Jumapili, tarehe 24, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 17 Rajab mwaka 1440 Hijria, sawa na tarehe 24 Machi 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 319 iliyopita, yaani sawa na tarehe 17 Rajab 1121 Hijiria, alifariki duani Allamah Fadhil Sheikh Sulaiman Bahrani, mmoja wa wasomi wakubwa wa Kishia. Sheikh Abul-Hassan Sulaiman Ibn Abdillah Ibn Ali Ibn Hassan Bahrani Mahuzi, maarufu kwa jina la Muhaqqiq Bahrani, mmoja wa maulama wa Kishia wa mwanzoni mwa karne ya 12 Hijiria, alizaliwa katikati ya mwezi wa Ramadhani mwaka 1076 Hijiria. Alibobea katika elimu ya hadithi, wapokezi wa hadithi, historia na maisha ya mtukufu Mtume (saw) na Ahlu Baiti wake (as). Sheikh Abdullah Samahiji na Sayyid Hashim Bahrani, mwandishi wa tafsiri ya Qur'an ya Al-Burhan na Sheikh Ahmad Bahrani, ni miongoni mwa wanafunzi wa Allamah Fadhil Sheikh Sulaiman Bahrani. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu cha 'al-Shifaau fil-Hikmat al-Nadharia wal-Mi'raaj.' Msomi huyo mkubwa alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 46.
Siku kama ya leo miaka 169 iliyopita, Ayatullahil Udhma Sayyid Abu-Turab Khonsari, mmoja wa maulama na maustadhi wakubwa alizaliwa huko Khonsar moja ya miji ya katikati mwa Iran. Ayatullahil Udhma Khonsari alisoma masomo ya akili na nakili kwa maustadhi muhimu wa zama zake. Juhudi zake masomoni zilimfanye aondokee kuwa ustadhi mahiri katika masomo ya fiqhi, usulul fiqhi na tafsiri ya Qur'ani. Ayatullah Khonsari ameandika vitabu vingi kuhusiana na elimu mbalimbali za kidini. Kitabu cha Qasdus Sabil kuhusiana na elimu ya usulul fqhi na Misbahus Swalihiin kinachozungumzia misingi ya dini, ni baadhi tu ya vitabu vyenye thamani vya msomi huyu mahiri wa Kiislamu aliyefariki dunia mwaka 1346 Hijria.
Katika siku kama ya leo miaka 113 iliyopita, alifariki dunia mwandishi wa hekaya wa Kifaransa Jules Verne akiwa na umri wa miaka 77. Verne alizaliwa Februari mwaka 1828 na alifanikiwa kuandika vitabu vingi na vya kuvutia vya hekaya ambapo ndani yake alielezea utabiri wake kuhusu ustawi wa sayansi ya mwanadamu. Miongoni mwa athari hizo ni pamoja na vitabu alivyoviita Twenty Thousand Leagues Under the Sea, A Journey to the Center of the Earth na Around the World in Eighty Days. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, filamu mbalimbali zenye kutoa mafunzo kwa watoto na vijana zilitengenezwa kwa mujibu wa baadhi ya hekaya hizo za Jules Verne.
Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, yaani sawa na tarehe nne Farvardin 1365 Hijiria Shamsia, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 57 Ustadh Amir Hussein Yazdigardi, kati ya wataalamu wa elimu ya fasihi wa Iran. Sambamba na kufundisha katika chuo kidogo cha al-Hayat cha mjini Tehran, alikuwa pia muhariri wa baadhi ya majarida kwa kushirikiana na Ustadh Forouzanfar, ambaye naye alikuwa kati ya wataalamu mashuhuri wa fasihi ya lugha ya Kifarsi. Kazi muhimu ya Yazdigardi ilikuwa ni kusahihisha, kufanya uchunguzi na kusherehesha vitabu vya watafiti wengine hususan kwenye uwanja wa vitabu vya historia. Mbali na fasihi, Ustadh Amir Hussein Yazdigardi alikuwa na shughuli nyingine tofauti.
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, msikiti mkuu wa mji wa Ganja ambao ni wa pili kwa ukubwa katika Jamhuri ya Azerbaijan ulikarabatiwa na kufunguliwa upya baada ya kufungwa kwa miaka 70. Msikiti huo ulikuwa umefungwa tangu mwaka 1920 na kufunguliwa tena katika muongo wa 80 katika hafla iliyofanyika sambamba na kuswaliwa Swala ya jamaa. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, makumi ya misikiti ilikarabatiwa na kutumiwa na Waislamu kufuatia matukio ya kisiasa yaliyotokea Urusi ya zamani na katika jamhuri zake na pia kutokana na matakwa ya Waislamu wote wa Jamhuri ya Azerbaijan.
Na miaka 137 iliyopita katika siku kama ya leo, Robert Koch daktari na mtafiti wa Kijerumani aligundua vijidudu maradhi vinavyosababisha ugonjwa wa kifua kikuu au Tuberculosis vinavyoitwa tubercle bacillus. Koch alifanya utafiti na kutwalii sana kwa zaidi ya miaka 10 ili kutambua chanzo cha maradhi ya kifua kikuu au TB na hatimaye akafanikiwa kugundua vimelea maradhi hivyo na kuvipa jina lake la Baccilus Koch. Mwaka 1905 Miladia, tabibu huyo wa Kijerumani alitunukiwa tuzo ya Nobel katika fani ya fiziolojia na tiba.