Jun 23, 2019 02:59 UTC
  • Jumapili, Juni 23, 2019

Leo ni Jumapili tarehe 19 Mfunguo Mosi Shawwal, mwaka 1440 Hijria, inayosadifiana na tarehe 23 Juni mwaka 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1175 iliyopita alifariki dunia Ya'qub ibn al-Layth al-Saffar, mwasisi wa silsila ya utawala wa Masaffari nchini Iran, katika mji wa Gondēshāpūr moja ya miji ya zamani ya Iran. Sifa za Ya'qub ibn al-Layth al-Saffari katika ujana wake zilimfanya kuwavutia wananchi na kwa muda fulani wakazi wa mji wa Sistan, kusini mashariki mwa Iran, walimfanya kuwa kiongozi wao. Baada ya kushika nyadhifa tofauti na kwa msaada wa wafuasi wake alifanikiwa kudhibiti miji kadhaa  na kuanzisha utawala mmoja katika maeneo ya Sistan. Hatimaye mwaka 261 Hijiria, Ya'qub ibn al-Layth al-Saffari na akitumia jeshi kubwa, alielekea mjini Baghdad, uliokuwa mji mkuu wa watawala wa Bani Abbas. Hata hivyo alishindwa na majeshi ya Bani Abbas na kulazimika kurejea nyuma. Baada ya kushindwa huko na akiwa katika kuandaa jeshi kwa ajili ya kufanya shambulizi jingine katika mji wa huo, Ya'qub ibn al-Layth aliugua na kufariki dunia.

Ya'qub ibn al-Layth al-Saffar

Siku kama ya leo miaka 1099 iliyopita liliundwa bunge la kwanza duniani huko Iceland. Bunge hilo ambalo wawakilishi wake walikuwa wakichaguliwa na wananchi kupitia masanduku ya kura, lilikuwa na kazi ya kuisaidia serikali kifikra. Bunge la zamani zaidi duniani kuwa na mfumo wa hivi sasa ambapo mabunge yana uwezo na madaraka maalumu, lilianza kazi zake nchini Uingereza katikati ya karne ya 13.

Siku kama ya leo miaka 1006 iliyopita yaani tarehe 19 Shawwal 434 alizaliwa Abu Zakaria Yahya bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Mandeh ambaye alikuwa mwanahadithi, faqihi na mwanahistoria wa Kiirani. Alikuwa wa mwisho katika kizazi cha Ibn Mandeh na baada ya kupata elimu za zama zake alianza kufunza na kuandika vitabu. Mwanahistoria huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha Maisha ya Tabarani.

Abu Zakaria Yahya bin Muhammad

Siku ya leo miaka 483 iliyopita, ilianza harakati ya kiongozi wa kidini na mpenda mageuzi wa Ufaransa John Calvin huko Geneva mji mkuu wa Uswisi. Alizaliwa mwaka 1509 Miladia na kujifunza sheria na masomo ya kidini. Katika zama za ujana wake, John Galvin alijiunga na harakati ya Kiprotestanti iliyoasisiwa na Martin Luther. Aliivamia Geneva Uswisi kwa kusaidiwa na wafuasi wa Kiprotestanti na kujaribu kuasisi mfumo wa uongozi wa kidini katika jamii ya nchi hiyo kwa mujibu wa dhehebu la Protestanti. John Calvin pia alianzisha mfumo wa ideolojia ya Kikristo iliyojulikana kama Calvinism na kubainisha itikadi zake katika kitabu chake alichokiita" Institutes of Christian Religion."

John Calvin

Siku kama ya leo miaka 262 iliyopita, vilijiri vita vya kwanza kati ya vikosi vya Uingereza na India huko katika eneo la Bengali kaskazini mashariki mwa India. Waingereza walishinda vita hivyo na kulidhibiti eneo hilo ambalo katika zama hizo lilikuwa sehemu ya ardhi ya India. Waingereza ambao walianza kuingia nchini India miaka kadhaa nyuma kupitia East Indian Company, mbali na kuyarejesha nyuma majeshi ya India, katika vita vilivyofuata walimshinda pia hasimu wao mkubwa Ufaransa na kufanikiwa kuyatoa kabisa majeshi hayo katika ardhi ya India.

Vita vya Bengali

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, yaani sawa na tarehe 23 Juni 1939, Wafaransa waliikabidhi Uturuki bandari muhimu ya Iskenderun, eneo ambalo katika zama hizo lilikuwa sehemu ya ardhi ya Syria. Kwa miaka kadhaa kabla ya tukio hilo, Uturuki ilikuwa ikidai umiliki wa bandari hiyo. Hata hivyo baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, eneo hilo lilikabidhiwa Syria kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwa yamefikiwa baina ya Uingereza na Ufaransa. Hata hivyo baada ya kuangushwa utawala wa Othmania na kuchukua hatamu za uongozi nchini Uturuki, Mustafa Kamal Ataturk aliyekuwa na mielekeo ya Kimagharibi Ufaransa ambayo wakati huo ilikuwa ikiikalia kwa mabavu Syria, iliikabidhi Bandari ya Iskenderun kwa Uturuki. Hatua hiyo ilipelekea kuongezeka hisia za chuki dhidi ya Ufaransa nchini Syria na kuongeza mapambano dhidi ya mkoloni huyo. Hadi leo hii serikali ya Syria ingali inasisitiza kwamba, Bandari ya Iskenderun ni mali yake.

Bandari ya Iskenderun