ani. Kwa miaka 46 alijipinda sana katika kazi hiyo sambamba na kuasisi vituo tofauti vya kidini ambavyo baadhi vilinasibishwa kwake. Aidha kuanzia mwaka 1338 hadi 1363 aliandika kitabu cha juzuu sita kinachotoa mwongozo wa ufundishaji wa Qur'ani Tukufu kwa njia nyepesi. Aidha kitabu cha 'Mazungumzo ya Hassan na Hussein', ni kati ya athari za msomi huyo wa kike wa Iran. 'Bi. Kaukab Pur Ranjbar alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 88.

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita ilifanyika kura ya maoni kwa ajili ya uhuru na kujitawala Jamhuri ya Bosnia Herzegovina. Kura hiyo ya maoni iliungwa mkono na karibu asilimia 100 ya wananchi walioshiriki katika zoezi hilo na kupelekea nchi hiyo kujitenga na Yugoslavia, baada ya Slovenia na Croatia kufanya hivyo. Jamhuri ya Bosnia Herzegovina ina ukubwa wa kilomita mraba karibu 51,129 na inapakana na Croatia kwa upande wa kaskazini na magharibi, Serbia upande wa mashariki na Jamhuri ya Montenegro upande wa kusini mashariki. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwaka 1991, asilimia 44 ya jamii ya nchi hiyo ni Waislamu, jamii ambayo inaunda kundi kubwa zaidi la kidini katika jamhuri hiyo ya eneo la Balkan.
Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, Wahindu wenye misimamo mikali walifanya mauaji makubwa dhidi ya Waislamu katika jimbo la Gujarat nchini India. Serikali ya India ilitangaza kuwa, Waislamu 790 waliuawa kwa umati katika mauaji hayo, lakini vyombo vingine huru vilisema kuwa, idadi ya Waislamu waliouawa ilikuwa ni zaidi ya 2000. Kisingizio kilichotumiwa na Wahindu kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waislamu wa Gujarat hususan katika mji wa Ahmadabad ni moto uliotokea katika gari moshi lililokuwa limebeba Wahindu lakini baadaye ilibainika kuwa, Waislamu hawakuhusika kwa njia yoyote na tukio hilo. Katika mauaji hayo polisi na maafisa wa jimbo la Gujarat walishirikiana na Wahindu katika mauaji hayo dhidi ya Waislamu.