Jumapili, Aprili 21, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 15 Sha'aban 1440 Hijiria, sawa na tarehe 21 Aprili 2019 Miladia.
Leo tarehe Mosi Ordibehesht katika kalenda ya mwaka wa Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi Sheikh Muslihuddeen Saadi Shirazi malenga, mshairi na mwalimu stadi wa tungo za mashairi na nathari wa Kifarsi. Saadi Shirazi alizaliwa karibu mwaka 606 Hijria Qamariya katika familia ya kielimu kwenye mji wa Shiraz ulioko kusini mwa Iran na baada ya kukipitisha kipindi cha utoto na kuinukia kwake katika mji alikozaliwa wa Shiraz, akiwa kijana Saadi aliamua kwenda katika mji wa Baghdad huko Iraq. Akiwa huko alisoma katika shule ya Nidhamiya na baadaye kufanya safari katika maeneo ya Sham, Hijaz, Roma na maeneo mengine ya dunia. Katika safari zake hizo, malenga huyo mashuhuri alifanikiwa kufahamiana na jamii mbalimbali na kuona mengi yaliyoimarisha kipawa chake cha kutunga mashairi. Saadi Shirazi ni miongoni mwa malenga na washairi wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Saadi Shirazi ameandika vitabu kadhaa, muhimu zaidi ni kile cha tungo cha Bustan na kitabu chake cha nathari cha Golestan.
Siku kama ya leo miaka 1190 iliyopita, Egbert Mfalme wa Kwanza wa Uingereza alichukua madaraka baada ya vita vya muda mrefu. Kabla ya hapo Uingereza ilikuwa ikiongozwa na wafalme wa kiukoo huku ikiwa imegawika katika sehemu kadhaa za kijiografia na kila mtawala akitawala eneo lake maalumu. Egbert aliyekuwa mfalme wa Wessex, eneo lililokuwa Kusini mwa Uingereza ya sasa, baada ya kupambana na watawala wa kitabaka na kuwashinda, mwaka 829 alifanikiwa kuingia madarakani akiwa Mfalme wa Kwanza wa Uingereza na kuasisi silsila ya utawala wa Wasaxoni wa Magharibi.
Siku kama ya leo mika 1185 iliyopita alizaliwa Imam Mahdi (af) mwokozi wa ulimwengu katika mji wa Samarra kaskazini mwa Baghdad mji mkuu wa Iraq. Yeye ni mwana mpendwa wa Imam Hassan Askari (as) ambaye ni mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu (saw). Miongoni mwa lakabu mashuhuri za Imam huyo wa Zama ni Mahdi, ambayo ina maana ya mtu aliyepewa hidaya na kuongozwa na Qaim, kwa maana ya msimamishaji mapambano. Imam Mahdi alipitisha miaka mitano ya kwanza ya uhai wake akiwa na baba yake mpendwa Imam Askari (as). Alichukua jukumu la kuwaongoza Waislamu kama Imam baada ya kuuawa shahidi baba yake huyo mtukufu na kisha kughibu machoni pa walimwengu kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu. Kwa muda wa miaka 69 mtukufu huyo alikuwa akiwasiliana na kuwaongoza Waislamu kupitia wawakilishi wake maalumu. Baada ya hapo na kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Imam Mahdi alienda kwenye ghaiba kubwa na ya muda mrefu ambapo atadhihiri tena ulimwenguni wakati muwafaka ambao Mwenyezi Mungu ataona unafaa. Atakapodhihiri humu duniani, ataujaza ulimwengu kwa uadilifu na usawa baada ya kujaa dhuma na uonevu.

Siku kama ya leo miaka 1111 iliyopita, Ali bin Muhammad Samori mwakilishi wa nne wa Imam Mahdi (af), ambaye alikuwa mwanazuoni mcha-Mungu na mwenye fadhila nyingi aliaga dunia. Baada ya kwenda ghaiba, Imam kwa makumi ya miaka alikuwa akiwasiliana na watu kupitia wawakilishi maalumu. Katika mazungumzo yake ya mwisho na Imam wa Zama (af) Samori alipokea barua kutoka kwake ambayo ilikuwa ikisisitiza kwamba hangemteua mwakilishi mwingine baada yake. Baada ya kuaga dunia Samori, Imam aliwataka watu kuwafuata wanazuoni wajuzi wa masuala ya dini kuhusiana na mambo mapya ambayo yangejitokeza.
Siku kama ya leo miaka 603 iliyopita, alifariki dunia Ibn-e Hejjah Hamavi malenga na mwandishi wa vitabu wa karne ya tisa Hijiria. Alizaliwa Sham, (Syria ya leo) na akiwa kijana akawa amehifadhi Qur'ani yote. Aidha alishiriki masomo ya fasaha kwa maulama wakubwa wa zama hizo kiasi cha kutokea kuwa malenga mkubwa na maarufu. Mashairi ya Ibn-e Hejjah Hamavi yalipata umashuhuri katika zama hizo na moja ya kitabu chake ni 'Alkhazatul-Adab.'
Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, Allamah Muhammad Iqbal Lahori mwanafikra, mwanafalsafa na malenga wa Kiislamu aliaga dunia huko Bara Hindi. Alizaliwa mwaka 1873 katika mji wa Sialkot kwenye jimbo la Punjab. Baada ya kumaliza masomo ya awali na ya juu na kupata shahada ya uzamili, Allamah Muhammad Iqbal Lahori alielekea nchini Ujerumani na baadaye Uingereza kwa lengo la kujiendeleza katika elimu ya falsafa na kubaki huko kwa kipindi cha miaka minne. Malenga huyo alianza kutunga mashairi akiwa katika masomo yake ya sekondari. Baada ya kurejea India, Iqbal Lahori alianza kuwaamsha Waislamu wa nchi hiyo na kufanya jitihada za kuwaunganisha pamoja huku akibainisha fikra na mitazamo yake kupitia beti za mashairi. Mwanafalsafa huyo anahesabiwa kuwa mmoja wa waanzilishi na waasisi wa Pakistan huru.
Na siku kama ya leo miaka 39 iliyopita aliaga dunia Sohrab Sepehri malenga na mchoraji mashuhuri wa Kiirani. Sohrab alizaliwa mwaka 1307 Hijria Shamsiya katika mji wa Kashan katikati mwa Iran. Awali malenga huyo wa Kiirani alianza kufundisha na baada ya hapo alijiunga na taaluma ya sanaa. Vilevile alikuwa na kipaji kikubwa katika masuala ya uchoraji. Kazi za malenga na mchoraji huyo wa Kiirani zilimpatia tuzo na zawadi nyingi katika maonyesho mbalimbali yaliyofanyika ndani na nje ya Iran. Shairi lake la kwanza alilitunga mwaka 1330 Hijria Shamsiya na kulipa jina la The Death of Colours.