Jun 15, 2019 04:18 UTC
  • Jumamosi, tarehe 15 Juni, 2019

leo ni Jumamosi tarehe 11 Shawwal 1440 Hijria sawa na tarehe 15 Juni mwaka 2019.

Tarehe 11 Shawwal miaka 1443 iliyopita Mtume Muhammad (S.A.W) alielekea katika mji wa Twaif karibu na Makka kwa lengo la kuwalingania Uislamu watu wa kabila la Thaqif. Safari hiyo ya Mtume mtukufu ilifanyika katika kipindi ambacho alikuwa ameondokewa na ami yake na mlezi wake kipenzi Abu Twalib, jambo lililowafanya Maquraishi wa Makka wazidishe maudhi na manyanyaso dhidi ya Mtume Muhammad (S.A.W) na wafuasi wake. Hivyo ilitarajiwa kuwa, iwapo wakazi wa Twaif wangekubali Uislamu, mji huo ungeweza kuwa kituo na makazi salama kwa Waislamu waliokuwa wakidhulumiwa wa Makka. Hata hivyo viongozi wa kabila la Thaqif sio tu kwamba hawakumwamini Mwenyezi Mungu Mmoja na risala ya Mtume Muhammad (S.A.W), bali pia baadhi ya watu wa kabila hilo walimfanyia maudhi, dhihaka na kumjeruhi Mtume mtukufu.

Ramani ya eneo la Twaif

Katika siku kama ya leo miaka 953 iliyopita kwa mujibu wa nukuu za baadhi ya wanahistoria aliaga dunia Abdul Aziz Andalusi aliyekuwa mtaalamu wa lugha ya Kiarabu na mwanahistoria mashuhuri wa karne ya 5 Hijria. Andalusi alikuwa hodari katika elimu nyingi za wakati huo na aliandika vitabu vingi katika taaluma mbalimbali. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo wa Kiislamu ni Sherh Amthal Abu Ubaida" na Sherh Nawadirul Qaali.

Tarehe 15 Juni miaka 311 iliyopita harakati ya wapigania uhuru wa Scotland ilikandamizwa vikali na Uingereza. Uingereza daima imekuwa ikifanya jitihada za kuiunganisha Scotland na ardhi ya kaskazini mwa nchi hiyo. Hata hivyo harakati za mapambano za Wascotland zilipinga vikali suala hilo. Hata hivyo mwaka 1707 mabunge ya nchi hizo mbili yaliunganishwa. Suala hilo liliwakasirisha sana Wascotland walioanzisha harakati nyingine ya mapambano mbayo ilikandamizwa vikali katika siku kama ya leo hapo mwaka 1708.

Na tarehe 15 Juni miaka 171 iliyopita Kansela wa Ujerumani wa wakati huo aliufanya mji wa kihistoria na mashuhuri wa Berlin kuwa mji mkuu wa nchi hiyo. Kuchaguliwa Berlin kuwa kituo cha utawala wa Ujerumani kulifanyika baada ya kutekelezwa mpango wa kuiunganisha Ujerumani, ambao mwasisi wake alikuwa Bismark.

Otto von Bismarck

 

Tags