Apr 01, 2019 20:31 UTC
  • Jumanne tarehe Pili Aprili 2019

leo ni Jumanne tarehe 26 Rajab 1440 Hijria sawa na tarehe Pili Aprili mwaka 2019.

Miaka 1443 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Abu Talib, ami na mtetezi mkubwa wa Mtume SAW katika mji wa Makka. Baada ya kufariki Abdul Muttalib, babu mtukufu wa Nabii Muhammad SAW, Abu Talib ndiye aliyebeba jukumu la kumlea Mtume na akawa bega kwa bega na mwana huyo wa nduguye katika hali zote. Baada ya kupewa Utume Nabii Muhammad SAW, Abu Talib hakumwacha mkono mtukufu huyo na alisimama imara kukabiliana na washirikina wa Kiqureishi. Baada ya kufariki dunia Abu Talib, washirikina walizidisha maudhi na manyanyaso dhidi ya Bwana Mtume SAW kiasi kwamba kutokana na hali ngumu mno iliyomkabili, hatimaye kwa amri ya Mwenyezi Mungu, mtukufu huyo aliondoka Makka na kuhamia Madina ambako aliasisi utawala wa kwanza wa Kiislamu.

Katika siku kama ya leo miaka 214 iliyopita, alizaliwa huko nchini Denmark, Hans Christian Andersen malenga, mwandishi na msimulizi wa visa maarufu vya watoto. Andersen ambaye alikuwa mtoto wa bwana mmoja maskini na fundi viatu, alihamia Copenhagen mji mkuu wa Denmark na kuanza kucheza michezo ya kuigiza. Baada ya muda, Hans Andersen alianza kutunga visa na kuwa mashuhuri baada ya kuandika kitabu chake cha kwanza cha hadithi alichokipa jina la "Fairy Tales, Told for Children" mnamo mwaka 1838.

Hans Christian Andersen

Miaka 37 iliyopita katika siku kama hii ya leo, vikosi vya jeshi la majini la Argentina vilivamia visiwa vya Falkland kwa jina jingine (Malvinas) na kuvidhibiti visiwa hivyo vya kiistratejia vilivyoko kusini mashariki mwa nchi hiyo. Visiwa vya Falkland ambavyo kwa lugha ya Kiargentina vinatamkwa kama Malvinas, viligunduliwa katika karne ya 16 na kukaliwa kwa mabavu na Uingereza mwaka 1832.

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, vibaraka wa utawala wa Baath uliokuwa ukiongozwa na Saddam Hussein walivamia na kuvunjia heshima Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib A.S katika mji mtakatifu wa Najaf na ya Imam Hussein A.S huko katika mji mtukufu wa Karbala, sambamba na kuyakandamiza mapambano ya Waislamu wa kusini mwa Iraq. Wananchi wa Iraq walianzisha mapambano ya kuuondoa madarakani utawala wa kidikteta Saddam Hussein baada ya muungano wa vikosi vya majeshi ya nchi kadhaa kutekeleza oparesheni ya kuwaondoa wanajeshi wa Iraq katika ardhi ya Kuwait. Wakati huo wanajeshi wa Marekani walisitisha oparesheni zao za kijeshi na kuungana na wanajeshi wa Saddam ili kumwaga damu za Wairaqi waliokuwa wakiendesha mapambano huku wakiwa kwenye saumu.

Saddam Hussein alishambulia na kuvunjia heshima maeneo matakatifu ya Iraq

Siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, aliaga dunia Papa John Paul II aliyekuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani. Papa John Paul II alizaliwa mwaka 1920 huko Poland na kufikia daraja ya uchungaji baada ya kuhitimu masomo ya dini. Mwaka 1964 Papa John Paul alikuwa askofu wa mji wa Kraku huko Poland na miaka mitatu baadaye akawa Kadinali. Hatimaye mwaka 1978 John Paul wa Pili aliteuliwa kushika wadhifa wa ngazi ya juu zaidi wa kanisa Katoliki, yaani Papa. Papa John Paul wa Pili alikuwa mfuasi wa mazungumzo baina ya dini mbalimbali hususan kati ya Uislamu na Ukristo. Alikuwa akipinga vikali utoaji mimba na ndoa za watu wa jinsia moja na ufisadi wa kimaadili kwa ujumla uliotanda katika ulimwengu wa Magharibi. Aidha alikosoa vikali mashambulio ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iraq.

Papa John Paul II