Alkhamisi, tarehe 28 Machi, 2019
KLeo ni Alkhamisi tarehe 21 Rajab 1440 Hijria inayisadifiana na Machi 28 mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 1192 iliyopita mwezi wa Rajab mwaka 284 Hijiria, alifariki dunia Abu Hatam, Sahl bin Muhammad Sajestani. Abu Hatam alikuwa ametabahari katika elimu ya Qur'ani, hadithi, fasihi na mashairi. Mbali na kuwa alikuwa akiisoma Qur'ani Tukufu na kuifundisha kwa mapenzi makubwa, Abu Hatam pia alijishughulisha na masuala ya kijamii. Msomi huyo ameacha vitabu vingi miongoni mwavyo ni I'irabul Qur'an', na Akhlaqul Insan.
Siku kama ya leo miaka 151 iliyopita, alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Russia Alexei Maximovich Peshkov aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Maksim Gorky. Gorky alilazimika kusoma na wakati huo huo akifanya kazi ili kuweza kukidhi mahitaji yake ya maisha kutokana na umaskini mkubwa uliokuwa ukimkabili. Alianza kuandika riwaya haraka sana na kufanikiwa kuchapisha riwaya yake ya kwanza katika gazeti la Tbilisi wakati alipokuwa akifanya kazi katika sekta ya reli. Miaka miwili baadaye mwandishi Gorky alipata mafanikio makubwa ambapo alichapisha riwaya yake katika kitabu na taratibu akaanza kuingia katika safu ya waandishi wakubwa na mashuhuri duniani.
Katika siku kama leo miaka 80 iliyopita, baada ya kupita karibu miaka miwili na nusu ya vita vya ndani huko Uhispania, wapigania usultani chini ya uongozi wa Jenerali Francisco Franco waliwashinda wapigania jamhuri na kudhibiti Madrid, mji mkuu wa nchi hiyo. Machafuko yalianza huko Uhispania wakati Alphonso wa 13 mfalme dikteta wa nchi hiyo alipolazimika kujiuzulu kufuatia mashinikizo ya wapigania jamhuri na baadaye mfumo wa jamhuri ukaasisiwa huko Uhispania.
Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita mwandishi wa Kiingereza, Bi Virginia Woolf aliaga dunia kwa kujiua. Woolf alizaliwa mwaka 1882 na alianza kufaidika na maktaba binafsi ya baba yake ambaye alikuwa mwandishi na mkosoaji wa fasihi, akiwa bado mtoto. Virginia Woolf alianza kuandika vitabu mapema na miongoni mwa vitabu hivyo ni Mrs. Dalloway, The Waves na To the Lighthouse. Hata hivyo maradhi ya kiakili na kinafsi yaliyompata akiwa bado kijana yaliendelea kumuandama na hatimaye mwandishi huyo wa Uingereza aliamua kujiua katika siku kama hii ya leo.