Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain 118
Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka hapa mjini Tehran. Hiki ni kipindi cha 118 katika mfululizo wa vipindi hivi vya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambavyo ni vipindi vinavyochambua na kujibu maswali mbalimbali yanayohusiana na itikadi ya dini tukufu ya Kiislamu.
Katika vipindi kadhaa vilivyopita tumekuwa tukijadili suala la Uimamu ambalo ni moja ya misingi ya dini ya haki, na ulazima wa kuwepo Imam mwongozaji katika kila zama, tokea wakati wa Nabii Adam (AS) hadi Siku ya Kiama.
Swali la kipindi cha leo ni, je, ni zipi sifa au masharti anayopasa kuwa nayo Imam wa haki ambaye Mwenyezi Mungu ameapa kutoiacha ardhi bila ya kuwa na Imam wa aina hii, na kwamba Maimamu hao watakuwa hoja yake kwa viumbe na sababu ya kuongoka kwao kama tulivyoona katika vipindi vilivyopita?
Hebu turejee maandiko matakatifu katika kutafuta jibu la swali hili, hivyo basi kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi. Karibuni.
**********
Wapenzi wasikilizaji, isma au kwa ibara nyingine umaasumu ni sharti la kwanza la mtu anayechaguliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Imam wa kuwaongoza viumbe wake kwenye njia nyoofu ili wapate saada ya milele. Tuliashiria sharti hili katika kipindi kilichopita tulipokuwa tukiarifisha maana ya Uimamu kwa kutegemea aya tukufu ya 124 ya Surat al-Baqarah ambapo Mwenyezi Mungu mtukufu anasema: Na Mola wake alipomjaribu Ibrahim kwa matamko, naye akayatimiza, akamwambia: Hakika Mimi nitakufanya uwe mwongozi wa watu. Akasema: Je, na katika kizazi changu pia? Akasema: Ahadi yangu haitawafikia madhalimu.
Kwa hivyo Uimamu ni ahadi ya Mwenyezi Mungu na ahadi hii haiwafikii madhalimu. Imethibiti kwa hoja ya Qur'ani kwamba kila maasi ni dhulma anayoitekeleza mwanadamu kwa madhara yake mwenyewe au kwa madhara ya wenzake, kwa mfano shirki ambayo Mwenyezi Mungu ameitaja katika Qur'ani Tukufu kuwa ni dhulma kubwa.
Imepokelewa katika kitabu cha Amaali cha Sheikh at-Tusi na al-Manaqib cha Ibn al-Maghazili akinukuliwa Ibn Mas'oud kwamba Mtume Mtukufu (saw) alitolea hoja aya hii katika kuthibitisha isma iliyo mbali na shirki. Alisema (saw): 'Katika aya hii tukufu, Mwenyezi Mungu anamwambia Nabii Ibrahim: Mtu anayesujudia sanamu badala ya kunisujudia sitamfanya kuwa Imam. Kisha Mtume (saw) alisema: Na wito uliishia kwangu na kwa ndugu yangu Ali. Kamwe hakuna mmoja wetu aliyesujudia sanamu.'
Kwa kuzingatia upana na ujumla wa matumizi ya neno 'madhalimu’ katika aya tuliyotangulia kuisoma, inabainika wazi kwamba ahadi ya Uimamu unaotoka kwa Mwenyezi Mungu haiwafikii watu waliofanya dhulma katika shirki au maasi, hata kama dhulma hiyo itakuwa imefanywa na mtu katika kipindi fulani cha maisha yake na kisha mtu huyo kutubu na kujirekebisha. Na hili ndilo suala analoashiria Allama Tabatabai katika tafsiri yake ya al-Mizaan ambapo anasema mwishoni mwa aya hii tukufu: 'Aliulizwa mmoja wa walimu wetu (MA) katika kukurubishwa dalili ya aya iliyotajwa na isma ya Imam naye akajibu kwa kusema: Watu wanagawanyika katika makundi manne: Mtu anayedhulumu katika maisha yake yote, mtu asiyekuwa dhalilimu katika maisha yake yote (naye ni maasumu), mtu anayekuwa dhalimu mwanzoni mwa umri wake na sio mwishoni mwake (yaani anayetubu) na mtu nayekuwa kinyume chake. Na Ibrahim (as) ni mtukufu zaidi kuliko kuweza kuuliza Uimamu katika kundi la kwanza na la nne kwa ajili ya kizazi chake (yaani dhalimu katika umri wake wote na mwishoni mwa maisha yake). Kwa hivyo yanabakia makundi mawili (yaani la maasumu na aliyetubu). Na mwenyezi Mungu amekataa mojawapo ya makundi hayo, nalo ni la wale wale watu wanaokuwa madhalimu mwanzoni mwa maisha yao na kutubu mwishoni mwa maisha hayo (yaani dhalimu aliyetubu). Kwa hivyo ni kundi moja tu linalobaki nalo ni la mtu asiyekuwa dhalimu katika umri wake wote.'
Na kundi hili la mwisho ndilo la maasumu aliye na isma kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye kamwe hafanyi dhulma, shirki wala maasi ya aina yoyote ile kama anavyoashiria ukweli huo Mtume Mtukufu (saw) kwa kusema: 'Na wito uliishia kwangu na kwa ndugu yangu Ali. Kamwe hakuna mmoja wetu aliyesujudia sanamu.'
