Mar 03, 2019 23:08 UTC
  • Jumatatu tarehe 4 Machi 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 26 Jumadithani 1440 Hijria sawa na Machi 4 mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 1429 iliyopita vita vya Dhatus Salasil vilimalizika kwa Waislamu kujipatia ushindi. Vita hivyo vilianza baada habari kusambaa kuwa kikundi cha washirikina kilitaka kushambulia mji wa Madina. Baada ya habari hiyo kumfikia Mtume Mtukufu (saw), aliwaamuru baadhi ya Waislamu waenda kukabiliana na washirikina hao wakiongozwa na kamanda mmoja aliyetoka upande wa Muhajirina. Hata hivyo baada ya kujua uwezo mkubwa waliokuwa nao maadui, kundi hilo la Waislamu lilirejea. Mtume alimtuma kamanda mwingine lakini naye pia alirejea na ndipo Mtume Mtukufu (s.a.w) alipomteua Ali bin Abi Twalib (a.s) aongoze Waislamu katika mapigano hayo. Imam Ali (as) aliwashambulia maadui kwa umahiri mkubwa na kurejea Madina na ushindi.

Siku kama ya leo miaka 171 iliyopita, yalianza mapambano ya wapigania uhuru wa Hungary dhidi ya serikali ya Austria. Siasa za kibeberu za Klemens Metternich, Kansela wa wakati huo wa Austria zilisababisha mapinduzi mwaka 1848 katika ardhi zisizo za Ujerumani zilizokuwa chini ya himaya ya Austria, ikiwemo Hungary. Uasi wa wananchi wa Hungary ulioibuka kutokana na dhulma ya Waaustria, ulienea kwa kasi kote nchini humo. Licha ya kutishiwa na serikali kuu, wanamapinduzi walitangaza nchi hiyo kuwa jamhuri tarehe 4 mwezi Aprili mwaka 1849 baada ya kushtadi harakati zao huko Hungary. Hata hivyo kwa msaada wa utawala wa Tsar wa Urusi, ufalme wa Austria uliyakandamiza mapinduzi hayo na kuwanyonga viongozi wake.

Tarehe 4 machi miaka 196 iliyopita, vikosi vya jeshi la Ugiriki vilifanya mauaji makubwa dhidi ya Waislamu wa ufalme wa Othmania kwa kuwaua kwa halaiki Waislamu elfu 12 katika mji wa Tripolitsa. Makundi ya Wagiriki waliokuwa wakiungwa mkono na nchi kadhaa za Ulaya, yaliungana na kutekeleza mauaji hayo katika muongo wa mwanzoni mwa karne ya 19, yaani mwaka 1822. Kufuatia mauaji hayo mwezi Novemba mwaka 1824 majeshi ya Kiislamu yaliamua kulipiza kisasi dhidi ya Wagiriki.