Hadithi ya Uongofu (141)
Assalamu alaykum, wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia na kujadili maudhui ya matumaini na kukata tamaa.
Tulisema kuwa, katika Uislamu matumaini na matarajio au rajua ni jambo ambalo lina nafasi ya hali ya juu; kiasi kwamba, katika hadithi na riwaya za Maasumina (AS), linatajwa kuwa ni "rehma ya Mwenyezi Mungu." Mtume (SAW) amenukuliwa akisema: Rajua na tumaini ni rehma kwa ajili ya umma wangu; na lau rajua na tumaini visingelikuweko, basi hakuna mama ambaye angemnyonyesha mwanawe na hakuna mtunza bustani ambaye angepanda mche. Tulieleza kwamba, baada ya shirki na kumshirikisha Mwenyezi Mungu hakuna dhambi ambayo ni kubwa zaidi ya kukata tamaa na Mwenyezi Mungu.
Mja aliyetenda dhambi, madhali angali si mwenye kukata tamaa na rehma na msamaha wa Mwenyezi Mungu, basi yumkini akafanya toba na kuomba maghufira na akasamehewa na Mola Muumba. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 141 kitazungumzi maudhui ya hofu na matarajio. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio niliyokuandalieni kwa leo.
Hofu na matarajio ni aina mbili muhimu za tablighi na ufiklishaji ujumbe katika dini zote za mbinguni, na Mitume wa Mwenyezi Mungu walikuwa wakitumia mbinu hizi katika kulea watu na kadhalika katika kulea nafsi zao. Kimsingi hofu ina nafasi katika kumzuia mtu kufanya matendo mabaya na dhambi na huu ni wenzo bora kabisa wa nguvu ya hofu katika ujudi na uwepo wa mwanadamu. Matarajio au matumaini zaidi huwa na nafasi katika upande wa ushajiishaji kwa ajili ya kutii na kutenda mema. Katika kitabu cha Qur’ani Tukufu kikawaida kila mahala ambapo kumezungumziwa adhabu ya Mwenyezi Mungu na moto uunguzao wa Jahanamu, basi pembeni yake kumetajwa pia rehma na neema za peponi. Katika hadithi pia hali iko namna hii.
Bwana mmoja alimuuliza Imam Jafar Swadiq AS kwa kusema, katika wasia wa Luqman al-Hakim kulikuwa na mambo gani?
Imam Swadiq AS katika kujibu swali hili akasema: Kulikuwa na mambo ya kustaajabisha ambapo kubwa zaidi ni pale alipomwambia mwanawe: Muogope Mwenyezi Mungu kiasi kwamba, kama utakwenda mbele yake ukiwa na mema ya majini na wanadamu atakuadhibu, na kuwa na matarajio na matumaini na Mwenyezi Mungu kiasi kwamba, hata kama utakwenda mbele yake ukiwa na madhambi ya majini na wanadamu akurehemu na kukusamehe.
Kwa hakika, baadhi wanayataja maneno mawili ya hofu na matarajio kwamba, yako mkabala na kwamba, haiwezekani kuyaweka pamoja. Lakini kama ambavyo Mwenyezi Mungu kwa uwezo wake ameweza kukusanya pamoja sumu na asali katika ujudi wa nyuki, vivyo hivyo ameweka hofu na matarajio katika moyo wa muumini. Hii hali ya uwiano baina ya hofu na matarajio ni muhimu kiasi kwamba, katika baadhi ya hadithi inatajwa kuwa ni sharti la Imani, na mja bila ya kuwa na hofu na matarajio hawezi kunufaika na ukweli na uhakik wa imani.
