Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain 117
Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika kipindi cha juma hili cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain kunachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutagazieni kutoka mjini Tehran.
Katika kipindi hiki tutajibu swali lifuatalo: Je, kuna hadithi zozote za Mtume Mtukufu (saw) zinazokubalika na madhehebu zote za Kiislamu ambazo zinaashiria kuwepo kwa Imam aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu, katika zama zote hadi Siku ya Kiama?
Wapenzi wasikilizaji, katika kipindi kilichopita tulizungumzia aya za Qur'ani Tukufu zinazoashiria suala hilo ambapo tuliona kwamba kitabu hicho kitakatifu kinazungumzia kwa uwazi mkubwa ukweli kwamba Mwenyezi Mungu amemchagua Imam mwongozaji katika kila zama ambaye anapasa kuwaongoza wanadamu kuelekea kwake na kwa amri Yake. Je, kuna uwazi kama huo katika hadithi za Mtume Mtukufu (saw)? Jongeeni redio zenu ili tupate kujadili kwa pamoja suala hili.
************
Ndugu wasikilizaji, kuna hadithi nyingi za kuaminika katika madhehebu zote za Kiislamu zinazoashiria kwamba kutokana na rehema zake kwa waja wake, Mwenyezi Mungu hakuacha zama zozote zile, tokea zama za Nabii Adam (as) hadi Siku ya Kiama, bila ya kuwa na mwongozaji mwema wa kuwaongoza wanadamu kuelekea kwake. Kuna vitabu vingi sana vya utafiti ambavyo vimeandikwa katika uwanja huu ambapo wanazuoni na watafiti wameandika na kunukuu mamia ya hadithi tukufu ambazo zinathibitisha ukweli tuliotangulia kuuashiria kuhusiana na suala la Uimamu. Vitabu hivyo ni pamoja na Ihqaqul Haq, Abaqaat al-An'waar na al-Ghadir. Sisi hapa tutatosheka tu kwa kutaja hadithi kadhaa za Mtume Mtukufu (saw) zilizonukuliwa katika vitabu vya Ahlu Sunna vya Bukhari, Muslim na Musnad Ahmad bin Hambal. Mtume ananukuliwa katika vitabu hivyo akisema: 'Suala hili litaendelea kuwepo miongoni mwa Qureish hata kama ni watu viwili tu watakuwa wamesalia ardhini.' Na kusudio la 'suala' katika hadithi hii ni Uimamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ulioashiriwa katika aya ya 59 ya Surat an-Nisaa inayosema: Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi.
Aya hii inatuelekeza kwenye ukweli kwamba kusudio la Uimamu hapa ni kufungamanishwa utiifu wa wenye mamlaka na utiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa namna ambayo ni ya moja kwa moja. Jambo hilo bila shaka linamaanisha kwamba Maimamu ni maasumu na kwamba wamepata isma au umaasumu huo kutoka kwa Mwenyezi Mungu moja kwa moja. Hadithi hii tukufu inathibitisha wazi kwamba ardhi haiwezi kuwa bila ya Imam kutoka ukoo wa Quraish, ambaye anaongoza wanadamu baada ya Mtume Mtukufu (saw), kwa amri ya Mwenyezi Mungu, hadi Siku ya Kiama. Na dalili na hoja hii pia inaonekana wazi katika vitabu vya Tarikh Bukhari, Musnad Ahmad, Sahih Ibn Hibban na vingine vya Ibn Abi Shaibah, Tayalisi, Abu Ya'la, Tabarani, Bazaz na wengine ambao wamemnukuu Mtume (saw) akisema: 'Mtu anayekufa bila ya kuwa na Imam huwa amekufa kifo cha ujahili.’
********
Ndugu wasikilizaji kuna hadithi nyingi mno ambazo zimepokelewa na Ahlu Sunna zinazothibitisha suala hili la Uimamu, ambapo al-Allama al-Majlisi amekusanya baadhi ya hadithi hizo katika juzuu ya 23 ya kitabu chake cha Bihar katika mlango wa 'Udharura wa kuwepo Hujja' kuhusu suala la Uimamu. Tunataja baadhi ya hadithi hizo hapa. Imam Swadiq (as) amenukuliwa katika kitabu cha al-Mahasin akisema: 'Unabii wa Adam ulipomalizika, Mwenyezi Mungu Mtukufu alimteremshia Wahyi akimwambia: Ewe Adam! Unabii wako umemalizika….basi tazama una nini katika elimu, imani, urithi na Unabii…. na jina kuu la Mwenyezi Mungu. Nitavijalia vitu hivi kuwa hiba ya Mwenyezi Mungu kwenye kizazi chako (kwa mwanao). Hakika mimi sitaiacha ardhi bila ya kuwa na aalim (mjuzi) ambaye kupitia kwake itiifu na dini yangu itafahamika na hivyo (aalim huyo) kuwa mtu wa kumnusuru atakayemtii.'