************
Sharti au sifa ya pili ya Imam wa kweli, wapenzi wasikilizaji, ni kuwa anapasa kujiongoza mwenyewe kwa kutegemea mwongoza kutoka kwa Mwenyezi Mungu bila kuhitajia mwongozo wa kiumbe chochote katika viumbe vya Mungu Muumba. Na sifa hii ndiyo ile inayoashiriwa na aya za 35 na 36 za Surat al-Yunus zinazosema: Sema: Je, Yupo katika miungu yenu ya ushirikina anayeongoza kwenye haki? Sema: Mwenyezi Mungu ndiye anayeongoza kwenye haki. Basi, je, anayestahiki kufuatwa ni yule mwenye kuongoza kwenye haki au ni yule asiyeongoka ila aongozwe yeye? Basi mna nini nyinyi? Mnahukumu vipi? Na wengi wao hawafuati ila dhana tu. Hakika dhana haifai kitu mbele ya haki. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wanayoyatenda.
Uzingatia wa kina wa aya hii unatuelekeza katika ukweli huu kwamba Imam wa kweli ambaye anapasa kufuatwa ni yule asiyehitajia uongozi wa mtu mwingine ili apate kuwaongoza wenzake bali ni yule anayoengozwa na Mwenyezi Mungu moja kwa moja na kuwaongoza wanadamu wenzake kwa amri ya Mwenyezi Mungu.
Na Aya ya 36 ya Surat al-Yunus tuliyoisoma hivi punde inasema kuwa siri ya kuwekwa sharti hili katika Imam masumu na wa haki ni kwamba kufuatwa mtu asiyeongozwa na Mwenyezi Mungu kwa hakika ni kufuata dhana tu ambayo haifai kitu mbele ya haki.
Na hapa tunatambua na kufahamu sifa ya tatu ya Imam wa kweli nayo ni kuwa na yakini na aya za Mwenyezi Mungu na kupata mwongozo wa moja kwa moja. Na suala hili ndilo linaloashiriwa na kauli ya Mwenyezi Mungu katika aya ya 24 ya Surat as-Sajda inayosema: Na tukawafanya miongoni mwao maimamu wanaoongoza kwa amri yetu, waliposubiri na wakawa na yakini na Ishara zetu. Na yakini wapenzi wasikilizaji, ni miongoni mwa matunda yanayopatikana kutokana na msaada maalumu wa Mwenyezi Mungu kwa waja wake wema ambao wanaweza kuonyeshwa pia ufalme wa mbinguguni. Mwenyezi Mungu anasema katika aya za 74 na 75 za Surat al-An'aam: Na pale Ibrahim alipomwambia baba yake, Azar: Unayafanya masanamu kuwa ni miungu? Hakika mimi nakuona wewe na watu wako mmo katika opotofu ulio wazi. Na kadhalika tulimwonyesha Ibrahim ufalme wa mbingu na ardhi, ili awe miongoni mwa wenye yakini.
Imepokelewa katika Tafsiri ya Ali bin Ibrahim (MA) mwishoni mwa aya hii tukufu kwamba Imam Jaffar (as) alisema: 'Alifunuliwa ardhi na watu wanaoibeba, mbingu na waliomo pamoja na malaika wanaoibeba na Arshi na aliye juu yake. Mwenyezi Mungu pia alimfanyia hayo yote Mtume Mtukufu (saw) na Amir al-Mu'mineen (as).
Imepokelewa katika Usuul al-Kafi kutoka kwa Amir al-Mu'mineen (as) kwamba alibainisha hadithi inayoashiria athari ya Mwenyezi Mungu kuwaonyesha mbingu Maimamu anaowateua kuwaongoza wanadamu kwa kusema: 'Kwa utukufu wake Mwenyezi Mungu na nuru Yake, nyoyo za waumini zilipata kuona…., Naye ni uhai na nuru ya kila kitu, ametakasika na ametukuka juu kabisa na hayo wanayoyasema. Hivyo basi wale wanaobeba Arshi ni maulamaa ambao Mwenyezi Mungu amewapa elimu yake…. Na kiumbe chochote alichokiumba Mwenyezi Mungu hakitoki nje ya mambo haya manne katika mbingu ambazo aliwaonyesha waja wake wema na bora na pia kuomuonyesha rafiki yake (as)…. Na kwa uhai wake kunako nyoyo zao na kwa nuru yake waliweza kuongoka kuelekea maarifa yake.'
**********
Wapenzi wasikilizaji, tunafupisha mambo tuliyojifunza katika kipindi cha juma hili ambacho kimehusu sifa tatu muhimu anazopasa kuwa nazo Imam maasumu aliyechaguliwa na Mwenyezi Mungu, ambaye amejipa jukumu la kutoiacha ardhi bila ya kuwa na Imam mwema na mwangozaji wa waja wake, kwa kusema kuwa sifa hizo ni, kwanza anapasa kuwa ni maasumu kutokana na isma inayotoka kwake Mungu Muumba. Pili anapasa kutohitajia uongozi wa viumbe wengine bali anapasa kujiongoza mwenyewe na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na tatu, anapasa kuwa miongoni mwa waja wema walio na yakini na ambao Mwenyezi Mungu amewaidhinisha na kuwaridhia kwa kuwaonyesha siri za mbingu zake.
Tutazungumzia sifa nyingine za Imam mwongozaji katika kipindi kijacho cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain Inshallah. Kipindi hiki kama tulivyotangulia kusema hukujieni daima kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Basi hadi wakati huo tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.