Imam Jafar bin Muhammad al-Swadiq AS anazungumzia nukta hii kwa kusema: Muumini hawezi kuwa muumini mpaka atakapokuwa mwenye hofu na mwenye matarajio,na hawezi kuwa mwenye hofu na matarajio mpaka atakapokifanyia kazi kile anachokiogopa au kile ambacho ana matarajio nacho. Aidha katika hadithi nyingine amenukuliwa Imam Ali bin Abi Twalib AS akisema: Vitu vitatu kama mtu atakakuwa navyo, basi imani yake imekamilika. Mosi, uadilifu katika hali ya furaha na ghadhabu, pili hali ya kati na kati katika wakati wa kutokuwa na kitu na kuwa nacho (yaani katika hali ya umasikini na utajiri); na tatu kulingana hofu na matarajio. Yaani kuwa katika uwiano. Kadhalika Imam Ali bin Abi Twalib AS amenukuliwa akisema: Kwa mtu ambaye amemtambua Mwenyezi Mungu basi inastahiki moyo wake usikose matumaini na hofu ya Mwenyezi Mungu.
Katika hadithi na riwaya za Kiislamu suala la uwiano wa hofu na matarajio limekokotezwa na kutiliwa mkazo. Kwa maana kwamba, muumini mbali na kumuogopa Mwenyezi Mungu anapaswa wakati huo huo pia kuwa na matarajio na rehma za Mola Muumba. Mja anapaswa kuwa na hali ya uwiano baina ya mawili haya, yaani hofu na matarajio. Hii ni kutokana na kuwa, kukosa au kutokuwa na hali ya kati na kati na kuongezeka au moja kati ya hilo kuwa zito kuliko jingine, huweza kumfanya mhusika apate madhara ya kiroho yasiyofidika. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana wajuzi wa mambo wanainasibisha hofu na matarajio na mbawa mbili za ndege.
Wanasema kuwa, hofu na matarajio ni mithili ya mbawa mbili za ndege ambazo anazitumia kuruka na kupaa. Kama bawa moja kati ya mawili hayo litakuwa na mapungufu, ndege atakabiliwa na mushkili wa kuruka na kupaa. Na ikiwa mbawa zote mbili zitakuwa na mapungufu au majeraha basi ndege mwenye mbawa hizo hataweza katu kuruka na kupaa. Imam Muhammad Baqir AS anazungumzia ulazima wa mawili haya kuwa pamoja yaani hofu na matarajio akisema: Mja hawezi kuwa muumini isipokuwa kama katika moyo wake kutakuwa na nuru mbili; nuru ya hofu (woga) na nuru ya matarajio (matumaini) ambapo kama viwili hivi vitapimwa (katika mzani) hakuna kimoja ambacho kitakuwa kizito kwa kingine.
Wapenzi wasikilizaji, hofu na matarajio ni katika sifa za waumini na wacha Mungu. Waumini daima huwa na matarajio na matumaini na rehma za Mwenyezi Mungu, na daima hufanya hima wakiwa na nishati na uchangamfu katika njia ya uja wao na kila siku hujikurubisha na ahadi za Mwenyezi Mungu. Katika aya ya 60 ya Surat al-Muuminun Mwenyezi Mungu mbali na kuwasifia waumini anasema kwamba:
Na wale ambao wanatoa walichopewa, na hali nyoyo zao zinagopa kwa kuwa watarejea kwa Mola wao Mlezi.
Katika kufasiri aya hii, Imam Jafar Swadiq AS anasema: Waumini wana hofu ya kukataliwa amali zao kutokana na baadhi ya dhambi na katika upande mwingine wana matarajio ya kukubaliwa baadhi ya amali zao.
Katika kuhitimisha kipindi chetu cha leo tunasema kuwa, watu waumini ili waweze kupiga hatua katika njia ya Mwenyezi Mungu wana njia tatu mbele yao. Njia ya matumaini, njia ya hofu na njia ya huba, ambapo njia hii ya tatu ya huba ipo juu zaidi ikilinganishwa na njia mbili za matarajio na hofu. Kuhusiana na njia hizi tatu, Imam Ali AS anazibainisha katika maneno mafupi lakini yaliyobeba maana kubwa kwa kusema: Kuna kundi linamuabudu Mwenyezi Mungu kwa raghba na shauku na hii ni ibada ya wafanyabiashara; kundi jingine linamuabudu Mwenyezi Mungu kwa hofu na woga ambapo hii ni ibada ya watumwa na kundi jingine linamuabudu Mwenyezi Mungu ili kushukuru na hii ni ibada ya watu huru.
Wapenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.
Na Salum Bendera