Apr 25, 2019 02:17 UTC
  • Alkhamisi, 25 Aprili, 2019

Leo ni Alkhamisi tarehe 19 Sha'aban 1440 Hijria mwafaka na tarehe 25 Aprili, 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1434 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, kulijiri vita vya Bani Mustaliq. Mustaliq ni moja ya makabila ya Khuza'a ambayo yalihamia katika viunga vya mji wa Makka, muda mrefu katika historia. Viongozi wa kabila hilo walieneza ibada ya kuabudu masanamu. Baada ya Waislamu kusimamisha dola ya Kiislamu mjini Madina, kabila hilo la Mustaliq ambalo liliendelea kuabudu masanamu, lilitangaza utayarifu wake kwa ajili ya kupambana na Waislamu. Kwa ajili hiyo Mtukufu Mtume (saw) akiwa na kundi la wafuasi wake alilazimika kupambana na kabila hilo na hatimaye kulishinda vibaya. ***

Vita vya Bani Mustaliq

Miaka 527 iliyopita (kwa mujibu wa waaandishi wa historia) serikali ya mwisho ya Kiislamu barani Ulaya ilisambaratika huko Granada. Baada ya kudhihiri dini ya Uislamu na kupanua mamlaka yake katika maeneo ya Asia na kaskazini mwa Afrika, jeshi la Waislamu liliingia kusini magharibi mwa Ulaya kupitia lango bahari la Jabal Tariq (Gibraltar) na kulitawala eneo hilo kwa kipindi cha karne 8. Eneo hilo ambalo kwa sasa linaitwa Uhispania, wakati huo lilijulikana kwa jina la Andalusia. Katika kipindi cha ustawi wa ustaarabu wa Kiislamu eneo la Granada lilikuwa kituo kikuu cha ustaarabu huo na makao makuu ya kueneza Uislamu hususan barani Ulaya. Dola la Kiislamu la Andalusia liliangushwa kupitia njia ya kueneza ufuska na maovu baina ya watawala na makhalifa wa wakati huo. ***

Mabaki ya Ustaarabu wa Kiislamu katika mji wa Granada nchini Uhispania

Katika siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, Wamarekani laki mbili walifanya maandamano mjini Washington wakiendeleza upinzani wao dhidi ya mashambulizi ya nchi hiyo huko Vietnam. Maandamano hayo yalikuwa miongoni mwa vielelezo vikubwa vya upinzani wa wananchi wa Marekani dhidi ya siasa za kichokozi za serikali ya nchi hiyo huko Vietnam. Katika vita vya Vietnam vilivyoanza mwaka 1964 Marekani ilituma askari laki tano nchini humo ambako makumi ya maelfu miongoni mwao waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Kwa sababu hiyo wananchi wa Marekani walizidisha upinzani dhidi ya vita hivyo na mwaka 1975 Marekani ililazimika kufunga virago na kuondoka Vietnam kutokana na mashinikizo ya ndani na ya kimataifa na kushindwa mara kwa mara jeshi la nchi hiyo katika medani za vita. ***

Vita vya Vietnam

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita,  inayosadifiana na tarehe 5 Ordibehesht mwaka 1359 Hijiria Shamsia, Marekani ilishambulia kijeshi ardhi ya Iran kwa kutumia helikopta na ndege kadhaa za kivita. Serikali ya Marekani ilifanya mashambulizi hayo baada ya kushindwa njama zake mbalimbali za kutaka kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu wa Iran. Lengo la mashambulio hayo lilikuwa ni kutaka kuwakomboa majasusi wake waliotiwa mbaroni wakati wa kutekwa ubalozi wa Marekani hapa nchini uliokuwa pango la kijasusi. Licha ya kuweko mipango makini, kutumiwa vyombo vya kisasa kabisa na mazoezi mengi yaliyofanywa katika eneo linalofanana na hilo ili kuhakikisha operesheni hiyo inafanikiwa, lakini mashambulizi hayo yalikatishwa na tufani kubwa ya mchanga iliyotokea Tabas na kupelekea kuanguka baadhi ya ndege, kushika moto helikopta za Marekani na kufa baadhi ya askari wa nchi hiyo huku waliobakia wakiikimbia ardhi ya Iran. ***

Tukio la Tabas