May 05, 2019 02:29 UTC
  • Jumapili, 5 Mei 2019

Leo ni Jumapili tarehe 29 Sha'aban 1440 Hijiria sawa na tarehe tano Mei 2019 Miladia.

Siku kama ya leo tarehe 15 Ordebehesht Hijiria Shamsia ni siku ya kumuenzi Sheikh Swaduq, msomi mashuhuri wa Kishia. Abu Ja'far Muhammad Ibn Ali ibn Babawayh maarufu kwa jina la Sheikh Swaduq alizaliwa mjini Qum yapata mwaka 306 Hijiria katika familia ya wasomi. Akiwa kijana mdogo alianza kujifunza elimu ya dini ya Kiislamu na kufanikiwa kukwea marhala za elimu kutoka kwa baba yake na maulama wengine wa zama zake. Baada ya hapo alifikia daraja za juu katika elimu, huku akifanya safari katika maeneo tofauti kwa ajili ya kusoma zaidi na kukusanya hadithi ambapo inaelezwa kuwa alipata kusoma kwa wasomi zaidi ya 200 wa zama zake. Baada ya kufanya safari mjini Baghdad, wasomi wa mji huo walivutiwa naye sana na wakapata kusoma kwake. Miongoni mwa wanafunzi wake ni pamoja na Sheikh Al-Mufid, Hassan Bin Muhammad Qumi, Alamul-Huda Sayyid Murtadha, na wengine wengi. Ameacha athari nyingi ambazo miongoni mwazo ni 'Man laa Yahdhuru al-Faqihi' chenye juzuu nne ambacho ni kati ya vitabu mashuhuri kwa Waislamu wa Shia na chenye hadithi 6000 na pia kitabu cha 'Madinatul-Ilm' chenye juzuu 10, 'Aamaal, Khiswaal', 'Uyuunu Akhbaar al-Ridha (as)' na 'Ilalu ash-Sharaaii'.

Kaburi alikozikwa Sheikh Swaduq

Siku kama ya leo miaka 1221 iliyopita alifariki dunia fadhl Bin Dukayn maarufu kwa jina la Ibn Naim, mtaalamu wa hadithi, sheria za Kiislamu na mwanahistoria mahiri wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 130 Hijiria nchini Iraq kama ambavyo alikuwa mpokezi mkubwa wa hadithi mwenye itibari na kuheshimika na wasomi wa Kiislamu. Kitabu cha 'As-Swalaat' ni miongoni mwa athari za Abu Naim, kama ambavyo kitabu cha 'Al-Manaasik' na 'Masaail al-Fiqhi' vinanasibishwa kwake.

Bin Dukayn maarufu kwa jina la Ibn Naim

Siku kama ya leo miaka 201 iliyopita, alizaliwa Karl Marx mwanafalsafa wa Kijerumani na mwasisi wa shule ya fikra za Kimax. Marx awali alipata mafunzo katika taaluma ya sheria na baadaye akajitosa katika uwanja wa historia na falsafa. Karl Marx wakati fulani alikuwa mhariri wa gazeti moja na mwaka 1848 aliwasilisha maoni na mitazamo yake katika kitabu alichokiita "Manifesto ya Ukomonisti" kwa kushirikiana na mwanafilosofia mwenzake Friedrich Engels. Aidha miaka miwili baadaye, Karl Marx alihamishwa kutoka Ujerumani kutokana na harakati za kisiasa na kumalizia umri wake nchini Uingereza. Kitabu kingine muhimu kilichoandikwa na mwanafilosofia huyo ni kile alichokipa jina la Capital. Karl Marx alifariki dunia mwaka 1883, lakini fikra zake zikaenea katika harakati za hapa na pale kwa zaidi ya nusu karne ulimwenguni, kwa kadiri kwamba, fikra na utabiri wake usio sahihi uliweza kudhihiri wazi zaidi mwanzoni mwa muongo wa 90 miladia wakati wa kusambaratika nchi kubwa zaidi ya Kikomonisti duniani yaani Urusi ya zamani. 

