Jumanne tarehe 19 Machi mwaka 2019
Leo ni Jumanne tarehe 12 Rajab mwaka 1440 Hijria sawa na tarehe 19 Machi 2019.
Tarehe 12 Rajab miaka 1408 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Abbas bin Abdul Muttalib, ami yake Bwana Mtume SAW na mmoja wa shakhsia wakubwa wa Kikuraishi. Alijulikana kwa tabia njema, mwenendo mzuri, busara na maarifa ya hali ya juu. Baadhi ya wanahistoria wanaamini kwamba, Abbas bin Abdul Muttalib aliukubali Uislamu kwa siri kabla ya Bwana Mtume kuhamia Madina na alikuwa akimpelekea Mtume habari za harakati za washirikina mjini Makka. Mwaka wa 8 Hijria Abbas bin Abdul Muttalib aliungana na Waislamu na baada ya Fat'hu Makka aliteuliwa na Bwana Mtume kuchukua jukumu la kutoa huduma ya maji kwa watu wanaozuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al-Kaaba.

Siku kama ya leo miaka 1234 iliyopita, alifariki dunia Abu Hudheifa mpokezi wa hadithi, habari za kihistoria na mwandishi mkubwa wa visa vya Mitume. Kwa muda fulani aliishi katika miji ya Makka na Madina na kujishughulisha na masomo ya hadithi. Abu Hudheifa alikuwa mpokezi wa hadithi mwenye itibari kubwa. Miongoni mwa vitabu vyake muhimu ni pamoja na kile cha "Al Mubtada" kinachohusu uumbwaji wa mwanadamu na visa vya Mitume. Kitabu chake kingine ni kile kinachohusu uchambuzi wa hadithi ya Imam Swadiq (as) kuhusu mi'raji ya Mtume Mtukufu (saw).

Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita, alizaliwa Sir Norman Haworth, mtaalamu wa kemia wa Uingereza. Sir Haworth alifanya utafiti na uhakiki mwingi wa kisayansi kuhusu haidrokaboni na akafanikiwa kubuni mpango mpya kwa ajili ya muundo wa molekuli ya sukari. Vilevile Sir Haworth alifanya utafiti na majaribio kuhusu vitamini C ambayo muundo wa molekuli yake unashabihiana na sukari na akatayarisha aina yake ya kutengenezwa viwandani kwa jina la asidi askobiki. Mwaka 1937 Sir Norman Haworth alitunukiwa tuzo ya kemia ya Nobel kutokana na uhakiki na utafiti wake mkubwa. Sir Haworth alifariki dunia mwaka 1950.
Na siku kama ya leo miaka 32 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Machi 1987 alifariki dunia Louis de Broglie, ambaye alikuwa wa mwisho katika kizazi cha waasisi wa fizikia ya kisasa akiwa na umri wa miaka 95. Louis de Broglie alizaliwa mwaka 1892 na baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia alianza utafiti wa elimu ya fizikia. Mtaalamu huyo wa fizikia wa Ufaransa alitatua masuala mengi ya elimu hiyo kwa nadharia yake mashuhuri ya Wave Particle Duality. Mwaka 1929 alitunukiwa tuzo ya fizikia ya Nobel.