Mar 16, 2019 01:08 UTC
  • Jumamosi, 16 Machi, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 9 ya mwezi Rajab 1440 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 16 Machi 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 477 iliyopita yaani tarehe 9 Rajab mwaka 963 Hijria, alikufa shahidi Izzudeen Sayyid Hussein mmoja wa maulama wakubwa wa karne ya kumi Hijria. Alizaliwa mwaka 906 katika moja ya vijiji vya Jabal Amil nchini Lebanon na kusoma elimu zilizokuwa mashuhuri katika zama hizo. Bidii na hima kubwa aliyokuwa nayo Izzudeen Sayyid Hussein ilimfanya akwee kwa haraka mno daraja za kielimu na kuwa miongoni mwa wasomi na maurafaa wakubwa katika zama hizo. Hata hivyo, watu wabaya waliokuwa na chuki naye hawakuweza kustahamili shakhsia yake hiyo hivyo wakapanga njama na kumpa sumu katika mji wa Saida na hivyo kumuua shahidi. ***

Izzudeen Sayyid Hussein

Katika siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, Parvin I’tisami mwandishi na malenga mahiri wa Kiirani aliyekuwa na kipaji kikubwa alizaliwa katika mji wa Tabriz ulioko kaskazini magharibi mwa Iran. Mshairi huyu alizaliwa katika familia iliyosifika kwa fadhila na heshima. Baba yake ni Yusuf I’tisam al-Mulk aliyekuwa mmoja wa watarjumi na waandishi watajika katika zama zake. Parvin alijifunza fasihi ya Iran na ya Kiarabu kwa baba yake na alionyesha kipaji cha hali ya juu cha mashairi tangu akiwa mdogo. Katika kipindi chote cha masomo, Parvin I’tisami alikuwa mwanafunzi bora shuleni. Safari zote alizifanya akiwa pamoja na baba yake na kujifunza mambo mengi katika safari hizo. ***

Parvin I’tisami

Miaka 80 iliyopita katika siku kama ya leo, katika hali ambayo Vita vya Pili vya Dunia havikuwa vimeanza, nchi ya Czechoslovakia ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Ujerumani ya Kinazi. Kwa utaratibu huu, Jamhuri ya Czechoslovakia ikawa nchi ya pili baada ya Austria kukaliwa kwa mabavu na Adolph Hitler. ***

Czechoslovakia

Katika siku kama ya leo miaka  79 iliyopita, alifariki dunia Bi Selma Lagerlof mwandishi wa Sweden. Lagerlof alizaliwa mwaka 1858 na baada ya kumaliza masomo yake akaanza kujishughulisha na ukufunzi na uandishi wa hadithi na hekaya. Lagerlof alikuwa mwanamke wa kwanza kutunukiwa tuzo ya Nobel katika fasihi mwaka 1909. ***

Bi Selma Lagerlof

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, Kamal Fouad Jumblatt mwanasiasa mahiri wa Lebanon aliuawa.  Alizaliwa Disemba 6 mwaka 1917 huko Moukhtara kusini mwa Beirut. Mwaka 1952 na kuendelea, Kamal Fouad Jumblatt  alikuwa mwanasiasa wa mrengo wa upinzani na akafanikiwa kumuondoa madarakani Bechara El Khoury Rais wa muda wa wakati huo wa Lebanon. Hatimaye Kamal Fouad Jumblatt  aliuawa na wapinzani wake katika siku ma ya leo  akiwa na umri wa miaka 60. ***

Kamal Fouad Jumblatt

Katika siku kama ya leo miaka 34 iliyopita Mahdi Bakeri mmoja wa makamanda mashujaa na wenye tadibiri katika kipindi cha kujihami kutakatifu wanananchi wa Iran mbele ya hujuma na mashambulio ya kichokozi ya jeshi la dikteta  wa wakati huo wa Iraq Saddam Hussein alikufa shahidi. Alizaliwa katika mji wa Miandoab kaskazini magharibi mwa Iran na mama yake alifariki dunia wakati yeye akiwa mtoto mdogo. Kaka yake naye kutokana na kuonyesha upinzani dhidi ya utawala dhalimu wa Shah aliuawa na makachero wa utawala huo. ***

Mahdi Bakeri

Na siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, utawala wa Baath nchini Iraq uliushambulia bila huruma na kwa mabomu ya kemikali za sumu mji wa Halabja wa wakazi wa Kikurdi huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo kwa kutumia makumi ya ndege za kivita. Hujuma hiyo ilianza baada ya kushindwa kupambana na wapiganaji Waislamu wa Iran na wa Kikurdi wa huko Iraq, na katika upande wa pili wananchi Waislamu wa Halabja waliwakaribisha wapiganaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na dhulma na ukandamizaji usio na kipimo wa Saddam Hussein dhidi yao. Raia elfu tano wasio na hatia waliuawa kutokana na kuvuta gesi ya sumu huko Halabja. Hata hivyo nchi za Magharibi hazikuchukua hatua yoyote kwa jinai hiyo kubwa na ya kutisha. ***

Halabja