Na hadithi nyingine ya Qudsy ambayo imepokelewa kutoka kwa Imam Swadiq katika kitabu cha Ilal as-Sharai' inamnukuu mtukufu huyo akisema: 'Jibril alimteremkia Muhammad (saw) akiwa na habari kutoka kwa Mola wake Mtukufu na kumwambia: 'Ewe Muhammad (hakika mimi) sijaiacha ardhi bila ya kuwa na aalim (mjuzi) ambaye kupitia kwake utiifu na uongozi wangu utajulikana, na kuwa mwenye kunusuru baina ya (wakati wa) kuaga dunia nabii mmoja na kudhihiri mwingine. Na siwezi kumuacha Ibilisi awapotoze watu bila ya kuwepo kwenye ardhi hujja na mwenye kuita (watu) kuelekea kwangu na mwongozaji katika njia yangu na anayejua amri zangu. Hakika mimi nimeichagulia kila kaumu mwongozaji ambaye kupitia kwake nitawaongoza wenye saada na kuwa hoja kwa (dhidi ya) waovu.'
**********
Imam Muhammad Baqir (as) amepokelewa katika kitabu cha al-Kafi akisema: 'Aya hii (Siku tutakapowaita watu kwa Imam wao) ilipoteremka, Waislamu walisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, si wewe ndiwe Imam wa watu wote? Mtume (saw) akajibu: Mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa watu wote lakini baada yangu kutakuwepo na Maimamu ambao watawaongoza watu kutoka kwenye Aali zangu ambao watasimama miongoni mwa watu. Watakadhibishwa na kudhulumiwa na maimamu wa kufri na upotovu pamoja na wafuasi wao. Hivyo basi mtu atakayewakubali, kuwafuata na kuwasadiki atakuwa anatokana na mimi, pamoja nami na atakutana nami. Bila shaka mtu atakayewadhulumu na kuwakadhibisha hatakuwa anatokana na mimi wala kuwa pamoja nami na mimi nitajitenga naye.'
Na katika Tafsiri ya Ali bin Ibrahim (MA), Imam AS-Swadiq (as) ananukuliwa akisema: 'Mwonyaji ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Mwongozaji ni Amir al-Mu'mineen (as) –baada yake na Maimamu (as), na hilo linatokana na kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Na kila kaumu ina wa kuwaongoza… Kisha akasema (as): Katika kila zama kuna Imam mwongozaji anayebainisha, nayo (yaani aya tukufu iliyotajwa hapo juu) ni jibu dhidi ya watu wanaopinga kuwa kuna Imam katika kila zama, na kwamba ardhi haiwi bila ya hujja kama alivyosema Amir al-Mu’mineen (as): Ardhi haiwi bila ya mtu anayesimamisha hoja ya Mwenyezi Mungu, ima kwa kuonekana dhahiri na mashuhuri au kwa woga na kutokuwa mashuhuri, ili hoja na vibainishi vya Mwenyezi Mungu visibatilike.’
**********
Kwa maelezo hayo wapenzi wasikilizaji, mambo tuliyoyasema ni jibu la swali la kipindi cha juma hili, nalo ni kwamba hadithi tukufu kutoka katika madhehebu zote mbili za Sunni na Shia zinabainisha wazi kwamba katika kila zama kuna Imam aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwaongoza wanadamu kwa amri yake, tokea wakati wa Nabii Adam hadi Siku ya Kiama. Na hapa tunauliza swali hili kuwa je, Imam huyu anapasa kuwa na sifa gani? Tutatoa jibu la swali hili katika kipindi kijacho cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain, Inshallah. Tunakushukuruni kwa kuwa pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi hiki ambacho kama kawaida kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Basi hadi wakati huo tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.