Mar 06, 2019 05:18 UTC
  • Jumatano tarehe 6 Machi 2019

Leo ni Jumatano tarehe 28 Jumadithani 1440 Hijria sawa na tarehe 6 Machi 2019.

Miaka 850 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia katika mji mkuu wa Misri, Cairo Abul Qassim Shatibi, alimu na qarii mashuhuri wa Qur'ani ambaye ni mashuhuri kwa lakabu ya Imam al-Qurra. Alizaliwa mwaka 538 Hijria ambapo mbali na elimu ya usomaji Qur'ani, alikuwa amebobea pia katika elimu ya tajwidi, Tafsiri ya Qur'ani, hadithi, nahau, lugha na elimu  nyingine. Abul Qassim Shatibi ameacha athari nyingine katika nyuga mbalimbali ambapo Qasidat al-Shatibiyah ni moja tu ya vitabu vyake mashuhuri, kitabu ambacho kinazungumzia masuala jumla yanayohusiana na elimu ya tajwidi na kitabu hiki kimechapishwa mara chungu nzima katika nchi mbalimbali. 

Siku kama ya leo miaka 544 iliyopita, alizaliwa mjini Caprese Michelangelo, mchoraji na mhunzi wa masanamu wa Italia. Licha ya upinzani mkubwa wa baba yake juu ya fani hiyo ya uhunzi na uchoraji, Michelangelo alijiendeleza katika fani hiyo na kupata umahiri mkubwa. Uhodari wake ulionekana miaka michache baadaye, ambapo alifanikiwa kuchonga masanamu mengi ya kuvutia. Michelangelo, alitokea kuwa mhunzi hodari wa karne ya 16 Miladia. Mwaka 1505, wakazi wa mji wa Roma walimwalika Michelangelo, ili aende kuwachongea sanamu la papa kwenye kaburi lake. Baadaye papa wa wakati huo, alimtaka mtaalamu huyo kupamba paa la kanisa la Sistine, kazi iliyoanza hapo mwaka 1508 na kumalizika mwaka 1512 Miladia. Mbali na hayo, Michelangelo alichonga sanamu kubwa la Nabii Issa (as), ambalo lipo mjini Roma hadi leo.

Michelangelo

Siku kama ya leo miaka 467 iliyopita yaani tarehe 6 Machi 1552, vilimalizika vita vikubwa vya pili kati ya Wakatoliki na Waprotestanti wa Ujerumani, kwa kushindwa Waprotestanti. Vita hivyo vilipiganwa nchini Austria. Sababu ya vita hivyo zilikuwa za kimadhehebu na vilianza baada ya Martin Luther kuanzisha madhehebu ya Kiprotestanti katika dini ya Kikristo.

Miaka 119 iliyopita katika siku kama hii ya leo aliaga dunia mvumbuzi wa Kijerumani Gottlieb Daimler akiwa na umri wa miaka 64. Daimler alizaliwa mwaka 1834 na kazi yake ya mwanzo ilikuwa utengenezaji bunduki. Tangu akiwa kijana mvumbuzi huyo alivutiwa sana na kazi za viwandani na alifanya utafiti mkubwa katika uwanja huo hadi alipofanikiwa kutengeneza pikipiki. Gottlieb Daimler pia alikuwa miongoni mwa watu walioweka misingi ya utengenezaji wa magari madogo na hata mabasi.

Gottliieb

Tarehe 6 Machi miaka 62 iliyopita, nchi ya Ghana ilifanikiwa kupata uhuru chini ya uongozi wa Dakta Kwame Nkurumah. Ghana ilitumbukia katika makucha ya mkoloni wa Kireno kuanzia karne ya 15. Baada ya Wareno, Waingereza waliidhibiti na kuikoloni nchi hiyo iliyokuwa mashuhuri kwa jina la "Pwani ya Dhahabu" kutokana na utajiri wake mkubwa wa madini hayo.