Mar 29, 2019 00:02 UTC
  • Ijumaa, tarehe 29 Machi,  2019

Leo ni ijumaa tarehe 22 Rajab 1440 Hijria sawa na Machi 29 mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 446 iliyopita, yaani tarehe 29 Machi 1573 Mfalme Charles wa Tisa wa Ufaransa alitoa amri ya kihistoria iliyojulikana kama amri ya uhuru, ambayo ilikuwa kwa maslahi ya Wakristo wa madhehebu ya Protestanti. Kwa mujibu wa amri hiyo, Waprotestanti wa Ufaransa ambao walijipatia ushindi kwenye vita vya nne dhidi ya Wakatoliki wa nchi hiyo, walikuwa huru kufanya sherehe, ibada na misa zao nchini humo. Vita vya nne vya kidini kati ya Wakatoliki na Waprotestanti vilianza tarehe 16 Julai mwaka 1572 na vilikuwa maarufu kwa jina la Vita vya La Rochelle.

Mfalme Charles wa Tisa

Miaka 343 iliyopita katika siku kama ya leo vita baina Poland na Ufalme wa Othmania vilifikia tamati kwa ushindi wa Ufalme huo na kutekwa sehemu ya ardhi ya Ukraine iliyokuwa chini ya utawala wa Poland.

Siku kama ya leo miaka 247 iliyopita, alifariki dunia Emmanuel Swedenborg, aliyekuwa mwanafikra mkubwa na msomi wa Sweden. Swedenborg alizaliwa mwaka 1688 na baada ya kubobea kwenye taaluma ya hesabati, aliweza kuwa mhandisi mahiri nchini humo. Swedenborg hakutosheka na elimu hiyo na badala yake akaongeza juhudi kubwa na kutokea kuwa mtaalamu pia kwenye elimu ya falsafa na irfani. Msingi wa falsafa ya msomi huyo ulikuwa kujitenga na dunia ya kimaada na kuingia zaidi katika ulimwengu wa kimaanawi. Kwa msingi huo Swedenborg aliamini kuwa kadiri mwanadamu anavyosafisha roho yake ndivyo anavyomuelewa na kumjua zaidi Mwenyezi Mungu. Mtaalamu huyo aliandika vitabu zaidi ya 50 kwa ajili ya kuweka wazi falsafa yake.

Emmanuel Swedenborg

Siku kama ya leo miaka 212 iliyopita, inayosadifiana na 27 Rajab 1228 Hijria, alifariki dunia Allamah Sheikh Jaafar Kaashiful Ghitwa, mwanachuoni mashuhuri wa Kiislamu mjini Najaf, Iraq. Allamah Kashiful Ghitwa alikuwa mwanachuoni aliyebobea na kutopea kwenye fani mbalimbali za kielimu kama vile fiqhi, usuulul fiqh, tafsiir ya Qur'ani na hadith. Mwanachuoni huyo ameandika vitabu vingi vikiwemo, Kashful Ghitwaa, Bughyatu Twalib na al A'qaaidul Jaafariyya. 

Allamah Sheikh Jaafar Kaashiful Ghitwa

Na katika siku kama hii ya leo miaka 117 iliyopita sawa na tarehe 29 Machi mwaka 1902 Miladia, alizaliwa mwandishi wa Kifaransa kwa jina la Marcel Ayme. Katika masomo yake ya awali Ayme alisomea uhandisi hata hivyo kutokana na kupatwa na maradhi aliachana na taaluma hiyo. Baadaye alijishughulisha na uandishi wa magazeti na taratibu akaanza kujihusisha na uandishi wa riwaya ambapo alitokea kuwa mashuhuri katika uwanja huo. Marcel Ayme ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwake ni "Beautiful Image", na "The Green Mare".

Marcel Ayme