Mar 14, 2019 21:43 UTC
  • Ijumaa tarehe 15 Machi mwaka 2019

Leo ni Ijumaa tarehe 8 Rajab 1440 Hijria sawa na tarehe 15 mwezi Machi mwaka 2019.

Siku kama hii ya leo miaka 30 iliyopita ardhi ya Taba huko kaskazini mashariki mwa Misri ilikombolewa baada ya kukaliwa kwa mabavu kwa miaka kadhaa na utawala ghasibu wa Israel. Utawala wa Kizayuni ulilikalia kwa mabavu jangwa la Sinai katika vita vya mwaka 1967, ambalo upande wa mashariki mwake linapatikana eneo la Taba. Utawala wa Tel Aviv ulikubali kuirejeshea Misri jangwa la Sinai baada ya kusaini mkataba wa Camp David mwaka 1987. Israel iliendelea kulikalia kijeshi eneo muhimu la Taba huko kaskazini mwa Ghuba ya Aqaba, licha ya utawala huo wa Kizayuni kuondoka katika baadhi ya sehemu za jangwa hilo.

Taba, kaskazini mashariki mwa Misri

Miaka 34 iliyopita katika siku kama ya leo, vibaraka wa madola ya kigeni walilipua bomu katika hadhara kubwa ya waumini waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya ibada muhimu ya Sala ya Ijumaa  mjini Tehran na kuwaua shahidi waumini kadhaa pamoja na kuwajeruhi wengine wengi. Sambamba na kutekelezwa kwa kitendo hicho cha kigaidi dhidi ya raia wasio na hatia, ndege za kivita za Iraq ziliruka na kuingia katika anga ya mji mkuu Tehran kama tishio la kuonyesha kwamba, mji huu ulikuwa chini ya mashambulio.

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita uchaguzi wa Majlisi ya kwanza ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la kwanza la Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulifanyika hapa nchini na hivyo kutimiza moja ya malengo ya mapinduzi hayo. Kwa sasa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ina wawakilishi 290 ambao huhudumu bungeni kwa kipindi cha miaka 4. Wafuasi wa dini za waliowachache nchini Iran kama Wakristo na Wayahudi pia kwa uchache huwa na mwakilishi mmoja katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu.Bunge la Iran hutunga sheria zinazohusiana na masuala ya umma kwa sharti kwamba zisipingane na sharia za Kiislamu. Kazi nyingine muhimu ya Bunge hilo ni kuwasaili, kuwapasisha au kuwauzulu mawaziri wa serikali.

Uchaguzi wa Majlisi ya kwanza ya Ushauri ya Kiislamu

Siku kama ya leo miaka 165 iliyopita alizaliwa tabibu maarufu wa Kijerumani kwa jina la Emil Adolf von Behring. Behring aliendeleza utafiti wa Louis Pastor, mwanakemia wa Kifaransa wa zama hizo katika uwanja wa kutambua na kuzuia maradhi yanayoambukiza na kupata mafanikio makubwa katika suala hilo. Emil Adolf von Behring alitunukiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya fizikia mwaka 1901.

Emil Adolf von Behring

Na tarehe 8 Rajab miaka 407 iliyopita alizaliwa faqihi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Sheikh Abu Jaafar Muhammad bin Hassan maarufu kwa jina la Sheikh Hurr al Aamili huko Jabar Amil nchini Lebanon. Baada ya utafiti na uchunguzi wa muda mrefu Sheikh Aamili alitokea kuwa miongoni mwa maulama wakubwa wazama hizo hususan katika elimu za fiqhi na hadithi. Sheikh Hurr al Amili ameandika vitabu vingi katika taaluma hizo na miongoni mwao ni kile cha Wasailu Shia ambacho kina nafasi maalumu katika elimu ya fiqhi. Kitabu kingine muhimu cha mwanazuoni huyo ni Hidayatul Umma.