Jumamosi, 09 Machi, 2019
Leo ni Jumamosi tarehe Pili Rajab 1440 Hijria mwafaka na tarehe 9 Machi 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1219 iliyopita, kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa Ibn Rumi, malenga mashuhuri wa Kiarabu mjini Baghdad, Iraq. Alianza kusoma elimu ya awali kwa baba yake akiwa kijana mdogo, na baadaye akasoma kwa walimu wakubwa wa enzi zake. Aidha alipata kujifunza elimu za zama zake kama vile fasihi na mashairi. Ibn Rumi alikuwa akisoma sana mashairi ya kumsifu Imam Hassan Askari, mmoja wa Ahlubaiti wa Mtume (saw) kutokana na mapenzi yake makubwa aliyokuwanayo kwa watu wa familia ya Mtume wa Allah (as). Malenga huyo alifariki dunia mwaka 283 Hijiria. ***
Katika siku kama ya leo miaka 1000 iliyopita, alifariki dunia Abu Raihan Biruni msomi, mnajimu na mwanahisabati mkubwa wa Kiirani huko katika mji wa Ghazne katikati mwa Afghnaistan ya sasa. Abu Raihan Biruni alikuwa hodari katika elimu za historia, jiografia na hisabati, tiba na utengenezaji wa dawa. Akiwa safarini nchini India, msomi huyo wa Kiirani alikutana na kufanya mijadala na maulama na watawala wa zama hizo. Abu Raihan alikusanya taarifa muhimu alizokuwa akizihitaji kwa ajili ya kuandika kitabu chake alichokiita 'Tahqiq Ma Lilhind' baada ya kujifunza lugha ya Sanskriti yaani lugha ya Kihindi ya kale. Katika kitabu hicho, Abu Raihan ameandika taarifa muhimu kuhusu sayansi, itikadi, mila na desturi za Wahindi. Msomi huyo wa Kiirani ameandika vitabu vingine vingi kuhusu elimu ya nujumu, mantiki na falsafa. ***
Miaka 565 iliyopita sawa na tarehe 9 mwezi Machi mwaka 1454 Miladia alizaliwa mvumbuzi na baharia wa Kiitalia kwa jina la Americo Vespucci. Vespucci alijishughulisha na kazi za melini kutokana na hamu yake kubwa ya kupenda ubaharia aliyoionyesha tangu akiwa kijana na hivyo kupewa cheo cha unahodha. Baharia Americo Vespucci alisafiri mara nne katika nchi isiyojulikana ambayo hadi wakati huo ilikuwa haina jina na baadaye ikapatiwa jina la mvumbuzi huyo wa Kiitalia yaani Amerika. ***
Katika siku kama ya leo miaka 122 iliyopita, Sayyid Jamaluddin Asadabadi mwanazuoni na mmoja wa viongozi wa mapambano dhidi ya ukoloni wa kimaitaifa dhidi ya Waislamu aliuawa. Sayyid Jamaluddin alizaliwa huko Asadabad katika mji wa Hamedan wa magharibi mwa Iran na kupata elimu katika taalamu za falsafa, nujumu na historia. Mbali na kufahamu lugha za Kiarabu, Kifarsi na Kituruki, Sayyid Jamaluddin Asadabadi alikuwa mtaalamu pia katika lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kirusi. ***
Na miaka 23 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sheikh Muhammad Ghazali mwanazuoni na mwanamageuzi mkubwa wa Misri. Alizaliwa mwaka 1917 huko nchini Misri. Akiwa na umri wa miaka 10 tu, tayari Muhammad Ghazali alikuwa amehifadhi Qur'ani Tukufu yote. Muhammad Ghazali alihitimu Chuo Kikuu akiwa na umrii wa miaka 24. Fikra zake zilijengeka juu ya msingi wa mageuzi ya maarifa ya kidini, kukurubisha baina ya madhehebu na kupinga fikra za kikaumu. Muhammad Gahazli aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 79 kwa mshtuko wa moyo na kuuzikkwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina. ***