Karl Marx

Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita alifariki dunia Napoleon Bonaparte mfalme aliyekuwa na nguvu wa Ufaransa, akiwa uhamishoni. Napoleon alizaliwa mwaka 1769 na kuchukua madaraka makubwa ya uongozi baada ya mapinduzi ya Ufaransa mwaka 1789, ambapo aliifanya nchi hiyo ishinde vita na nchi nyingi za Ulaya. Baada ya kuwa mfalme wa Ufaransa, Napeleon alibadilika na kuwa mtawala aliyependa kujitanua na kuzivamia nchi nyingine katika maeneo mbalimbali duniani. Kwa ajili hiyo katika kipindi cha utawala wake alipigana vita kadhaa na nchi nyingine na kukalia kwa mabavu maeneo mengi ya bara Ulaya.

Napoleon Bonaparte

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, hayati Imam Ruhullah Khomeini akiwa na umri wa miaka 42, alitoa taarifa yake ya kwanza ya kisiasa akiwataka wananchi kusimama na kuanza harakati kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Katika taarifa hiyo Imam Khomeini alichunguza hali ya miaka ya nyuma, ya kipindi hicho na mustakbali wa wananchi wa Iran na Waislamu kwa ujumla na kusema: Kuanzisha harakati na mapambano kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ndiyo njia pekee ya kurekebisha hali ya dunia. Alisema suala hilo ndiyo falsafa ya kutumwa Manabii wote wa Mwenyezi Mungu. Imam pia aliashiria hali mbaya ya Waislamu na wananchi wa Iran na kukumbusha majukumu mazito ya wanazuoni wa dini na athari mbaya za tabaka hilo kughafilika na masuala ya kisiasa. Katika taarifa hiyo Imam Khomeini alipiga kengele ya hatari na kuwaamsha Waislamu husuan wanafunzi wa vyuo vya kidini kuhusu umuhimu wa kusimama na kuanza mapambano ya kurekebisha umma.

Imam Khomeini (MA)

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita alifariki dunia Bi Nosrat Amin, maarufu kwa jina la 'Hajiyeh Seyyedeh Nosrat Begum Amin' mwanamke wa kwanza kufikia daraja ya ijtihadi katika ulimwengu wa Kiislamu. Bi Amin alizaliwa mwaka 1265 Hijiria Shamsia sawa na 1308 Hijiria mjini Isfahan nchini Iran. Alianza kujifundisha Qur'ani na lugha ya Kiarabu katika maktaba ya mji huo akiwa na umri wa miaka minne, ambapo aliinukia katika maarifa ya dini huku kukiwa hakuna mwanamke yeyote aliyekuwa akisoma masomo hayo. Aidha alilipa umuhimu mkubwa suala la elimu ya dini yakiwemo masomo ya fiqhi na usulu fiqhi. Miongoni mwa walimu wake wakubwa wa elimu ya fiqhi na usulu fiqhi alikuwa Ayatullah Najaf Abadi. Aidha Bi Nosrat Amin alitabahari katika elimu ya irfan (ya kumjua Mwenyezi Mungu) ambapo aliweza kudiriki siri nyingi za kimaanawi. Katika uwanja huo ushahidi wa athari ya tafsiri yake ni kitabu cha Arbaiin al-Haashimiyyah na pia Nafahaatu a-Rahmaaniyyah. Baada ya kuchapisha kitabu cha Arbaiin al-Haashimiyyah alipewa daraja ya ijtihad na Ayatullah Haeri Yazdi, Ayatullah Sayyid Mohammed Kazem Yazdi na Ayatullah Agha Mirza Shirazi. Aidha baada ya kushiriki mtihani wa maulama na maraajii wa kidini wa wakati huo yaani Ayatullah Sheikh Abdulkarim Qumi na Ayatullah Sayyid Muhammad Kadhim Shirazi, akatunukiwa daraja ya ijtihadi na uwezo wa kufahamu sheria za kidini kutoka kwa wanazuoni hao na hivyo kuwa mwanamke wa kwanza mujtahid katika ulimwengu wa Kiislamu.

Bi Nosrat Amin

 

Tags