Jumatano tarehe 13 Machi 2019
Leo ni Jumatano tarehe 6 Rajab 1440 Hijria inayosadifiana na tarehe 13 Machi 2019.
Tarehe 6 Rajab miaka 924 iliyopita, alifariki dunia Abu Muhammad Qasim bin Ali Basri maarufu kwa jina la Ibn Hariri, mwanafasihi na mwandishi mashuhuri wa Kiirani aliyekuwa akiishi Basra nchini Iraq. Ibn Hariri ndiye mwandishi wa kitabu maarufu cha 'Maqamaat' ambacho ni cha aina yake katika taaluma ya fasihi ya Kiarabu. Katika kitabu hicho, Ibn Hariri alieleza siri za fasihi ya lugha ya Kiarabu katika kalibu ya hikaya na semi nyepesi za hekima.

Siku kama ya leo miaka 286 iliyopita, inayosadifiana na 13 Machi, 1733 alizaliwa Joseph Priestley, mkemia na mwanafizikia wa Uingereza. Priestley alikuwa mashuhuri mno hasa katika taaluma ya kemia. Katika uchunguzi na utafiti wake, aliweza kuvumbua uvutaji pumzi katika mimea na hewa za oksijeni na nitrogen. Joseph Priestley alifariki dunia mwaka 1804.
Tarehe 13 Machi miaka 71 iliyopita Wazayuni waliokuwa na mfungamano na kundi la kigaidi la Haganah, walishambulia kitongoji cha Wapalestina cha Husseiniyah katika eneo la kaskazini mwa Jalilah. Wazayuni hao waliua shahidi zaidi ya Wapalestina 60 na kuharibu nyumba zao kadhaa. Katika siku hiyohiyo, wanajeshi wa Israel walizilipua kwa mabomu nyumba za Wapalestina katika eneo la 'Qatmuun' lililoko Baitul Muqaddas. Mauaji ya Waislamu wa Palestina yaliyofanywa na makundi ya kigaidi ya Israel, yalitekelezwa kwa lengo la kutaka kutangaza uwepo wa utawala huo bandia kwenye ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina baada ya kuondoka vikosi vya majeshi ya Uingereza katika eneo hilo.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, inayosadifiana na 13 Machi 1983, Joshua Nkomo kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe alikimbilia nchini Uingereza akihofia usalama wa maisha yake. Nkomo ambaye alikiongoza chama cha Zimbabwe African People's Union (ZAPU) alisema kuwa, alilazimika kutoroka nchini Zimbabwe na kukimbilia Uingereza kwa kuwa maisha yake yalikuwa hatarini. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Brigedi ya Tano ya jeshi la Zimbabwe kuizingira kambi yake iliyoko katika mji wa Bulawayo.
Na siku kama hii leo miaka 39 hayati Imam Ruhullah Khomeini alitoa amri ya kuundwa taasisi itakayokuwa ikishughulikia hali ya familia za mashahidi waliouawa katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Sehemu moja ya ujumbe huo ilisema: "Sisi sote tunajua kwamba, harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu na ushindi wa mapinduzi hayo nchini Iran ni matunda ya kujitolea mhanga kwa matabaka ya wananchi na kuna udharura wa kuwaenzi na kuwajali zaidi mashahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu".
